loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watanzania sasa wanalipa kodi, wanaiona na kuifaidi

SERIKALI ya Awamu ya Tano inatajwa kama iliyoimarisha ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi. Hivyo kumekuwa na ongezeko kubwa la mapato ya ndani.

Ongezeko hilo limetokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji kwenye taasisi, mashirika na kampuni kulikoiwezesha serikali kupata michango na gawio stahiki kutoka katika uwekezaji wake.

Aidha, serikali imeimarisha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye wizara na idara zinazojitegemea kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato uitwao ‘Government Electronic Payment Gateway (GePG)’

Kati ya Julai 2017 hadi Novemba 2018 kwa mfano, taasisi za serikali 325 zimeingia katika matumizi mfumo huo kukusanya maduhuli.

Hali kadhalika, kumekuwa na jitihada za kuweka mazingira mazuri kufanya biashara ambapo serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018/19, ilipunguza ada na tozo mbalimbali zilizokuwa kero kwa wananchi. Miongoni mwa ada na tozo zilizopunguzwa ni pamoja na tozo za mazingira, OSHA, FIRE, TBS, TFDA na tozo kwenye madini ya chumvi.

Aidha, serikali imeanzisha vituo vya utoaji huduma mahali pamoja (One Stop Centres) katika maeneo ya mipakani ili kurahisisha na kupunguza gharama za biashara, na tovuti mpya imeanzishwa ili kupunguza gharama na kuwezesha wawekezaji kupata huduma kwa urahisi na haraka.

Taarifa zinaonesha kuwa, vituo hivyo vimeongeza makusanyo ya mapato ya serikali. Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuongeza mapato, zipo changamoto nyingi ambazo bado zipo na zinakwamisha juhudi hizo.

Changamoto hizo ni pamoja na ukwepaji wa kodi, misamaha ya kodi isiyokuwa na tija, usimamizi mbaya wa ukusanyaji wa kodi, wigo mdogo wa walipakodi na mwamko mdogo wa wanunuzi kudai risiti na wauzaji kutoa risiti.

Kwa mfano, TRA imefichua mbinu sugu za ukwepaji wa kodi. Mbinu hizo ni: mosi, matumizi ya risiti za kughushi za kielektroniki (EFD); pili, kutumia risiti moja halali kwa bidhaa na huduma kwa ajili ya muamala zaidi ya mmoja na tatu, kutoa risiti zenye kuonesha taarifa zenye upungufu badala ya mauziano sahihi.

Mbinu nyingine chafu ya kukwepa kodi ni wafanyabiashara kutotoa risiti kabisa na tano ni wafanyabiashara kuwapa wateja risiti zilizo tofauti na manunuzi ya siku husika huku wengine wakitumia nakala za barua walizoiandikia TRA taarifa kuwa mashine ni mbovu hivyo, kutuimia risiti za kawaida.

Kama serikali inataka kuongeza mapato ya ndani, hayo ndiyo maeneo ya kuendelea kushughulikia kwa kubwa zaidi.

KUNUFAIKA NA RASILIMALI

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa ikipambana na mikataba mibovu ambayo serikali ya awamu zilizopita iliingia na kampuni mbalimbali za uwekezaji.

Kampuni hizo zimekuwa zikifanya udanganyifu mkubwa kimapato kwa kukwepa kodi mbalimbali za serikali na utoroshaji wa madini na mitaji.

Aidha, kampuni hizo zilifanya uharibifu wa kutisha wa mazingira na uporaji wa ardhi ya wananchi wa vijiji ambako rasilimali za madini zilipatikana. Ili kukabiliana na uporaji na dhuluma hiyo, serikali ya awamu ya tano, imetunga sheria za kulinda rasilimali za madini ili nchi inufaike na rasilimali zake.

Vilevile, serikali imeweka na kusimamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi, kuhamasisha uzalishaji na upatikanaji wa masoko ya madini na kukomesha utoroshaji wa madini kwenda nje na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba katika mazingira bora zaidi huku wakilipa kodi.

Serikali imeweka wakaguzi wa madini katika migodi yote mikubwa nchini ili kuhakiki kiasi na thamani ya madini yanayozalishwa na kuuzwa nje ya nchi na migodi inafahamika.

Aidha, serikali imeanzisha minada na maonesho ya madini ili kuhakikisha madini yananunuliwa kwa bei ya ushindani. Hatua hii inahakikisha kwamba serikali inapata mrabaha stahiki.

Pia, serikali imefanya mazungumzo na kampuni ya Barrick na wamekubaliana kwamba nchi itapata hisa asilimia 16 na mgawanyo wa asilimia 50/50 wa faida na mipango iko mbioni kufanya mazungumzo katika maeneo mengine kama tanzanite na almasi.

Rais John Magufuli alisitisha usafirishaji wa mchanga wenye madini (makanikia) nje ya nchi ili kudhibiti wizi na uporaji wa madini.

Matokeo yake, hadi mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 194 hadi Sh bilioni 301 kwa mwezi.

Pia, ujenzi wa ukuta Mirerani umewezesha mapato kuongezeka kutoka Sh milioni 71 hadi Sh bilioni 1.3. Kama hiyo haitoshi, serikali imekuwa ikiendesha mazungumzo na wadau mbalimbali ili kubaini mianya ya utoroshaji wa madini na kisha kuifanyia kazi.

MUHIMU KUFANYIA KAZI

Matokeo ya juhudi zote hizo ni kwamba, kwa jumla mapato yameongezeka yakiwamo mapato ya baadhi ya mashirika yaliyofufuliwa.

Kwa mfano, mapato ya Dawasa yameongezeka kutoka Sh bilioni 32 kwa mwaka hadi Sh bilioni 120 kwa mwaka na yale ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari  Tanzania(TPA) kutoka Sh milioni 700 kwa mwaka hadi Sh milioni 850 kwa mwaka.

Kwa kuwa mapato ya mashirika hayo yameongezeka ni wazi kuwa serikali itapata gawio lake na hivyo kuongeza mapato yaserikali.

Kwa jumla, serikali imefanikiwa kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 9.9 mwaka 2015 mpaka Sh bilioni 15 mwaka 2018.

Kama hiyo haitoshi, katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza (Julai - Novemba) ya mwaka 2018/19, makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yalifikia Sh trilioni 7.37 sawa na Sh trilioni 1.474 kwa mwezi au Sh trilioni 17.688 kwa mwaka.

Hii ina maana kwamba, tukiongeza juhudi zaidi tunaweza kufikia Sh trilioni 20 kwa mwaka ambayo itakuwa asilimia 63 ya bajeti ya mwaka 2018/19.

Haya ni mafanikio makubwa sana ambayo mtu hahitaji kuvaa miwani ili ayaone. Tukitambua hivyo, ni vyema tukakiri kwa midomo yetu kwamba serikali imefanya mambo makubwa na ndiyo maana manufaa mengi yanaonekana ukiwamo ujenzi wa miundombinu mbalimbali wezeshi ya kiuchumi, uimarishaji wa huduma za kijamii kama elimu, afya na maji na uanzishwa na uimarishaji wa kampuni na miradi mbalimbali ya kiuchumi.

MATUMIZI YASIYO NA TIJA

Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikikabiliwa ‘kansa’ ya malipo hewa ambayo ilikuwa inatafuna mabilioni ya mapato ya serikali.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imedhibiti aina mbalimbali ya malipo hewa.

Kwa mfano, serikali imewaondoa katika mfumo wa malipo wafanyakazi hewa takriban 20,000 na kuokoa Sh bilioni 238 kwa mwaka.Huu ni uamuzi na utendahji ulioleta tija kwa taifa.

Halikadhalika, takribani wafanyakazi 2,000 wenye vyeti feki wameondolewa katika mfumo na serikali na hivyo kuokoa Sh bilioni 142.9 kwa mwaka.

Awali, serikali ilikuwa inalipa Sh bilioni 700 kwa ajili ya mishahara kwa mwezi, lakini kwa sasa inalipa Sh bilioni 250.

Serikali pia ilifuta sherehe mbalimbali za kitaifa na kuokoa mabilioni ya fedha ambazo zimeelekezwa kwenye mahitaji maalumu. Vilevile, serikali ilihakiki madeni yote na kufanikiwa kuondoa madeni hewa.

Matumizi yasiyo ya lazima Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujasiri mkubwa imefanikiwa pia kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima.

Maeneo yaliyoguswa ni pamoja na kupunguza au kufuta kabisa safari holela za mara kwa mara na za muda mrefu zilizojumuisha idadi kubwa ya washiriki ndani na nje ya nchi na badhi ya sherehe mbalimbali za kitaifa.

Vingine vilivyoangaliwa ni posho za vikao zisizostahili, vyakula na vinywaji vya anasa wakati wa vikao, vikao kufanyika nje ya kumbi za taasisi za umma ndani na nje ya nchi na manunuzi ya samani za ofsini na vitu vingine vya anasa nje ya nchi.

Kwa mfano, matumizi ya safari za nje kwa viongozi na maofisa yameshuka kutoka Sh bilioni 216 mwaka wa fedha 2014/15 mpaka Sh bilioni 25 tu kipindi cha miaka miwili ya fedha 2015/16 - 2016/17.

Kimsingi, mianya imezibwa sana ya ufisadi na wizi wa mali ya umma, huduma za kijamii zinaimarishwa.

Tazama sasa hata barabara za mitaani katika miji mingi zinajengwa kwa kiwango cha lami, huduma za afya zinazidi kusambaa na kuwanufaisha wengi zaidi, miundombinu ya usafiri ukiwamo wa ndege na reli umefufuliwa na kuzaliwa upya.

Tazama hata ujenzi wa reli ya kisasa na idadi ya ndege za Tanzania. Elimu bila malipo kuanzia msingi hadi sekondari, ni miongoni mwa mambo yanayoonesha kuwa, Serikali ya Awamo ya Tano inazitendea haki kodi za Watanzania.

Kimsingi, hata ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (SGR) unaoendelea nchini ukikamilika, utaongeza kasi ya

kukua kwa uchumi wa nchi na kuongeza mapato kwa watu na taifa kwa jumla.

 

Mwandishi ni mchumi. Aliwahi kufanya kazi katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa. Kwa sasa ni mshauri binafsi wa masuala ya uchumi, hususani katika eneo la diplomasia ya uchumi. Anapatikana kwa 0754 487 985

TANGU mwishoni mwaka jana 2020, ...

foto
Mwandishi: Prof. Kitojo Wetengere

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi