loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wabunge wajibebe

WATU wa kada tofauti, wakiwamo wasomi na wanasiasa wamewataka wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kusimama wenyewe na kutatua kwa kasi kero katika maeneo yao badala ya kutegemea kubebwa na mafanikio ya kitaifa.

Ushauri huo umetolewa huku baadhi ya wabunge wakiwa wameanza ‘mchaka mchaka’ wa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa wakati wa kampeni hatua iliyotajwa kuwa itawajengea wananchi imani na kuwa tayari kuwapa ridhaa ya kuendelea kuongoza.

Kwenye uzinduzi wa Bunge la 12, Novemba 13 ,mwaka huu, Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima alisema utendaji kazi wa Rais Magufuli umechangia ushindi wa wabunge wengi majimboni.

Pia Spika wa Bunge, Job Nduga alisema baadhi ya wabunge waliochaguliwa wanapaswa kumshukuru Rais Magufuli kwani kama si yeye kuwaombea kura, walikuwa hawachaguliki.

Wabunge wajibebe

Baadhi ya wasomi, wanasiasa, wanasheria na watu wa kawaida wamewataka wabunge kutobweteka, vinginevyo uchaguzi mkuu ujao watatakiwa kujisimamia.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema wabunge hao wanapaswa kufahamu majukumu yao ya kitaifa, ndani ya majimbo na chama chao. Alisema wanatakiwa kuwa na uelewa mpana na ubunifu katika kutatua kero za wananchi.

"Mbunge asiishie kukaa bungeni na kusikiliza wenzake wakichangia, bali wanapaswa kuwa na uwezo wa kushawishi serikali ndani ya Bunge hilo ili miradi mbalimbali ipelekwe katika majimbo yao…itasaidia kuwapa imani wapiga kura wao na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuchaguliwa tena," alisema.

Mwanasheria kutoka Kampuni ya Uwakili ya Locus Attorney, Dk Onesmo Kyauke alisema kutokana na utendaji wa Rais Magufuli unaoonekana wazi, wasaidizi wake wanapaswa kuiga aliyofanya kujiweka katika mazingira mazuri ya kurudi bungeni katika kipindi kingine.

"Wachape kazi, zaidi waone namna nzuri ya kukutana na wapiga kura wao mara kwa mara na kujua matatizo yao, wakati mwingine ushauri mzuri juu ya utendaji unatoka kwa wananchi, hili litawasaidia sana katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo," alisema Kyauke

Mkurugenzi wa taasisi ya Kila Kona Schools inayoshughulikia masuala ya elimu, Salim Mngodo, alisema wabunge hao wanatakiwa kutobweteka na badala yake wafanye kazi kwa kubeba utendaji wa Rais Magufuli mambo yaweze kuwaendea vizuri majimboni.

Mngodo alikumbushia hotuba ya Rais Magufuli ya kuzindua Bunge la 12 ambayo pamoja na masuala mengine, aliwataka wabunge kuchapa kazi kujengea wananchi imani.

Akizunguza hivi karibuni na waandishi jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwataka viongozi wanaotokana na chama hicho kutekeleza ilani ya chama wakitanguliza maslahi ya wananchi.

Mchaka mchaka waanza

Miongoni mwa wabunge walioanza kazi kwa vitendo ni Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ambaye siku chache kabla ya kuapishwa, alitekeleza ahadi ya kuchimba kisima cha maji katika soko la Kilombero-Arusha.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson pia ametangaza ratiba ya kukutana na kusikiliza hoja na kero za wananchi mara mbili kwa kila wiki katika siku za Alhamisi na Jumamosi.

Tulia aliwaambia waandishi wa habari kuwa amefanya hivyo baada ya kubaini kwamba, wakati mwingine wananchi wamekuwa wakihangaika kutafuta mwakilishi. “Sasa nimeona nitangaze mapema utaratibu huo ili kazi iendelee,” alisema.

Wakati huo huo, Dk Tulia ametoa bodaboda 12 za mkopo zenye thamani ya Sh milioni 30 na kusisitiza kuwa wataendelea kuwezesha vikundi mbalimbali vya vijana na wanawake.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Mavunde hivi karibuni alizindua kisima cha maji katika eneo la Chikola, Kata ya Matumbulu kitakachonufaisha kaya 370 na wananchi zaidi ya 2000. Awali walitembea zaidi ya kilometa nne kufuata maji.

Kisima kimechimbwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Islamic Help Tanzania kwa ushirikiano na Taasisi ya Dabbagh Welfare Trust ya Denmark kutokana na maombi yaliyowasilishwa na mbunge kwa taasisi hizo.

Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole ameanza kutatua kero ya maji kwa kuchimba visima vikubwa vitano katika kata ya Mlowo vitakavyogharimu zaidi ya Sh milioni 60 na kuhudumia watu zaidi ya 20,000.

Mwenisongole alisema vile vile Desemba 12 mwaka huu atakutana na wakuu wa shule 25 za jimbo hilo na kukabidhi kila shule kompyuta mbili, vitabu vya sayansi 50, seti ya jezi na mpira.

“Tuna wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwa kuwa hiyo ndiyo dawa pekee itakayotusaidia kufanikisha matakwa ya wananchi wetu na taifa kwa ujumla,” alisema Mbunge wa Mkuranga,  Abdallah Ulega.

Kati ya wabunge 393 wanaotakiwa kikatiba, 256 ni wa CCM. Siku Rais Magufuli alipozindua Bunge, Spika Job Ndugai alisema walikuwapo wabunge 359 akiwamo Mwanasheria Mkuu, watatu  wa Chama cha Wananchi (CUF), ACT Wazalendo wanne. Chadema kilikuwa na mmoja wa jimbo lakini wiki hii, wabunge 19 wa viti maalumu kutoka Chadema wameapishwa.

 

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi