loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bil 96/- zilizopokwa ushirika zarejeshwa

 

MRAJISI wa Ushirika amesema hadi sasa vyama vya  ushirika vikubwa vitatu nchini vilivyopokwa mali zake zaidi kuliko vyama vingine , vimerejeshewa mali zilizokwishabainika zenye thamani ya zaidi ya Sh  bilioni 96 .

Akizungumza na HabariLEO juzi jijini Dar es Salaam, Mrajisi huyo Dk Benson Ndiege alivitaja vyama hivyo na kusema kuwa kazi ya kutambua mali hizo ni endelevu.

Vyama hivyo ni Chama cha Ushirika Shinganya(Shirecu), Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) na  Vyama Vikuu vya Ushirika Nyanza.

Alisema  hadi sasa mali  za Shirecu zilizorudishwa ni zaidi ya Sh bilioni 15, wakati mali za Nyanza zilizorejeshwa ni Sh bilioni 61 na mali za KNCU ni takribani Sh. Bilioni 20.

Dk Ndiege alisema kurejeshwa kwa mali hizo ni mchakato mrefu ambao hauwezi kuisha kwa siku moja au muda fulani kwani, kadri muda unavyosonga ndivyo mali nyingine za vyama hivyo zinabainika na kufanyiwa uchunguzi kubaini uhalali wake katika mchakato wa uuzwaji wake.

Alisema awali mwaka 2016, Rais John Magufuli alitoa maagizo kutaka uchunguzi ufanywe kurejesha mali za vyama vyote vya ushirika zinazomilikiwa na watu isivyo hahali.

Katika kutekeleza maagizo hayo, Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa aliunda Kamati Maalumu mwaka 2016 kuchunguza mali za vyama vya ushirika na kutaka ziwekewe alama ili zisitokwe na zile zinazomilikiwa na watu isivyo halali zirejeshwe kwenye vyama.

Dk Ndiege alisema katika takwimu za Ofisi ya Mrajisi, hadi Aprili mwaka huu kulikuwa na jumla ya vyama 9,185 vya ushirika nchi mzima.

“Awali kabla ya Aprili mwaka huu tulikuwa na vyama vya ushirika 11,000 lakini baadaye tulifuta vyama karibu 3,000 tukabakiwa na hivyo 9,185 nchi mzima, na kati ya hivyo vikubwa ni vitatu ambavyo ndivyo vilikuwa na changamoto za mali baadhi ya mali zake kupokwa isivyo halali na ndio maana tunazihakiki na kurejesha”,alisema Dk Ndiege.

Alisema vyama vingine vya ushirika viligawanyika na kuzaliwa vyama vingine ndani ya vyama hivyo lakini vyeme changamoto zaidi ni hivyo vikubwa na kuwa changamoto hizo zimetokana na mfumo wa kubadilisha viongozi wa vyama.

“Kinachofanywa kwenye kamati hiyo siyo kupora mali zilizouzwa kihalali za vyama hivyo, la hasha, bali mali zilizouzwa isivyo halali ndio zinarejeshwa na hii inafanywa kwa kutumia pia busara kwani wakati mwingine unakuta mtu aliyenunua labda eneo la chama aliuziwa kwa bei isiyo halali na amepaendeleza amejenga nyumba, kinachofanyika ni kuzungumza naye na anaweza kutoa eneo lake jingine lenye thamani sawa akafidia’’,alisema Dk Ndiege.

Alisema kamati inayofanya kazi hiyo inabaini mali kwa nyakati tofauti na kuwa zinapongudulika hufanyiwa uhakiki na kurejeshwa kwa chama kama zikibainika kuuzwa au kumilikishwa isivyo halali na kuwa kazi hiyo ni endelevu.

Alisema mikoa mingi haijafanyiwa ukaguzi kubaini uhalali wa mali za vyama hivyo na kutoa mfano kuwa mkoani Geita bado kuna mali za vyama hivyo zikiwa mikononi mwa watu isivyo halali.

“Bado kuna mikoa kamati haijaenda, mfano Geita inaonesha bado mali za ushirika ziko mikononi mwa watu isivyo halali, Morogoro nako kamati haijaenda, ila tunajua kuna mali nyingi zimefujwa.Mfano vipo vyama kama viwili vya ushirika ambavyo vyama mama vilikufa na mali nyingi chukuliwa isivyo halali, ukaguzi utafanywa ili kuzibaini’’,alisema Dk Ndiege.

Akizungumzia changamoto iliyosababisha upotevu au ufujaji wa mali hizo, Dk Ndiege alisema unatokana na mfumo wa mabadiliko ya uongozi.

“Viongozi wa vyama vya ushirika huwa wa muda wa kukaa madarakani, wanapomaliza muda wao na kuja wengine wakati mwingine makabidhiano yanakuwa mabaya hakuna utambuzi wa mali au kuna ujanja ujanja umefanywa, nakala za mali hazionekani”,alisema Dk Ndiege.

Akizungumzia walivyojipanga kuhakikisha mali zinazorudishwa zinatunza na kuendelezwa, Dk Ndiege alisema kamati hiyo inaendelea na kazi na kwamba moja ya kuhakikisha mali zinazorudishwa zinaendelezwa na kuzalisha ni kupanga vizuri safu ya uongozi.

Wiki hii, Wizara ya Kilimo ilisema kazi ya kutambua mali za vyama vya ushirika na kuzirejesha zile zinazomilikiwa isivyo halali ni endelevu na inaratibiwa kwa karibu na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerald Kusaya.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Dk ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi