loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Balozi wa Poland atunukiwa cheti kwa ujuzi wa Kiswahili

BALOZI wa Poland hapa nchini, Krzysztof Buzalski, amesema lugha ya Kiswahili imemsaidia kuwasiliana na Watanzania kwa urahisi na kufanya kazi zake za kidiplomasia kwa wepesi hususani maeneo ya vijijini.

Aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kumtunuku cheti cha utambuzi wa ujuzi wa Kiswahili kwa wageni.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Bakita, Dk Method Samwel alimpongeza Balozi Buzalski kwa uamuzi wake wa kujifunza Lugha ya Kiswahili na kufaulu vizuri kwani uamuzi huo siyo tu kwamba unamwezesha kufanya kazi kwa urahisi na Watanzania, bali pia anakuwa sehemu ya familia ya Watanzania.

“Siyo rahisi kupata Balozi hasa wa Ulaya kujifunza Kiswahili kwa muda wote huu kutokana na shughuli nyingi walizonazo, juhudi kubwa aliyofanya siyo tu kwa faida yake binafsi lakini pia kwa mahusiano mazuri ya kidiplomasia.

“Alitenga muda wake na ameweza kufaulu kwa kiwango cha juu, tunamwomba Balozi atusaidie kufikisha ujumbe kwa Mabalozi au Wanadiplomasia wenzake kwamba waje wajifunze Kiswahili,”alieleza Dk Samwel.

Ili Tanzania iwe kama nchi zingine ikiwemo China na Ujerumani ambazo sera na sheria zao zinawataka wageni kujifunza Kichina au Kijerumani, Dk Samwel alisema huu ni muda mwafaka kwa Tanzania nayo kuwa na sera na sheria itakayowataka Wanadiplomasia au kampuni za kigeni zinazokuja kufanya kazi hapa nchini kujifunza Lugha ya Kiswahili kwa kuwa walimu wapo wazuri na watajifunza kwa muda mfupi.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi, alisema Balozi Buzalski alifaulu mtihani wa Kiswahili kwa wageni katika hatua ya tatu kiwango cha kati kwa daraja A. Alisema ufaulu huo ni sawa na C1 kwa viwango vya upimaji vya Ulaya.

Consolata alisema katika mtihani wa kusikiliza Balozi Buzalski alipata alama A, kuzungumza alama B, kusoma alama A na kuandika alama B.

"Mitihani yetu ni ya hatua tatu, yaani hatua ya awali, kati na juu. Kwa hatua zote kuna kiwango cha chini, kati na juu. Mtunukiwa alionesha ujuzi wa kiwango cha juu na hivyo aliandaliwa mitihani ya hatua ya juu," alisema Consolata.

Baada ya kutunukiwa cheti hicho, Balozi Buzalski alisema Kiswahili kimemsaidia kuwasiliana na Watanzania kwa urahisi na kufanya kazi zake za kidiplomasia kwa wepesi, kupata habari za Kiswahili kuhusu Tanzania kila siku na kujua utamaduni wa Watanzania.

“Niliamua kujifunza Kiswahili kutokana na sababu mbili, kwanza nilijua Rais John Magufuli alitoa mwito kwa wageni waongee lugha hii, pili nilifikiri kwamba kujua lugha ya wenyeji wa Tanzania itanisaidia kufanya kazi yangu, ni suala la muhimu kwa Wanadiplomasia kuongea lugha ya wenyeji,”alisema Balozi na kuongeza:

“Mara nyingi nilipoenda vijijini nilipata shida kuwasiliana katika Kiingereza, lakini sasa ninapozungumza nao kwa Kiswahili wanafurahi sana, kujua Kiswahili ni ufunguo wa utamaduni wa asili ya Tanzania kwa kuwa Kiswahili siyo lugha tu, bali pia ni njia ya kufikiri na kuburudika.”

Balozi Buzalski alisema alianza kujifunza Kiswahili tangu mwanzoni mwa mwaka 2017 hadi Oktoba mwaka huu.

Alikuwa akijifunza mara mbili kwa wiki ubalozini kwake chini ya Mwalimu Joshua Mshani, hivyo aliishukuru Bakita kwa kumpatia mtihani ambao amefaulu vizuri.

Rais wa Tanzania Dk John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi