loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waridhishwa udhibiti ukatili kijinsia

WADAU wa masuala ya jinsia nchini wameeleza kuridhishwa na hatua  zinazochukuliwa na serikali na taasisi nyingine binafsi kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia huku wakipongeza uwazi unaowezesha waathirika kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, baadhi wamesema miaka ya zamani, wanawake walifundishwa kuvumilia vipigo na vitendo vya ukatili wakiaminishwa kuwa ni mambo ya kawaida katika ndoa yasiyotakiwa kusemwa hadharani.

Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi, Anna Abdallah, alishukuru serikali kwa kuwezesha mabadiliko kiasi kwamba masuala ya ukatili yanapingwa hadharani.

“Nashukuru sana serikali ya Tanzania kwa nyakati tofauti imekuwa ikiboresha mifumo na mitazamo katika jamii, enzi zetu, miaka hiyo ya 1970, vipigo na mambo mengi ya ajabu ya kinyanyasaji ilikuwa sehemu ya ndoa, na mwanamke alifundishwa kuvumilia,” alisema Abdallah.

Aliongeza, “Tulikuwa tunafumbia macho, tunaambiwa ni masuala ya ndani ya ndoa,basi wanandoa wanavumilie wee inakuwa sehemu ya maisha, kumbe ndio ukatili,ila sasa tunashukuru mambo yamebadilika, ukatili unasemwa hadharani kwa lengo la kuukomesha.’,

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Anna Henga alisema matukio ya ukatili yanaongezeka katika jamii yakiwemo ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na mengi yanafanywa na watu wa karibu wa familia au jamii husika.

Henga alisema madawati ya jinsia kwenye vituo vya Polisi nchini yamekuwa na msaada mkubwa kwani familia nyingi zimebadilika.

Alisema hata vipigo kwenye baadhi ya ndoa vimekoma kutokana na kutolewa taarifa na wahusika kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuelimishwa.

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘’Zuia ukatili, mabadiliko yanaanza na mimi’ ina maana kubwa iwapo kila mmoja ataichukua na kuifanyia kazi.

“Lazima tukatae kufanyiwa vitendo hivi na tupaze sauti kwa wanaowafanyia wengine, sheria zipo ila kama  matukio hayo hayataripotiwa, itakuwa kazi bure,” alisema Henga.

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), Dk Lulu Mahai alisema  mwanandoa anayefanyiwa vitendo vya ukatili anapaswa kutoa taarifa kwa sababu sheria zipo wazi na pia anaweza kushirikisha mashirika ya msaada wa kisheria au jinsia yamsaidie.

Askofu William Mwamalanga alisema suala la ukatili ndani ya jamii lisiachwe kwa wanandoa pekee bali liende mbele zaidi kwa kushirikisha jamii nzima kwani ndoa moja ikisarambatika huathiri jamii mzima.

“Masuala ya ukatili yasifichwe kwenye jamii yazungumzwe kwa uwazi ili kuijenga jamii kufahamu matendo hayo ni mabaya na hayapaswi kufanywa, ndoa moja inaposarambatika, jamii mzima huathirika na hilo linaenda pia kuleta madhara kwa taifa,” alisema Askofu Mwamalanga.

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni  inayotoa fursa kwa wanawake, wanaume, vijana wa kike na kiume na wanaharakati wengine kukuza uelewa wa umma juu ya mchango wa jinsia zote katika maendeleo.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Dk ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick na Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi