Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi amewataka wafanyabiashara kutoka Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kuwekeza visiwani Zanzibar.
Dk Mwinyi amebainisha hayo hii leo Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na wajumbe wa Jumuiya hiyo wakiongozwa na kiongozi wao, Sheikh Tayabali Patanwalla.
Amesema Zanzibar ina fursa nyingi zinazoweza kuwekezwa katika sekta mbalimbali za maendeleo, hivyo amewataka wajumbe hao ambao wengi wao ni wafanyabiashara watumie fursa hizo ili zitengeneze ajira kwa vijana.
“Niwapongeze kwa namna mnavyoiunga mkono serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo hasa kwa kutoa huduma za afya na elimu” amesema Dk Mwinyi.
Amesema serikali anayoiongoza itaendelea kushirikiana na madhehebu mbalimbali visiwani humo kuhakikisha kunakuwepo mashirikiano ya pamoja kwa lengo la kuimarisha sekta za maendeleo.