loader
Dstv Habarileo  Mobile
Karibu Waziri Mambo ya Nje wa China

Karibu Waziri Mambo ya Nje wa China

TANZANIA itakuwa na ugeni mkubwa wa siku mbili wa Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Baraza la Taifa la China, Wang Yi anayetarajiwa kutua nchini leo.

Wang Yi anakuja ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa kindugu na wa muda mrefu kati ya Tanzania na China ambao uliasisiwa na viongozi wa kwanza wa mataifa haya, Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong.

 Awali, tungependa kumkaribisha Waziri Wang Yi pamoja na ujumbe wake nchini Tanzania, tukiamini kwamba kwa siku mbili atakazokuwa nchini atajisikia nyumbani kutokana na urafiki na uhusiano huo wa muda mrefu wa mataifa haya mawili, lakini zaidi kutokana na ukarimu wa Watanzania kwa wageni.

Ushirikiano huo wa China na Tanzania umedumu kwa muda mrefu na umeziwesha pande zote mbili kunufaika na ushirikiano huo katika nyanja mbalimbali kama vile za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Kwa mfano, uhusiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na China umewezesha nchi ya China kwa miaka 30 sasa kuwekeza miradi 940 nchini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 7.5 iliyozalisha ajira zaidi ya 117,810.

 Miradi hiyo ni iliyosajiliwa Tanzania Bara kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Mwaka 2017, China ilikuwa na miradi 723 ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.9 ikitoa ajira 87,126. Aidha, kwa upande wa Zanzibar, jumla ya miradi minane ya thamani ya Dola za Marekani milioni 142.9 imesajiliwa katika Mamlaka ya Uhamasishaji wa Uwekezeji Zanzibar (ZIPA).

Hivyo, ziara ya Waziri Wang Yi nchini ni udhihirisho tosha kwamba nchi hiyo itaendelea kuwa nchi yenye lengo la kuwekeza zaidi katika maeneo mbalimbali ikiwamo kilimo, viwanda, utalii, ujenzi, teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na miundombinu nchini Tanzania.

Ndio maana katika ziara hii, Waziri wa Mambo ya Nje ya China atakuwa na majukumu ya kujionea maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania pamoja na kujionea maeneo ambayo China inaweza kuendelea kuisaidia Tanzania.

 Tufahamu kuwa leo atafungua Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilayani Chato, mkoani Geita na kesho kutembelea mwalo mjini humo kuona jinsi China inavyoweza kununua mabondo ambayo yanasafirishwa kwenda nchini humo na hivyo kuchangia katika biashara kati ya nchi hizi mbili.

 Pia katika mazungumzo yake rasmi na Rais John Magufuli na ujumbe wa pande hizo mbili, masuala ya kibiashara kati ya Tanzania na China yatachukua nafasi kubwa pamoja na masuala ya mikopo na misaada ya maendeleo.

 Ni kwa msingi huo, tunamkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa China tukisisitiza kudumishwa kwa uhusiano na urafiki wa muda mrefu wa Tanzania na China ambao umejengwa katika misingi ya kusaidiana bila ubaguzi na yenye kuzingatia maslahi ya pande mbili, jambo linalodhirishwa na ziara hii ya Wang Yi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/062ae5094a37d373f1060440b148bd12.jpg

KWA mara ya kwanza leo dunia inaadhimisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi