loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Umuhimu wa takwimu sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuandaa mipango mbalimbali ya muda mfupi na mrefu inayolenga kuimarisha uchumi na kupunguza umaskini.

Utekelezaji wa mipango hiyo, umeongeza mahitaji ya takwimu bora kwa ajili ya kufuatilia, kutathmini na kupima mafanikio yanayopatikana.

Kati ya mambo muhimu yaliyopangwa kufanyika katika programu za kuimarisha uchumi na kupunguza umaskini, ni pamoja na kufanyika kwa sensa ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kupima mafanikio na maendeleo katika sekta ya kilimo ili kuendelea kuimarisha uchumi wa kipato cha kati unaotegemea viwanda.

Kwa mujibu wa Ilani  ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 Sura ya  Kwanza, Sehemu ”C”,  Serikali italeta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika  wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote sambamba na  kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.

Katika kipengele cha kwanza, Ilani imesisitiza kuhakikisha uzalishaji  unaongezeka katika mazao ya chakula, mifugo na uvuvi kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula na lishe bora.

Kipengele cha pili kinasisitiza kuongeza tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuchochea maendeleo ya uchumi hasa katika sekta za viwanda na huduma.

Katika muktadha huu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inasema takwimu zilizokusanywa katika sensa ya  mwaka huu, 2020  zitatumika kupima na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuendeleza sekta ya kilimo mifugo na uvuvi.

Tathmini hiyo ni muhimu kwa kuwa itawezesha kufahamu maeneo ambayo nchi imefanya vizuri na yale ambayo bado yanahitaji kuwekewa juhudi zaidi.

“Takwimu hizo mbali ya kuonesha tulikotoka, tuko wapi, pia zitatuonesha kule tunakotaka kwenda kutimiza malengo ya Taifa ya kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi,” anafafanua Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa, alipokuwa mkoani Singida hivi karibuni kukagua kazi ya ukusanyaji wa takwimu hizo.

Anasema kwa mara ya kwanza, Sensa hii imefanyika kwa kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya kiteknolojia hasa ile ya kidigitali, ambayo imeboresha usahihi wa takwimu na kupunguza gharama ya kuzikusanya kwa kwa kiwango kikubwa.

Dk Chuwa anaongeza: ”Hivyo kwa kweli tunajivunia kwamba Taasisi yetu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu iko mstari wa mbele si tu katika kuhakikisha Taifa linakuwa na takwimu sahihi, bali hata katika jitihada za kitaifa za kuhakikisha nchi inaingia na inanufaika na uchumi wa kidigitali”.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk Anjelina Lutambi anasema sensa ya  takwimu ni kitu mumimu kwa kuwa kinawezesha kufanya tathimini kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa na kwamba, takwimu sahihi zilizokusanywa kutoka kwenye sekta mbalimbali za kimkakati za mifugo, kilimo na uvuvi nchini zimeifanya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais John Magufuli kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati duniani.

Dk Lutambi anasisitiza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Msikii katika Kata ya Mghano  mkoani Singida kwamba, madhumuni makuu ya sensa inayofanyika mwaka huu ni kupata taarifa muhimu za kilimo, mifugo na uvuvi zitakazotumika kupanga na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta nchini  Tanzania.

Anasema ukusanywaji wa takwimu huuu ukiwa katika ubora unaositahili, utasaidia kulifanya taifa kupaa kwenda uchumi wa juu kabisa katika kipindi kifupi kijacho.

Anafafanua akisema, taarifa za magonjwa ya mifugo na mazao zitaisaidia serikali kuainisha maeneo yanayokabiliwa na visumbufu /magonjwa ili kuchukua hatua stahiki na kupanga mipango ya kudhibiti.

Aidha, taarifa kuhusu uzalishaji wa mazao zitasaidia kujua kiasi cha uzalishaji kwa maeneo husika na kuiwezesha Serikali kupanga upatikanaji wa masoko na uwezekano wa kuanzisha viwanda vya kusindika mazao hayo.

Aidha, Dk Lutambi anasema, taarifa kuhusu upatikanaji na matumizi ya ardhi zitatumika kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini hivyo zitatumika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

Kwa upande wake, Dk Chuwa anatanabaisha kuwa, matokeo ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanatarajiwa kuweka msingi imara wa sekta hizi kwa miaka mingi iyajo.

Anasema hii ni kwa  kuwa sekta ya kilimo ina umuhimu mkubwa  katika mustakabali wa maisha ya binadamu kwa kuwa ndiyo chanzo cha chakula na malighafi zinazohitajika katika viwanda hususani katika awamu hii inayoongozwa na dira ya uchumi wa viwanda.

“Kutokana na umuhimu huo, na kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya Mwaka 2030, sekta ya kilimo ilipewa Lengo la Pili  la Kutokomeza Njaa, Kuwa na Uhakika wa Chakula, Lishe Bora na Kukuza Kilimo Endelevu,” anasema Dk Chuwa.

Anaongeza: “Aidha, lengo hilo limesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao na pia, kusisitiza matumizi bora ya ardhi na kurutubisha udongo, ili kuongeza uwezo wa binadamu kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi na athari zake yakiwemo majanga mbalimbali kama mafuriko na ukame pamoja na majanga mengine ikiwemo ndege waharibifu.”

Anasema pamoja na faida za jumla ambazo mkulima atakazozipata, sensa hii itamsaidia mtu mmoja mmoja kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo, mifugo na uvuvi hasa upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Ni muhimu tukafahamu kuwa takwimu sahihi za mifugo, mazao na uvuvi zitasaidia uchangiaji wa malighafi za viwanda vyetu hivyo kukuza uchumi wetu ambao tunautaka wa viwanda,” amesisitiza Dk Chuwa.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Mohamed Bashe, alisema katika ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi wa sensa ya kilimo, mifugo na uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, iliyofanyika katika  jijini Mwanza Julai, 25 mwaka huu kwamba Mwaka huu 2020, Benki ya Dunia (WB) imeitangaza Tanzania kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati.

Alisema taarifa hizi zimeleta faraja kubwa kwa sekta ya kilimo kwa kuwa ndiyo iliyotoa mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa wa asilimia 26.6 mwaka 2019 na pia inatoa ajira kwa takribani asilimia 66 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi.

“Sekta ya kilimo ilichangia asilimia 24.3 ya mapato ya mauzo nje ya nchi mwaka 2019. Fedha hizi kwa kiasi kikubwa zinatumika nchini katika mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi ya barabara, reli, maji, usambazaji umeme na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za jamii kama vile afya na elimu kili kuimarisha maendeleo ya wananchi,” anafafanua Bashe.

Anaongeza kuwa, kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Umasikini Tanzania Bara ya Mwaka 2018, sekta hii ikiendelezwa vyema, ndiyo pekee yenye uwezo wa kuleta maendeleo jumuishi nchini, hivyo  kuna umuhimu mkubwa wa zoezi la sensa ya mifugo, mazao na uvuvi likafanyika kwa ubora na kwa umakini unaositahili.

Katika ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi wa sensa hii, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk Amina Msengwa, anasisitiza kuwa takwimu zina mchango mkubwa katika maandalizi na utekelezaji wa sera na mipango, na katika kufanya uamuzi sahihi unaotakiwa kufikiwa kwa kutumia ushahidi stahiki.

Amesema Sensa ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, ni ya tano kufanyika nchini tangu nchi ipate uhuru.

Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo, anaishukuru Serikali ya Mkoa wa Singida kwa kusaidia kufanikisha kazi hiyo iliyofanyika kwa takribani siku 50 na anawapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano wa kutosha.

Kipuyo anasema taarifa zilizokusanywa kupitia sensa hii ni za kipindi cha kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi 30 Septemba 30, 2020 na kuongeza kuwa, Mkoa wa Singida umekamilisha kazi hiyo kwa maeneo.

Anafahamisha kuwa, kaya 1087 katika maeneo madogo 90 ya kuhesabia zilizochaguliwa kwa ajili ya kufanyiwa sensa hii, zilifikiwa.

John Mapepele ni Ofisa Habari wa Mkoa wa Singida. Anapatikana kwa 0784441180

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi