loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maendeleo ya China yanabebwa na sera yake

MAENDELEO ya nchi au taifa lolote duniani hutegemea uhusiano wake na mataifa mengine duniani. 

 

Nchi yenye uhusiano nzuri na mataifa mengine uchumi na maendeleo yake huwa mazuri, lakini uhusiano ukiwa mbaya hata hali yake kimaendeleo hudorora.

 

Hayo yote pamoja na masuala mengine ya uhusiano yanaingia kwenye masuala ya diplomasia na tunapozungumzia masuala ya uhusiano baina ya taifa moja na jingine tunazungumzia masuala ya Sera ya Mambo ya Nje.

 

Duniani kwa sasa taifa la China ndilo linaloongoza kwa uchumi wake kukua kwa kasi sambamba na ukuaji wa miji na idadi ya watu ambao hivi sasa ni takribani watu bilioni 1.5.

 

China imebadilika na inazidi kubadilika kwa kuwa na maendeleo ya kasi sambamba na ukuaji wa miji na majengo ya ghorofa ndefu huko pia matumizi ya teknolojia za kisasa na mtandao wa 5G ukiwa ndio gumzo kwa uchumi.

 

Hayo yote ni kutokana na siasa na utawala bora wa sheria unaozingatia maslahi mapana ya taifa hilo chini ya uongozi wa Rais mwanamageuzi, Xi Jinping aliyeingia madarakani mwaka 2013.

 

Pamoja na mambo mengine, Xi Jinping amebadilisha hali ya uchumi wa taifa hilo na kuongeza marafiki na mataifa mengine kwa kuzingatia mageuzi ya sera ya mambo ya nje ya taifa hilo, ambayo sasa imefungua zaidi milango na kujipambanua kama nchi inayopenda marafiki wa kweli kwa maslahi ya pande zote.

 

China inajipambanua kama taifa lililoendelea kwa amani. Rais Jinping katika Kitabu chake cha ‘The Governance of China’ Toleo la Pili, anasisitiza kuwa nchi hiyo imefanya mageuzi ya kiuchumi na kisera ambapo sera yake ya mambo ya nje imejizatiti kuitangaza nchi hiyo kimataifa na kufungua milango kuongeza marafiki.

 

Moja ya mambo ya msingi anayozungumzia katika kitabu hicho kuhusu masuala ya sera ya nje ya taifa hilo na maendeleo yaliyofikiwa ni kwamba taifa hilo limeendelea na litazidi kuendelea kwa kuzingatia mipango miwili; moja ni ule wa muda mfupi na mwingine ni wa muda mrefu.

 

Katika mipango hiyo moja ni kuhakikisha maendeleo ya taifa hilo yanaakisi maisha ya wananchi kuanzia ngazi ya chini ambako wananchi maskini wanasaidiwa kukua kimaendeleo na Rais Jinping anaamini maendeleo ni lazima yabadilishe maisha ya wananchi kwanza.

Kisha, ili kuendelea kuwa nchi yenye maendeleo endelevu ni lazima uwepo uhusiano mzuri wa ushirikiano na mataifa  makubwa na madogo.

 

Hii ndio sababu China imefungua milango yake kwa mataifa mengine huku ikibuni mikakati ya kimaendeleo na ushirikiano kama vile Mkakati wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja” maarufu kama Belt Road Initiative (BRI).

 

Kupitia mkakati huo wa BRI, China imejizatiti kuboresha ushirikiano na nchi za Afrika, Ulaya,Asia na nchi za Marekani ya Kusini kwa kuboresha miundombinu na kisasa ya barabara, reli, watu, elimu na mingineyo.

 

Pia upo mkakati mwingine wa China uitwao Asia –Pacific uliofungua ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na masuala ya usalama kwa nchi za Ukanda wa Pasifiki ambapo kupitia mikakati hiyo taifa hilo limefanikiwa kujitangaza na kupata washirika wa maendeleo.

 

Jambo la pili ambalo China imefanikiwa kwenye sera ya mambo ya nje ni kuimarisha diplomasia ya ujirani ambapo Rais Jinping anaamini katika maendeleo na siasa bora kila taifa linapaswa kuheshimu taifa jingine kwenye masuala yake ya ndani na maamuzi.

 

Na mfano mzuri ni pale Rais huyo anapozungumzia kwenye kitabu chake hicho kuhusu njia bora za kutatua migogoro katika mataifa yenye malumbano. Akitoa mfano, anasema sio sahihi kwa taifa moja au jingine kuingilia mgogoro wa taifa jingine na kutaka utatuliwe kwa matakwa yao.

 

“Nchi za Afrika ziachwe zitatue migogoro yao kwa kutumia njia zao na kwa kuzingatia sheria zao za nchi badala ya mataifa ya nje kutaka migogoro hiyo kutatuliwa kwa mirengo yao, hili sio sawa. Endapo zitahitaji msaada wa usuluhishi sheria ziko na zitumike lakini sio kuingiliwa mambo yao ya ndani,” anaandika Rais Jingping kwenye kitabu hicho.

 

Katika hilo la ujirani mwema, Rais Jingping kwamba anaongeza nchi rafiki zinaweza kutoa ushauri pale inapobidi, lakini sio kulazimisha nchi husika kufuata matakwa ya nchi nyingine kwani kufanya hivyo ni kinyume cha diplomasia ya ujirani na hiyo inaweza kuharibu uhusiano baina yao.

 

Jambo jingine linalotoa funzo kwenye siasa za China iwapo nchi za Afrika na nyingine zinataka kukua kisiasa ni kuhakikisha zinakuwa kwenye mtangamano wa kikanda kwa ajili ya kukuza ushirikiano na kukua kiuchumi.

 

Ukiacha masuala ya Diplomasia ya Ujirani pia Sera ya China ya nje inaangalia pia uhusiano wake na mataifa mengine na kwamba jambo la msingi ni kuhakikisha maslahi ya taifa hilo nje yanalindwa.

 

China ina ofisi za ubalozi kwenye nchi nyingi duniani, hiyo ni moja ya mbinu yake ya kukuza uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa mengine ambapo mabalozi wake wanahakikisha wanaitangaza na kufungua fursa mbalimbali kwenye nchi wanazowakilisha taifa hilo, jambo ambalo linazidi kujenga na kukuza taifa hilo.

 

China ina historia ndefu ya kuwa nchi yenye uchumi mdogo, lakini baada ya kuanza kufanya mageuzi ya kisera, kiuchumi, kimtazamo ndio ukawa mwanzo wa taifa hilo kukua kwa kasi ya ajabu achilia mbali mrengo wao wa siasa ambao ni wa chama kimoja cha Kikomunisti.

 

Tujifunze kupitia Sera ya Mambo ya Nje ya China ya kufungua milango na kutafuta marafiki na mataifa mengine wa maendeleo na jambo ambalo limefanikiwa. Hivi leo duniani katika kila watu 100, wanne ni Wachina.

 

Katika kutekeleza Sera yake ya Mambo ya Nje, China inapenda kila taifa huru liachwe lifanye mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na taifa jingine na katika hilo, Serikali ya Jamhuri ya Wwtu wa China ilitoa tamko la kuiunga mkono Tanzania katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.

 

Tamko hilo liliionesha dunia kwamba Tanzania ina uwezo wa kusimamia mambo yake yenyewe bila kuingiliwa na nchi za nje. Serikali ya China ilifanya hivyo mara kadhaa kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wu Peng na pia kupitia kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Zhao Lijian na pia kupitia kwa Balozi wa China nchini, Wang Ke.

 

Ni kupitia Sera ya Mambo ya Nje, China ilitambua na kuieleza dunia kwamba mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliendeshwa kwa uwazi, uhuru na haki na hivyo kutoa salamu za pongezi.

 

Kwa hayo machache, China inatoa picha kamili kwamba pamoja na juhudi zake za maendeleo suala la Sera ya Mambo ya Nje limechangia sehemu kubwa ya uchumi na maendeleo yao na kupitia diplomasia yake hiyo inayataka mataifa mengine kutambua na kuheshimu uhuru wa taifa lolote huru na kutoingilia masuala yake ya ndani bali yaongeze bidii kutafuta marafiki.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi