loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dhamira ya Wizara kufufua kilimo cha kahawa

WIZARA ya Kilimo Tanzania inakusudia kufufua zao la kahawa nchini kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) ndani ya kipindi kifupi kijacho.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gelard Kusaya, alipokwenda kukagua mradi wa vitalu vya kuzalisha miche ya kahawa unaotekelezwa na TaCRI katika wilaya za Butiama na Tarime mkoani Mara, Ijumaa iliyopita.

“Wizara ya Kilimo kupitia TaCRI tuna jitihada za makusudi za kuzalisha miche mingi ya kahawa kadri inavyowezekana na lengo ni kuzalisha maradufu,” anasema Kusaya.

Anasema wizara inawahusisha wakuu wa mikoa inayozalisha kahawa ili wasaidie kuhamasisha wakulima kujikita katika uzalishaji wa zao hilo la biashara.

Kusaya anasema, wizara hiyo itahakikisha wakulima wanapata miche bora ya kahawa kupitia TaCRI popote walipo nchini kila wanapoihitaji na kwamba, soko la zao hilo kwa sasa ni kubwa.

Mkurugenzi wa TaCRI, Deus Kilambo, anasema taasisi hiyo imefanya mapinduzi makubwa ya kuzalisha miche ya kahawa kwa njia ya vikonyo na mbegu chotara.

“Hata lengo ambalo tumepewa la kuzalisha miche 340,000 kwa wilaya ya Butiama tutalimudu,” Dk Kilambo anasema hayo akimweleza Katibu Mkuu, Kusaya.

Anasema TaCRI itaendelea kutoa mafunzo na matokeo ya utafiti kwa wakulima ili kuharakisha mpango wa kufufua kilimo cha kahawa nchini.

Kwa mujibu wa Kilambo, TaCRI imeweka mkakati kabambe wa miaka mitatu wa kuzalisha na kusambaza kwa wakulima miche ya kahawa milioni 23.

Mkakati huo unalenga mikoa 18 ambayo ni Mara, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Rukwa, Katavi, Kagera, Mwanza, Geita na Kigoma.

Hivi karibuni, TaCRI ilitumia maadhimisho ya Siku ya Mara kwenye viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama kuelimisha wakulima mintarafu teknolojia bora za uzalishaji wa miche na uanzishaji mashamba ya zao hilo.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika sambamba na maonesho ya kilimo, maofisa wa TaCRI walielimisha wakulima faida za mashamba mseto ya mazao ya kahawa na migomba.

“Kuhusu uzalishaji wa miche ya kahawa, tumeelimisha wakulima teknolojia za kuzalisha kwa njia ya vikonyo na kutumia mbegu,” anasema Meneja wa TaCRI Kanda ya Ziwa - Kituo cha Sirari, Almas Hamad Mshihiri, katika mahzungumzo na HabariLEO katika viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama.

Akizungumzia uanzishaji wa mashamba ya kahawa, Mshihiri anasema walijikita kuelimisha wakulima jinsi ya kuandaa na kuendesha kilimo mseto cha kahawa na migomba.

Mkulima kutoka wilayani Butiama, Martin Keng’eta, anasema teknolojia bora aliyojifunza katika banda na kitalu cha TaCRI imemwongezea ari ya kujikita katika kilimo cha mashamba mseto ya mazao hayo.

Kwa mujibu wa Mshihiri, kilimo cha mashamba mseto ya kahawa na migomba kinamwezesha mkulima kutanua wigo wake wa kiuchumi.

“Mkulima anapolima shamba mseto la kahawa na migomba, huvuna ndizi kwa ajili ya chakula na kuuza, ambapo mauzo ya ndizi yanamsaidia gharama za kutunza shamba lote, huku kahawa ikibaki kuwa zao la biashara moja kwa moja,” anasema Mshihiri.

KAHAWA AINA YA ARABIKA

Kahawa inayosisitizwa katika mkakati wa sasa ni aina ya ‘arabika’ inayosifiwa na wataalamu na hata wakulima kwamba mauzo yake ni ya juu katika soko la dunia.

Wakulima wa kahawa, Boniface Sagamo na Grace Magesa kutoka wilayani Tarime MKOANI Mara wanasema arabika inayozalishwa mkoani humo inapendwa na wateja wengi katika soko la dunia kutokana na ladha yake tamu.

“Kahawa aina ya arabika inayozalishwa hapa mkoani Mara ni ya ubora wa daraja la kwanza na la pili katika soko la dunia, na hata Mzungu akifika huku ananunua arabika iliyokobolewa kuanzia Sh 7,000  kwa kilo moja na kuendelea,” anasema Sagamo.

Meneja wa TaCRI Kanda ya Ziwa, Mshihiri, anasema kuna aina 19 mpya za mbegu za arabika zinazotiliwa mkazo katika kilimo cha kahawa kutokana na uwezo wake wa kutoshambuliwa na magonjwa.

“Lakini pia aina hizi mpya za arabika zinakomaa kwa muda mfupi; ni kati ya miezi 12 na 18,” anafafanua.

KITALU CHA MICHE

Katika kuimarisha uhamasishaji wa kilimo hicho Kanda ya Ziwa, TaCRI imeanzisha kitalu cha kudumu kwenye viwanja hivyo vya Mama Maria Nyerere, chenye uwezo wa kuzalisha miche bora ya kahawa 200,000 kwa mwaka.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anna-Rose Nyamubi, anasema kitalu hicho kimewekwa kwenye eneo sahihi kwani viwanja hivyo vimetengwa na serikali kwa ajili ya maonesho ya kilimo.

Mshihiri anasema TaCRI itashirikiana na halmashauri za wilaya, miji na jiji katika uzalishaji huo na wataalamu wa kilimo wameelekezwa kuhamasisha wakulima kuandaa mashamba husika.

Kwa mujibu wa meneja huyo, miche 15,000 ya kwanza itakayozalishwa kwenye kitalu hicho itatolewa bure, baadaye wakulima watatakiwa kuchangia gharama kidogo.

“Lakini kwa sasa tunashirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania kupata miche milioni moja kwa ajili ya kuigawa bure kwa wakulima mkoani Mara,” anasema.

ASEMAVYO MKUU WA MKOA

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mara na maonesho ya kilimo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, anasema serikali itashirikiana na TaCRI kuuwezesha mkoa huo kuongoza kwa uzalishaji mkubwa wa kahawa aina ya arabika nchini.

“Nataka Mkoa wa Mara uongoze kwa uzalishaji wa kahawa hii na katika hili tunaitagemea TaCRI, tuzalishe zaidi kahawa yenye ubora wa kimataifa, watu watoke mataifa mengine kuja kuinunua huku.”

“Hiki kitalu cha kuzalisha miche ya kahawa kilichoanzishwa na TaCRI nataka kiwe darasa namba moja, wakulima waje kujifunza hapa,” anasema Malima.

Awali, Malima aliwahimiza wananchi mkoani Mara kutumia maadhimisho hayo kujifunza teknolojia na kanuni bora za kilimo, lakini pia kuongeza juhudi za kutunza mazingira na ikolojia ya Mto Mara.

“Maonesho haya yana umuhimu wa pekee katika mkoa wetu wa Mara, ninawaomba wananchi tuyatumie kujifunza kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali,” anasema Malima.

Anaongeza: “Tunakumbushwa pia kutunza mazingira na ikolojia ya Mto Mara… ninataka maonesho haya yawe kichocheo cha kiuchumi na kijamii mkoani kwetu.”

Mkuu wa Mkoa wa Mara anawashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kushiriki maadhimisho hayo kwa kujenga mabanda ya maonesho ya bidhaa zao wakiwamo TaCRI, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria na Ofisi ya Maji Bonde la Mto Mara.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa alimshukuru mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere kwa kukubali viwanja vya maonesho hayo ya kilimo kupewa jina lake.

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: Christopher Gamaina

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi