loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mali nyingine Ushirika za bil 3.3/- zarejeshwa

WIZARA ya Kilimo imesema kazi ya kuzitambua mali za vyama vya ushirika zinazomilikiwa isivyo halali ni endelevu kwa kuwa baadhi ya waliokuwa watumishi wa vyama hivyo na wengine waliopo sasa wameendelea kuzificha.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerald Kusaya aliyasema hayo jana wakati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akimkabidhi hati saba za viwanja vinavyomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (Shirecu) na mali zingine zenye jumla ya thamani ya Sh bilion 3.3.

Baada ya Telack kumkabidhi hati hizo, Kusaya alisema kazi hiyo imefanywa kwa ujasiri mkubwa na kila upande umetendewa haki.

“Nitahakikisha mali zote zinarudi kwani hivi sasa tumeanzia na vyama vya ushirika vitatu ambavyo ni Nyanza, Shirecu na KCU na vyama vingine vijiandae na zoezi hili ni endelevu na ushirika unatakiwa ujiendeshe kibiashara kwa mali zilizopo sio wakulialia muda wote hawana fedha,” alisema Kusaya.

Alisema Shirecu imekuwa ikikabiliwa na madeni mengi na kufikia hatua ya kushindwa kuyalipa. “Kama nasema uongo wapo viongozi wake wataeleza kwa nini madeni hayo yanashindwa kulipika na kuanza utaratibu mpya wa kuendesha ushirika,” alisema Kusaya.

Telack alisema alipokea hati ya viwanja saba kutoka kamati maalumu iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuchunguza mali za vyama vya ushirika. Alitaka mali hizo ziwekewe alama kwani bila kufanya hivyo zitapotea tena.

Mwenyekiti wa timu iliyoundwa na Waziri Mkuu, Asange Bangu alisema hati mbili ni za mali zilizokuwa Dar es Salaam na mali sita za majengo yaliyopo mkoani Shinyanga zote zikiwa na thamani ya Sh bilioni 3.3.

“Baadhi ya maofisa kutoka serikali ndiyo waliokuwa wameuziwa mali hizo kinyemela lakini baada ya mahojiano walikiri na kudai kuzirejesha mali za ushirika kwa kutoa fidia ya viwanja vingine vinavyoendana na thamani ya walivyonavyo kwa wakati huu,” alisema Bangu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirecu, Lenis Jishanga alisema wanadaiwa kiasi cha Sh bilioni 15 mpaka sasa na mali zilizorejeshwa zimefika mahali salama na atahakikisha wanazisimamia kwa umakini ili zisipotee tena.

Jumatatu wiki hii, Kusaya alikabidhi mali za vyama vikuu vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu zenye thamani ya Sh bilioni 61 zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha utaratibu.

Katika hafla iliyofanyika jijini Mwanza, Kusaya alikabidhi hati 37 kwa wenyeviti wa vyama vya Nyanza (NCU), Geita (GCU) na Simiyu (SIMCU) kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa Agosti, 2016.

“Leo (Jumatatu) nimekabidhi hati miliki 37 zinazojumuisha ardhi, majengo na mitambo yenye thamani ya Sh bilioni 61 zilizoporwa kinyemela na watu kutoka vyama vya ushirika Nyanza, Geita na Simiyu ambao ndio walikuwa wamiliki halali,” alisema Kusaya.

Kusaya alisema kazi ya kufuatilia na kurejesha mali imefanywa na timu iliyoundwa na Waziri Mkuu mwaka 2016.

Alitoa maagizo kwa viongozi wa vyama vya ushirika nchini kwamba mali zilizorejeshwa zitumike kwa manufaa ya wakulima ambao ni wamiliki.

Pia alimuagiza Mrajis wa Ushirika nchini ahakikishe mali zilizorejeshwa zinakuwa salama na kuwa asitokee kiongozi yeyote atakayefanya ubadhirifu.

Kusaya pia aliagiza watu ambao bado wanamiliki zilizokuwa mali za ushirika kinyume cha utaratibu wazirejeshe serikalini kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa kupitia timu ya Waziri Mkuu.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Dk ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy, Shinyanga

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi