loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchaguzi Mkuu Uganda uimarishe EAC

MAPEMA Januari mwakani taifa jingine la Afrika Mashariki la Uganda litaingia katika Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Huo utakuwa mtihani mkubwa kwa wananchi wa Uganda kuamua kupita katika barabara ya amani au ya vurugu, fujo na uvunjifu wa amani.

Kama wana wa Afrika Mashariki tunataka uchaguzi utakaoimarisha mshikamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dunia nzima inaitambua EAC kama jumuiya imara barani Afrika na sababu ni kuwa wanachama wake wana amani na utulivu mkubwa.

Kwa baadhi ya kanda katika Bara la Afrika kuna chaguzi mbalimbali zimefanyika ambazo nyingine zimeacha vumbi la machafuko.

Jumuiya ya Afrika Mashariki haitaki uchaguzi wa kuigawa nchi katika vipande bali inahitaji uchaguzi wa kuimarisha mshikamano na ushirikiano.

Katika chaguzi zilizofanyika hivi karibuni barani Afrika ni pamoja na Ivory Coast, Senegal, Afrika ya Kati na Ghana na  Tanzania.

 

Kutokana na hali inavyoendelea nchini Uganda inatia wasiwasi kuhusu uchaguzi huo kutokana na kuwapo kwa viashiria vya kuvurugika kwa amani, huku kukiwapo na mazuio ya kudhibiti maambukizi ya corona.

Tayari vurugu zimeshachukua maisha ya watu zaidi ya 50 baada ya mgombea wa upinzani kukaidi vizuizi vilivyowekwa. Polisi walimtaka mgombea huyo kupitia vuguvugu la nguvu ya umma Robert Kyagulanyi kutofanya mikusanyiko mikubwa ili kuwakinga wananchi na maambukizi ya corona huku akikaidi.

Rais Yoweri Museveni ameshatoa taarifa ya kulaani mauaji hayo na kuahidi kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote waliohusika na uhalifu huo.

Ninafahamu kuwa uchaguzi wa safari hii nchini humo utakuwa na ushindani mkubwa tofauti na chaguzi nyingine zilizowahi kufanyika nchini humo. Kwa kuzingatia hilo, kama Waganda wenyewe hawatakuwa makini watajiweka katika matatizo makubwa.

Siku zote kunapokuwa na uchaguzi kama huu ni rahisi nchi kuingia katika matatizo ya vurugu endapo kila mmoja hatatekeleza majukumu yake ili uchaguzi uwe wa amani na utulivu.

Tanzania imeonesha mfano mzuri katika suala la uchaguzi mkuu, ukianzia mwaka 2015 baada ya uchaguzi nchi ilibaki salama mpaka uchaguzi wa mwaka huu nao umeisha na umeiacha nchi ikiwa salama.

Hata ukiangalia rekodi za kipindi cha nyuma, baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 Tanzania ilibaki salama mpaka na wa mwaka 2010 nao uliisha salama na nchi ikabaki na amani na utulivu.

Hivyo wananchi wa Uganda na viongozi wake wanapaswa kuiga mfano wa Tanzania ili kuwa na uchaguzi wa amani na utulivu ili nchi iendelee kuwa salama na watu kufanya shughuli za maendeleo.

Tunatarajia Waganda watafanya uchaguzi wa amani ili baada ya uchaguzi waweze kuendelea na shughuli zao za kujitafutia maendeleo, kufanya biashara, kilimo, uwekezaji na mambo mengine muhimu.

Kwa ujumla Kanda nzima ya Afrika Mashariki haiwezi kuwa imara na madhubuti endapo nchi moja itaingia katika machafuko. Nchi zote za Afrika Mashariki zinategemeana kijamii, kiuchumi, kisiasa,  kiteknolojia na mambo mengine

KUELEKEA mwishoni mwa mwaka 2020, ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi