KATIBU Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk John Jingu amewataka watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuepuka aina zozote za manyanyaso kwa umma.
Dk Jingu alisema wakati wa kilele cha kongamano la wanataaluma wa sekta ya watumishi wa jamii (TASWO) lililoandaliwa Mwanza na kuwakutanisha zaidi ya washiriki 450 kutoka Tanzania Bara na visiwani kwa lengo la kuhamasisha uwepo wa haki kwenye jamii.
Alisema fani ya ustawi wa jamii ni muhimu kwa ustawi wa taifa hivyo alisema serikali itaendelea kushirikiana nao kwa hali na mali ili waweze kuenenda vizuri katika utendaji wa kazi zao.
Alisema kada hiyo inapaswa kujikita kutoa elimu itakayoleta mabadiliko chanya kwenye jamii ili kuwezesha walemavu, wanawake, wasichana na wazee kupata haki zao wanazositahili.
Mwenyekiti wa Taswo,Dk Mariana Makuu alisema sekta ya ustawi wa jamii ni muhimu saana kwa maendeleo ya taifa kwani inasaidia katika utatuzi wa masuala ya kisaikolojia ambayo ni tatizo linalosumbua jamii ya watu wengi hapa nchini.