loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watoto 1,059 waliofutiwa matokeo waombewa msamaha

MDAU wa elimu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif ameliomba Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), liwasamehe watoto 1,059 waliofuitwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba na liwape fursa ya kuufanya tena mtihani huo.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana, Seif alisema, ingawa kilichofanyika ni kosa lakini wanafunzi wengi wa darasa la saba umri wao huanzia miaka 12,13 hadi 14 na hivyo ni rahisi kwao kulazimishwa kufanya kilichofanyika.

“Hawa ni wadogo sana inawezekana wamelazimishwa. Kuwafutia matokeo kabisa ni kosa kubwa, wangepewa nafasi nyingine warudie mitihani kwani wengine ni watoto wa masikini si rahisi kuwapeleka shule binafsi,” alisema.

Aliiomba serikali iliangalie vyema suala hilo kwani kuwafutia mitihani watoto hao ni kuwaondolea matumaini yao ya baadaye. “hapa inawezekana tukapoteza madaktari, walimu na hata mawaziri au marais,”alisema Seif.

Hata hivyo, alisema, watu wengine wakiwemo walimu na wasimamizi wakibainika kuhusika kwenye udanganyifu huo wachukuliwe hatua kwa kuwa kitendo  walichofanya ni kinyume na maadili ya ualimu.

Alisema miongoni mwak kazi ya mwalimu anapokuwa na wanafunzi ni kufundisha maadili na kuwa mfano katika hilo.

“Sasa hiki kilichofanyika ni kufundisha mtoto kuiba ni kukiuka kabisa maadili yetu. Hawa lazima waadhibiwe kwa sababu wakiachwa wataleta shida katika jamii kwa kuwa na wasomi wasio na sifa,”alisema.

Hivi karibuni Katibu Mtendaji wa NECTA Dk Charles Msonde alibainisha kuwa, baraza hilo limefuta matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba kwa shule 38, zilizobainika kufanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo iliyofanyika Oktoba 7 na 8, mwaka huu na kwamba wanafunzi 1,059 wamefutiwa matokeo.

Shule zilizofutiwa matokeo ni Mafiri, Kibogoji, Ng’wambe, Digalama, Dihinda kutoka Halmashauri ya Mvomero na shule za msingi za Nyawa A iliyopo Halmashauri ya Bariadi vijijini, Ngiloli, Nguyami, Ibuti, Ihenje, Bwawani, Mogohigwa, Chakwale na Msingisi zilizopo Halmashauri ya Gairo.

Shule zingine ni Sikonge Tabora ikiwemo shule ya msingi Chabutwa, Usagari, Uyui Tabora Siashimbwe iliyopo Moshi Kilimanjaro, Dominion Arusha, Matogoro ya Tandahimba Mtwara, Ng’arita Bariadi vijijini mkoani Simiyu, Olkitikiti Kiteto iliyopo Manyara na Nyamimina Buchosa Mwanza.

Dk Msonde alisema, udanganyifu ni dhana pana bila kujali unafanywa na mtu wa umri upi na pia upo wa aina tofauti.

Alitataja miongoni mwa mbinu zinazotumika kufanya udanganyifu kuwa watahiniwa kupeana majibu ndani ya chumba cha mtihani, walimu kushirikiana na wasimamizi wa mitihani kuhakikisha mitihani inafanyika nje ya vyumba vya mitihani kwa kutumia ‘vikosi kazi’ na kisha majibu yanapelekwa ndani kwa watahiniwa.

“Wapo watu ambao wanaingia ndani ya chumba cha mtihani na vitabu au karatasi walizoandaa notisi labda wakaangalizie hicho kitendo kinaitwa ni cha kidanganyifu ukibainika na ukakamatwa lazima adhabu yake kwa mwanafunzi ni kufutiwa matokeo”alisema Dk Msonde wakati akizungumza kwenye kipindi cha Asubuhi Hii cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Alitoa mfano wa Shule ya Msingi Msingisi Gairo mkoani Morogoro kuwa walimu walikokotoa majibu wakawapelekea wanafunzi ili wayanakili na kwamba watoto hao wamefutiwa matokeo.

RC mkoa uliofanya vibaya atoa neno

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi, amesema baada ya mkoa huo kutofanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu, watafanya tathmini ili kubaini chanzo cha matokeo hayo mabaya.

Alilieleza HabariLEO kwa njia ya simu kwa sasa hawezi kusema kitu gani hasa kilichangia mkoa huo ufanye vibaya kwa kuwa bado walikuwa hawajafanya tathmini.

Wakati anatangaza matokeo ya darasa la saba hivi karibuni, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde, mbali na kutaja mikoa 10 iliyofanya vizuri pia aliitaja mikoa ya Mtwara na Singida kuwa ufaulu wake umeshuka.

“Mimi ni mwalimu, siwezi kwa sasa kusema nini kimesababisha tusifanye vizuri, tunatakiwa kufanya tathmini kwa sababu kuna vitu lazima tuvitazame kwa pamoja na kwa upekee wake”alisema Dk Nchimbi.

Alisema kwa kuwa Mkoa huo upo jirani na makao makuu ya Serikali Dodoma,  hawanabudi kufanya vizuri mwaka ujao kwa kuyafanyia kazi mambo watakayoyabaini kuchangia kufanya vibaya katika matokeo yaliyopita.

Kuhusu matokeo ya kidato cha nne na sita alisema mara nyingi Mkoa wa Singida umekuwa ukifanya vizuri, hivyo kwa matokeo ya darasa la saba watahakikisha wanafanyia kazi viashiria  vyote vilivyochangia kufanya vibaya ili mwakani waweze kufanya vizuri.

ASILIMI 80 ya wafanyakazi wa maofisini ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi