loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Mimba ya mtoto darasa la nne inazua utata

WANDE Shija (siyo jina lake halisi) anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Ilobi iliyopo kijiji cha Ikonda, kata ya Mwaweja katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Shinyanga, amekuwa akitaja majina kadha wa kadha kuhusu mtu aliyempa mimba.

Binti hiyo mwenye umri wa miaka 13 alianza kwa kuwataja kaka zake watatu, kwamba ndio waliompa ujauzito na mara akabadilika na kumtaja mwalimu wake kuhusika na ujauzito huo.

Tukio hilo lilianza kwa mwanafunzi huyo na wenzake tisa wa madarasa tofauti tofauti kwenda kupimwa hali zao katika zahanati ya eneo hilo baada ya kuhisiwa kuwa na mabadiliko fulani fulani.

Msichana huyo alipowataja kaka zake watatu kwamba ndio wamempa mimba, waliwekwa chini ya ulinzi ambako hadi makala haya yanaandikwa walikuwa bado wanashikiliwa kwa mahojiano.

Majina ya kaka zake hao kwa sasa yanahifadhiwa.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, binti huyo alidai kwamba baada ya kuhisi ana mabadiliko, alimweleza babu yake aliyefariki dunia hivi karibuni huku mama yake na bibi yake wakiwa hawana habari lakini anadai kwamba babu yake huyo hakuchukua hatua yoyote baada ya kumweleza hali yake.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, amethibitisha kaka za binti huyo kushikiliwa huku akisema mmoja wa kaka zake hao aliwatoroka polisi na kukimbia na bado anasakwa.

Daktari wa zahanati ya Ikonda, Salome Salaganda anasema alipewa jukumu la kuwapima wanafunzi wote tisa lakini aliyebainika kuwa na mimba miongoni mwao ni mwanafunzi huyo wa darasa la nne.

“Vipimo vimeonesha kwamba ana ujauzito wa miezi minne,” anasema Magiligimba. Mama mzazi wa binti huyo ambaye hajui kusoma wala kuandika, anasema ana watoto saba na kwamba binti yake huyo ni watano kuzaliwa.

“Mimi kwa kweli ninashangaa sana kuelezwa kuwa mwanangu ni mjamzito,” anasema na kuwa na wasiwasi kama kweli binti yake ni mjamzito.

Mama huyo anasema amekuwa akiishi na mwanawe na siku zote haonyeshi dalili zozote za kuwa na ujauzito na kwamba hata chakula alikuwa habagui wala kutapika kama ilivyo kwa wajawazito.

Lakini anakiri kwamba katika siku za karibuni aliona mwili wa Wande ukiongezeka na yeye akaamini binti yake ananenepa. Mama huyo (jina linahifadhiwa) haamini kama wanawe wa kiume wanaweza kuwa wanahusika na ujauzito wa dada yao na hajui ni kwa nini Wande aliamua kuwataja.

Alipoulizwa anamtuhumu nani anayeweza kuwa kampa mimba binti yake, mama huyo anadai ni mwalimu wake na kwamba anahisi amelazimishwa na walimu kuwataja ndugu zake ili kumwokoa mwalimu.

“Ninawatuhumu walimu kwa sababu alipokuwa anachelewa kurudi nyumbani, nikimuuliza ananiambia alikuwa ametumwa na walimu kufanya kazi,” anasema.

Anasema yeye ni mke wa pili na kwamba mara nyingi mume wake yuko kwa mke wake mkubwa na kwamba huja mara moja moja kuangalia familia yake.

Wakati mwandishi wa makala haya anazungumza na mama huyo, baba wa mtoto alikuwa hajapata habari kuhusu ujauzito wa binti yake na tuhuma dhidi ya vijana wake wa kiume.

Bibi wa binti huyo, Elizabeth Charles, anakataa kata kata madai kwamba Wande anaweza kuwa kapewa ujauzito na kaka zake.

“Nakataa, hilo haliwezekani,” anasema bibi huyo.

Baadhi ya majirani wa familia hiyo, Asha Juma na Dolnad Kulwa wanasema hawana imani na mmoja wa kaka wa Wande kutokana na tabia zake.

“Sina hakika kwa asilimia 100 lakini mmoja wa wale kaka zake tunasikia alishawahi kumpa ujauzito dada yake na walipoona ni kitendo cha aibu wakaenda kuitoa hiyo mimba,” anasema Asha na kuongeza kwamba mama yake Wande hawezi kukiri hilo kwa sababu ya kuona aibu.

Suzan Mososa ambaye ni jirani mwingine wa akina Wande anasema mazingira anayoishi binti huyo mdogo yanaweza kuchangia hali hiyo.

“Dada zake wakubwa aliwapeleka kwa bibi yao anayeishi kitongoji kingine ila huyu binti walimuacha hapa nyumbani huku mazingira ya nyumba yao ni ya chumba kimoja na sebule na vijana wa kiume wanalala humo humo ndani. Unaweza kuona hali ilivyo hatari,” anasema Suzan.

Mtendaji wa kata ya Mwaweja, Hapi Chonde, anasema baada ya kusikia tukio la mwanafunzi huyo kupewa ujauzito, alianza kushirikiana na uongozi wa shule kwa kumwita mzazi wa mwanafunzi huyo pamoja na mwanafunzi mwenyewe kuja kutoa maelezo.

“Lakini hawakuja mpaka tukatumia nguvu baada ya siku mbili kupita ndio wakaja. Lakini maelezo ya mtoto yanakanganya.

Mara ya kwanza alivyoulizwa na walimu aliwataja ndugu zake ambao mpaka sasa wanashikiliwa na jeshi la polisi na mmoja kakimbia lakini alipokuja siku ya pili akatoa maelezo tofauti na kumtaja mwalimu aliyekuwa anakaimu uongozi hapo shuleni,” anasema mtendaji wa kata.

Chonde anasema mwanafunzi huyo anaonekana kufundishwa maneno na familia yake kwani viongozi walipokwenda na polisi mama alimficha mtoto chini ya magunia ya michembe na kuwaeleza hayupo nyumbani na kwamba hajui alipokwenda.

Anasema polisi walipoamua kufanya msako ndani wakamkuta kachutama huku kafunikwa na gunia.

Mratibu Elimu katika Kata ya Mwaweja, Peace Rweyemamu anasema wao ndio waliishauri shule kupima wasichana baada ya taarifa kuhusu ujauzito wa mwanafunzi huyo kuwafikia.

Anasema walimu walikaa kikao na wanaharakati hao kujadiliana namna ya kupata vipimo ili mwanafunzi aliyekuwa akituhumiwa asiweze kugundua nini kinaendelea na ndipo alipochanganywa na mabinti wenzake kwenda kupimwa katika zahanati hiyo ya kijiji na kubainika kuwa ni mjamzito.

Rweyemamu aliyeshiriki kwenye mahojiano baina ya mwanafunzi na walimu, anasema mara ya kwanza aliwataja kaka zake akiwemo aliyekimbia kuhusika na ujauzito wake.

“Ninavyoona huyu mwanafunzi kafundishwa na familia yake aseme uongo kumsingizia mwalimu ambaye ana familia yake hapo shuleni.

Huyu mwalimu ndiye anasimamia nidhamu kwa watoto wote na ni mkali asiyetaka mzaha kwa wanafunzi hasa wanaochelewa,” anasema Rweyemamu.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ilobi, Musa Masunga alipofuatwa kusikia maelezo yake alikiri mwanafunzi wake huyo kudhihirika kuwa na ujauzito lakini akasema hawezi kulizungumzia kiundani suala hilo mpaka apate idhini kutoka kwa mwajiri wake, yaani mkurugenzi wa halmashauri.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Joseph Makwaya, anasema suala hilo bado linajadiliwa na kamati kwa vile hata mwalimu ametajwa lakini anasema hawezi kulieleza kiundani kwa sasa.

Katibu wa vituo vya taarifa na maarifa vilivyojengewa uwezo na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) wilayani Kishapu, Peter Nestori, anasema siku hizi kesi nyingi za kuwapatia ujauzito watoto wenye umri mdogo zinatoka ndani ya familia.

Anasema tatizo linakuwa kubwa likichangiwa na wazazi kuwakataza watoto kusema ukweli. “Hii ni kesi ya tatu ambayo ndugu wanatajwa kuhusika na ujauzito wa mtoto katika kipindi kifupi. Hii ni hatari sana,” anasema.

 

Itaendelea

foto
Mwandishi: Kareny Masasy, Shinyanga

1 Comments

  • avatar
    George Naganye
    17/11/2020

    Upelelezi uendelee mpaka pale watakapomta mhusika na sheria ifanye kazi yake

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi