loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ukatili kijinsia unahitaji mahakama maalumu

Ukatili kijinsia unahitaji mahakama maalumu

KUELEKEA mwishoni mwa mwaka 2020, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala lilitoa huduma za ‘mkono kwa mkono zinazotembea’ maarufu ‘One stop center mobile’ katika kata saba za Chanika, Pugu, Gongolamboto, Segerea, Vingunguti, Buguruni na Kiwalani.

Huduma hizo zilizopongezwa na wengi wakiwasifia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Janeth Magomi na Mwanzilishi na Mratibu wa One stop center katika mkoa huo wa kipolisi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dk Christina Onyango.

Zilivuta watu mbalimbali kiasi kwamba muda wa siku mbili katika kila kata ulikuwa mdogo  na wananchi wakaomba ziwe endelevu.

One stop center ni mahali zinapopatikana huduma zote kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia zikiwamo za polisi, mwanasheria, daktari na ofisa wa ustawi wa jamii ili kuepusha usumbufu kwa mwathirika kuzitafuta sehemu mbalimbali kwa gharama kubwa ya muda na fedha.

Katika vituo hivyo walijitokeza wanawake, wanaume na watoto kuelezea adha na madhila yaliyowakumba au yanayowakumba katika jamii ili wapatiwe msaada.

Miongoni mwa waliozungumza na HabariLEO, walisema wanaogulia madhila hayo nyumbani kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuona aibu na kuogopa unyanyapaa katika jamii wanapojitokeza, kuogopa kutengwa na kulaumiwa na pia kubanwa na mila kuwa baadhi ya mambo hayasemwi.

Kimsingi, mambo hayo na mengine mengi yakiwamo ya baadhi ya askari wachache wasio waadilifu kuwakejeli wanaofanyiwa ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia hali inayowaongezea madhala yakiwamo ya kisaikolojia na kiuchumi.

Mazingira ya ukusanyaji, utunzaji na utoaji ushahidi katika kesi hizo yanatajwa kama changamoto kubwa katika vita dhidi ya udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia hali inayohitaji kuwapo vyombo maalumu vya kisheria (mahakama) kwa ajili ya masuala hayo.

Kama Jeshi la Polisi lilivyoanzisha madawati ya jinsia na watoto yanayohudumiwa na askari polisi wenye mafunzo katika eneo hilo, ni wakati sasa baadhi ya watumishi wa mahakama (mahakimu na majaji) wakapata mafunzo maalumu ili wawe maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi hizo ambazo pia zina changamoto nyingi.

Hii ni kwa kuwa mara nyingi waathirika wakubwa wa ukatili huu ni watu wanyonge katika jamii wakiwamo watoto, wanawake, wenye ulemavu na vikongwe.

Ndiyo maana ninasema kuundwa kwa mahakama maalumu kama ilivyo mahakama maalumu kwa wahujumu uchumi maarufu mahakama ya mafisadi, kutasaidia kuharakakisha kesi za namna hiyo na haki itatendeka zaidi kwa kuwa watendaji  wake watakuwa na mafunzo maalumu kuhusu haki za binadamu na usawa wa kijinsia.

Naamini kuwapo kwa mahakama hiyo kutapunguza kasi ya ubakaji na mimba za utotoni kwa wanafunzi, ulawiti, vipigo na mauaji kwa imani za ushirikina.

Ndiyo maana ninasema umefika wakati watunga sera na watunga sheria na mamlaka nyingine husika kuona huruma zaidi kwa waathitrika na kulivalia njuga suala hili ili lishughulikiwe kwa nguvu maalumu hali itakayoleta ukombozi zaidi kwa jamii.

Ukombozi huu utapunguza ukatili huo na taifa lisipokuwa na watu waliofanyiwa ukatili litakuwa na watu wengi zaidi wasiotaka kufanyika kwa ukatili kwao na kwa wengine.

Ndiyo maana ninasema, kama uhujumu uchumi, ukatili wa kijinsia nao unahitaji mahakama maalumu.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5dee458cd53fc5f6a2d6608db1f04d46.png

LEO katika mwendelezo wa makala za ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi