loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jiji la Arusha lawamani kwa kubomoa nyumba

WAKAZI wa Kata ya Muriet jijini Arusha, wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati ili wapate haki yao wakidai Halmashauri ya Jiji la Arusha imebomoa nyumba zao bila kufuata utaratibu.

Wakizungumza juzi katika eneo la tukio wakati wakiwaelezea wanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, waathirika wa tukio hilo, Willson Mollel na Baraka Koole, walidai kuwa halmashauri hiyo imebomoa nyumba zao bila kufuata taratibu.

Wanasheria hao walikuwa wametumwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongosi kwenda kusikiliza kilio cha wakazi hao.

"Hawa jiji tumewashinda kwenye kesi ya mgogoro wa eneo hili mahakamani, sasa wanatumia nguvu nyingine kuhakikisha hatuendelezi eneo letu," alisema Koole.

Walisema awali walishinda katika kesi iliyokuwa katika Mahakama ya Ardhi ya Wilaya dhidi ya halmashauri hiyo kuhusu eneo hilo na mahakama ikawatambua kama wamiliki halali wa eneo wenye haki ya kuliendeleza.

 

"Tukiwa katika hatua ya kuendeleza eneo letu ikiwemo kujenga nyumba za kudumu, nilishangaa Desemba 30 mwaka jana kuona kutapila na mgambo zaidi ya 20 wakibomoa nyumba yangu wakiongozwa na Mwanasheria wa Jiji la Arusha, Sifael Kulanga," alisema Koole.

Naye Willson Mollel alisema eneo hilo ni mali ya familia yao na kwamba liliachwa na wazazi wake waliofariki miaka ya nyuma na kuzikwa hapo.

Alisema licha ya wenzake kulipwa fidia wakati halmashauri hiyo ilipomega maeneo yao ili kujenga dampo la taka ngumu, yeye hakuwahi kufidiwa na sasa anasikitika hata kipande kilichobaki anazuiwa kujenga na nyumba yake kubomolewa.

"Mwaka 2016 walibomoa nyumba yangu na sasa tumeshinda kesi wamekuja kunibomolea tena; Mimi namuomba sana Rais wetu John Magufuli aingilie suala hili ili anisaidie kupata haki yangu.”

Akijibu hoja hizo Mwanasheria wa Jiji la Arusha, Sifael Kulanga, alisema nyumba za wakazi hao zimebomolewa kwa kuwa ujenzi wake haukufuata taratibu za mipango miji kwa kupata kibali cha ujenzi.

"Hatukubomoa kwa sababu ya mgogoro wa eneo, tumebomoa kwa sababu hawana kibali cha ujenzi na tulitoa onyo kwa watu kuacha kujenga bila kuwa na kibali cha mipango miji," alisema Kulanga.

Baadhi ya wananchi na wakazi wa eneo hilo wameitaka halmashauri hiyo kufuata sheria inapotaka kubomoa nyumba ya mtu ikiwa ni pamoja na kutoa notisi ya barua tatu jambo wanalodai halikufanyika.

"Hii nchi inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu; sasa kama mtu anajichukulia sheria mkononi bila hata kuhusisha viongozi wa eneo husika si sawa  na kimsingi jambo hili limefanyika kiuonevu," alisema Mwenyekiti Mstaafu wa Mtaa wa Muriet, Petro Mollel.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kihongosi alisema anaisubiri taarifa kutoka kwa wanasheria wake na atalitolea uamuzi.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi