loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mila, asili na ndoa za Wangoni

KATIKA mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, leo tunaangazia jamii ya Wangoni, moja ya makabila yanayopatikana Tanzania na baadhi ya maeneo mengine kusini mwa bara la Afrika.

Kabila la Wangoni lina historia ya aina yake kama ilivyo kwa makabila mengine ya kibantu, hata yale yasiyokuwa ya kibantu. Kuna mambo mengi sana ya kuzungumzia juu ya kabila la Wangoni.

Naamini tumewahi kusoma au kusikia mengi sana juu ya kabila hili, hivyo katika makala haya tutaona kidogo kuhusu asili ya jina la Wangoni na masuala yanayohusu uchumba hadi ndoa.

Kwa nini waliitwa Wangoni na lipi chimbuko lao?

Kwa mujibu wa maandiko ya Fr. Elzear na Romanus Mkinga na masimulizi ya wazee inasimuliwa kuwa, asili ya jina la Wangoni linaanzia kusini mwa Afrika, ambako hapo awali kulikuwa na wakazi wengi katika koo za Wazulu waliofahamika kwa jina la Abanguni (kwa Kiswahili tunaweza kusema Wanguni) walioishi kusini mwa Afrika.

Kwa kipindi chote wakazi wote walikuwa wakifahamika kwa jina moja la Wanguni isipokuwa wale Khoisani.

Kwa miaka yote hiyo waliishi sehemu moja tu na hakukuwa na uhamiaji wowote nje ya ardhi ya Wanguni. Lakini baadaye eneo lao likaingiliwa na wageni, Wadachi. Na miaka ilivyozidi kwenda kuja wageni wengine, Waingereza.

Na kutokana na maslahi ya kiuchumi, kidini na kisiasa kulisababisha wageni hao kupigana na kuongeza migogoro mikubwa kusini mwa Afrika, ambayo kimsingi iliathiri sana jamii za Kiafrika, Wanguni wakiwemo.

Migogoro hiyo ikasababisha vita vya Mfekane miaka ya mwanzo ya 1800. Na vita hivyo vikasababisha baadhi ya Koo za Kinguni zilizokuwa kwenye makundi makubwa kuhama na kuelekea Afrika Mashariki na Kati. Wakati koo hizo zinatoka huko zilikuwa zikifahamika kama Wanguni.

Lakini mambo yalikuwa yakibadilika kadri walivyosonga, hasa maeneo waliyopita, mfano wakati Zwangendaba na Zwinde wanafika kwenye ardhi ya Wathonga maeneo ya Swaziland, Wathonga waliwaita Wangoni badala ya Wanguni.

Wao walitoa “U” na kuweka “O” kulingana na sheria na utaratibu wa lughu yao. Na hapo ndipo mabadiliko yalivyoanza kutokea katika zile koo maarufu, kutoka Wanguni hadi kuwa Wangoni.

Walipofika Nyasa kwenye miaka ya 1840/1850, walikuta makabila mengi sana, ila yaliyofahamika sana kutokana na biashara ni Wayao, ambao walihamia hapo baada ya kukimbia adha ya biashara ya utumwa iliyofanywa na Wamakua huko Msumbiji.

Hivyo kwa Wayao, Wangoni waliitwa Wagwangwala wakiwa na maana ya watu wenye haraka, na hii ni kutokana na mwonekano wa Wangoni kwenye ardhi ya Wayao, wakiwa wanatembea kwa haraka kuelekea maeneo mengine.

Mpaka kufikia kwenye miaka ya 1860, Wangoni walifika kwenye ardhi ya Wahehe. Lakini kabla ya kufika kwa Wahehe, walishafika maeneo ya Wasangu na Wabena. Lakini kutokana na kabila la Wahehe kuwa na ulinzi mkubwa na pia kuwa na jeshi imara lenye uzalendo wa hali ya juu hawakuwa tayari kuona ardhi yao ikivamiwa na kukaliwa na wageni ambao hawajulikani walipotoka.

Wahehe wakaingia vitani na Wangoni na kuwatimua katika ardhi ya Uhehe. Na mara baada ya vita hii Wahehe waliwapa jina kwa kuwaita Wamapoma au Wapoma, wakiwa na maana ya wavamizi waliovamia ardhi ya Wahehe na kuanzisha mapigano kuanzia kwa Wabena pamoja na Wasangu.

Na mpaka kufikia miaka ya 1870, Wangoni waliweza kufika kwenye ardhi ya Unyamwezi na Usukuma ambapo huko waliitwa Watuta. Na kuna baadhi ya maeneo ya Ziwa Tanganyika, Wangoni waliitwa Watuta hususan na makabila kama Wafipa waliokuwa na ufalme wao kwa wakati huo.

Suala la kupata mke au mume

Kupata mke au mume ni suala la lazima kwa dini zote duniani, kumekuwa na tamaduni nyingi za kuchumbia au kuposa mwanamke hususani hapa barani Afrika, huwa tunafuata mila mbalimbali na tamaduni zinazofuatwa ili kutovunja miiko ya kabila au jamii fulani husika.

Katika mila za Wangoni, hapo zamani, kijana wa kiume hata kama akikua na kuoa lakini kama hajaenda vitani ilikuwa haioneshi maana. Wakati wa kupigana vita kijana ilibidi aoneshe nguvu zake zilivyo.

Kijana ambaye hajaenda vitani aliitwa “lijaha” ikiwa na maana ya kijana/mvulana mdogo. Kijana ambaye ametoka vitani aliitwa “lidoda” ikiwa na maana kubwa.

Katika kuoa, alitafutwa mke mwenye sifa ya ukamilifu, anayejua kufanya kazi za nyumbani, aliyeweza kuokota kuni, kuchota maji, kutwanga, kupika chakula, kupika pombe na mcheshi anayecheka vizuri na watu wote katika mji.

Ndoa haifungwi katika ukoo, kwa maana kwamba Wangoni hawaoi mke au kuolewa na mume mwenye “kibongo”, yaani ubini mmoja. Kama watu wakioana katika ukoo, basi wazee wataulizia kwanza kama ukoo huo ni wa karibu au wa mbali. Kama hawa watu walioana ni wa ukoo wa karibu, basi watawaapizia.

Watu wanaogopa kuoana ndani ya ukoo kwa sababu wakifanya hivyo watoto watakaozaliwa watakufa. Na pengine watapata kifafa au “mahoka” (mababu) watakasirika, na hivyo kwa mila za Kingoni ndoa za koo moja huwa zinapitia katika matukio kadhaa mpaka kufungwa kwake.

Chiyagabuli

Kwa kabila la Wangoni, kama wakwe wa pande zote mbili wanakubaliana watoto wao waoane, “Watenga” watapeleka mahari kidogo kwa mama na baba wa binti, hii huitwa “chiyagabuli” yaani mahari ya mwanzo.

Baada ya muda yatapelekwa tena mahari ya mwanzo yaani kwa mara ya pili itakuwa ni Lusuka, kama aina fulani ya jembe “ngwamba” lenye tundu pale mpini unapotumbukizwa. Hii itamaanisha binti yao tayari kavunjwa ubikira.

Mtenga

Kwa Kingoni cha zamani, Mtenga ni mtu anayenunua au kuuza kitu. Mtenga anamuuza mtoto wa kike. Yeye ndiye atoaye chiyagabuli (mahari ya mwanzo) na “mawolowolo” ikiwa na maana mali yote kwa wenye mtoto wa kike.

Kulonda mdala

Wenye mtoto wa kiume wanapotaka kumwoza kijana wao, wazazi wengine walimtafutia mke (kulonda mdala). Wazazi wengine walimwacha kijana wao atafute mwenyewe mke amtakaye.

Kama walimwona msichana mrembo watamtafuta ndugu yao ambaye watamwelezea habari za ndoa. Na huyu ndiye atakayekuwa Mtenga wao.

Mtenga huyu ataanza kuulizia kwa siri mambo ya wazazi wa msichana husika na wanaukoo wake wote na halafu ataenda kuwaeleza wazazi wa kijana. Kama wazazi wataona ya kuwa ni msichana hodari, Watenga wataenda kwa wazazi wa msichana na kuuliza kama wanaruhusiwa kumwoa? Kama wenye binti watakataa, Watenga wataombeleza.

Lukotelu

Watenga wanapotaka kwenda kuulizia kumwoa mke lazima wawe na kiulizio. Wanapoenda kule, wanachukua kitu kinachoitwa “lukotelu” au “luhongelu” yaani kiulizio, kitu hicho chaweza kuwa nguo, ushanga, fedha n.k.

Kuchicha

Kuchicha ni kitendo cha msichana aliyechumbiwa kwenda rasmi kumtembelea mchumba wake, kimila huyo msichana aliyechumbiwa anaenda na rafiki yake wa kike. Hivyo basi siku hiyo inakuwa ni kama anaenda kuona mazingira atakayokuja kuishi.

Kimsingi katika siku ya kuchicha hairuhusiwi kulala pamoja na kufanya mapenzi ndiyo maana msichana alipaswa kusindikizwa na msichana mwenzake. Lakini mara nyingi imekuwa ngumu kujizuia na wengi wamekuwa wakiishia kufanya mapenzi, mbaya zaidi unakuta mvulana naye anaalika mvulana mwenzake halafu wanawagawana hao wasichana waliofika hapo.

Wakati mwingine kuchicha inaweza kuwa kinyume chake; kijana wa kiume pamoja na vijana wenzake wanaenda rasmi kumtembea mchumba/msichana. Huko ukweni kijana muoaji anafanya kazi nyingine nyingi.

Kwa kufanya hivyo, wakwe watamwona ni mume wa uhakika, kuwa anaweza kufanya kazi za kiume, kama anajua au anaweza kulima, kukata matema (kukata miti shambani kwa ajili ya kuandaa shamba), kama anaishi vizuri na watu au kama hana haraka ya kula.

Muda wote huo wa kuwepo hapo, kijana huyu hajioneshi kwa wakwe zake. Anapotaka kutoka nje ya nyumba alalayo ni lazima ajifunike nguo usoni gubigubi.

Kijana atafanya hivyo atakapotaka kumwona mtarajiwa mkewe, hakuna kujionesha kwa wakwewe mpaka atakapopata mtoto. Na mwanamke atafanya hivyo kwa wazazi wa mumewe.

Lakini sasa neno ‘kuchicha’ limekuwa likitumika isivyo rasmi, kwa mfano kitendo cha msichana kutongozwa na mvulana wapo walioita kuchicha na imezoeleka hivyo na wengi.

 

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

MOJA ya migogoro mingi inayojitokeza katika familia ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi