loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukaribisheni mwaka mpya kwa kuwa tayari kuwajibika

WAKATI leo Watanzania wote wakiungana na watu wengine duniani kusherehekea sikukuu ya Krismasi, zimebaki siku tano tu yaani Januari mosi kuukaribisha mwaka mpya wa 2021.

 

Ni wazi kuwa sasa mwaka wa 2020 uliotawaliwa na matukio mengi yakiwamo yaliyowagusa Watanzania kila mmoja binafsi na kitaifa na duniani kwa ujumla unafikia tamati na kuingia mwaka mpya wa 2021.

 

Pamoja na shamrashamra hizo, sasa ni wakati wa kuanza kujipanga upya na kila mtu kwa nafasi yake kuangalia namna atakavyojiinua kimaisha lakini pia kuwajibika ipasavyo kuijenga nchi yake.

Kwa bahati nzuri tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015 ikiwa ni miaka mitano kamili sasa, Watanzania wamejionea namna serikali yao inavyowajibika.

Serikali hiyo ikiongozwa na Rais John Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inapambana na ufisadi, wizi,  majanga, ubadhirifu, uonevu dhidi ya wananchi wanyonge na kuliletea maendeleo taifa.

Si hivyo tu, pia serikali imekuwa ikihimiza uwajibikaji hasa kwa watumishi wa umma na uchapakazi kiasi cha Dk Magufuli kuja na kauli mbiu yake ya ‘Hapa kazi tu.’

Hivyo basi, ni wakati sasa wa Watanzania kuuanza mwaka mpya wa 2021 kwa kufuata nyayo za serikali hiyo na kuwajibika ipasavyo kwa kufanya kazi katika kujijenga wenyewe kimaisha lakini pia kulijenga taifa hilo la Watanzania kimaendeleo.

Mwaka 2021 uwe si mwaka wa vijana kulundikana vijiweni wakipiga soga, kucheza bao au mchezo wa puli tebo. Mwaka mpya uwe wa kuchakarika kutafuta kazi au kujiajiri ili kila mmoja kwa wakati wake aweze kutimiza malengo yake.

Tukumbuke kuwa huu si wakati wa watu kuilalamikia serikali kwa kila kitu kwani ukweli ni kwamba huwezi kukaa nyumbani au kushinda kutwa kijiweni bila kujihangaisha mtaani kutafuta riziki halafu ukaishia kuibebesha lawama serikali kwa maisha magumu utakayokumbana nayo.

Hata vitabu vya dini vinasema kila mtu atakula kwa jasho lake kwa maana ya kwamba yule atakayehangaika juani ama kulima, kutafuta habari, kuuza mchicha, kuosha magari na hata kuponda kokoto mwisho wa siku yeye ndiye atakayepata riziki na kujiendeleza.

 

Kwa maana hiyo, kuanza kwa mwaka mpya iwe ni fursa ya Watanzania kujisafisha na kuanza upya kuijenga nchi yao si tu kwa kuwajibika na kujiinua kimaisha bali pia kulisimamia kidete taifa lao liendelee kuwa na amani na mshikamano.

Katika kipindi chote cha msimu wa sikukuu viongozi wa dini wamekuwa wakiwaasa Watanzania kuiombea nchi yao iendelee kuwa na amani na watu wake kuwa na mshikamano kwa maendeleo ya taifa.

Lakini pia viongozi hao wamekuwa wakihamasisha suala zima la mshikamano na uwajibikaji kwani hakuna taifa linaloweza kupiga hatua yoyote ya maendeleo endapo wananchi wake wameparaganyika.

Ni wakati wa kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika kuliletea maendeleo taifa zima kwa kuwa mstari wa mbele kuchapakazi, kuweka mbele uzalendo, kuepusha migogoro isiyo ya lazima ikiwemo uvunjifu wa amani, lakini pia kuwafichua wale wote wenye nia mbaya na taifa hili.

Pamoja na kuweka lengo hilo la kuijenga nchi, kila mmoja kwa wakati wake pia atumie mwaka mpya kujipanga upya katika kujiendeleza.

Endapo mwaka uliopita hakufanikiwa kutimiza ndogo zake, huu si muda wa kukata tamaa.

 

Mwaka 2021 uwe wa uthubutu. Uwe ni mwaka wa kujipanga na kuweka mikakati inayotekelezeka kwa faida ya mtu binafsi na maendeleo ya taifa.

Nawatakia Watanzania wote heri ya mwaka mpya.

KUELEKEA mwishoni mwa mwaka 2020, ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi