loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ushauri wa Pinda ni muhimu, tupande miti kuijanisha Tanzania

JUZI Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akiwa katika Shule ya Sekondari Msanga, wilayani Chamwino, mkoani Dodoma katika tukio la upandaji miti, alitoa ushauri kwa watendaji katika halmashauri zote nchini kuhakikisha miti milioni 1.5 inapandwa kila mwaka katika kila halmashauri.

Ushauri huo ulilenga kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiwango kikubwa yanaleta athari kubwa katika dunia hivi sasa.

Katika mataifa mbalimbali tunashuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaochangiwa kwa kiasi fulani na maendeleo ya teknolojia na viwanda mambo yanayochochea pia mvua zisizo na utaratibu zinazosababisha maafa ikiwamo mafuriko.

Maafa hayo yanapotokea husababisha uharibifu mkubwa wa mali yakiwamo makazi, miundombinu ya reli, barabara, kusitishwa kwa usafiri wa anga, kufungwa kwa shule na vifo vingi hutokea katika maeneo yanayokumbwa na athari hizo.

Yapo malengo yaliyowekwa miaka kadhaa iliyopita ya kuipeleka Tanzania kuwa ya kijani na tangu mwaka 2015 mpaka sasa zaidi ya miti milioni 608 imepandwa nchini.

Pinda katika hafla hiyo akiwa mgeni rasmi, alisema katika kuhakikisha nchi inapambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeelekeza suala la upandaji miti katika kila halmashauri kuwa ni miti milioni 1.5 kila mwaka.

Kwa Mkoa wa Dodoma kama ilivyo kwa mikoa mingine, miaka michache iliyopita, ilizindua kampeni ya kuufanya mkoa huo kuwa kijani (kuijanisha Dodoma) na kurudisha uoto wake wa asili.

Ni kutokana na hilo, Waziri Mkuu mstaafu Pinda alitumia fursa hiyo kuushauri uongozi wa shule hiyo na wananchi kwa ujumla kupanda na kutunza miti popote ilipo ili imee vizuri na kufikia lengo lililokusudiwa.

Hakuishia hapo, Pinda alitaka katika harakati hizo za kupanda miti mkoani Dodoma na kwingineko nchini, watoto wafundishwe kupanda miti hasa ya matunda kwa sababu miili ya binadamu inahitaji sana chakula cha matunda na mboga.

Aidha alitoa ushauri huo si tu kama njia mahususi ya kukirithisha kizazi mbinu bora za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, bali pia ili kukabiliana na utapiamlo ambao bado upo nchini na hivyo kutokomeza tatizo la udumavu.

Ushauri wa Waziri Mkuu mstaafu Pinda haupaswi kuangaliwa kwa jicho la karibu, bali la mbali, hasa ikizingatiwa kuwa dunia inaingia katika kipindi cha nne cha mapinduzi ya viwanda ambacho kinatumia zaidi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na intaneti kama njia ya mapinduzi ya uchumi wa kidijiti na viwanda vingi hutegemea malighafi ikiwamo mbao katika uzalishaji.

Hatua tunayopaswa kuchukua kama Watanzania ni kuhakikisha kila mtu anapanda miti nyumbani, shambani na maeneo ya mengine ikiwa kando mwa barabara ili kuhakikisha mapambano haya yanafanikiwa.

Naipongeza Taasisi ya Habari Development Association (HDA) kwa malengo ya kupanda miti 100,000 mwaka kufikia mwaka 2021 mkoani Dodoma, taasisi nyingine ziige mfano huu ili kwa pamoja tuijenge Tanzania ya kijani na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi.

LEO wachezaji wa Timu ya ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi