WAKATI Shule za Msingi na Sekondari zikitarajiwa kufunguliwa kesho Januari 11, mwaka huu, Serikali imesisitiza kila mtoto wa kitanzania lazima apate elimu na kwamba kukosa ada na changamoto zingine kisiwe kikwazo kwao.
Serikali ya awamu ya tano ikiongozwa na Rais John Magufuli imejipanga kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ya msingi itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye na imekuwa ikiboresha miundombinu ya shule kama madarasa na kuongeza idadi ya madawati.
Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa Januari 2, mwaka huu alifanya ziara ya kukagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tunduru licha ya kuwasisitiza wanafunzi kutunza miundombinu aliwaomba wazazi kuwapeleka watoto wote shuleni.
Jitihada zote hizo zinafanyika kwa lengo la kuwatengenezea wanafunzi mazingira mazuri yatakayowafanya wanafunzi wavutike na kuona umuhimu wa kupokea elimu wanayofundishwa na walimu wao wakiwa sehemu tulivu isiyokuwa na bugudha.
Ni wazi changamoto ya kukamilisha miundombinu kwa wanafunzi nchini nzima haiwezi kukamilika kwa asilimia kubwa kwa wakati mmoja, kwani idadi ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka kila mwaka na itahitaji kuchukua muda mrefu kwa kuwa serikali inakuwa na mipango mingi ikiwemo kuendesha sekta zingine za maendeleo.
Kutokana na umuhimu wa elimu katika maisha ya mtoto kwa baadaye ni wakati wa wazazi kujipanga kuwapeleka shuleni kwa kuwapa mahitaji yanayotakiwa ikiwemo ada, daftari na vitu vingine vitakavyo wawezesha katika masomo yao.
Kuna baadhi ya wazazi wanatumia sababu ya upungufu wa madawati kukwepa kuwapeleka watoto wao shule ni wakati wa kubadilika kwani serikali kwa kusaidiana na wadau wanajitahidi kuona changamoto hizo zinaisha.
Elimu ina nafasi kubwa ya kuwa chombo muhimu cha kuwatengeza vijana wetu kuishi kwenye maadili yanayotakiwa hususani katika kipindi hiki ambacho mambo mengi duniani yamebadilika na vizazi kuanza kufurahia na kuona mambo mabaya kama sehemu ya maisha yao.
Aidha serikali bado inachukua hatua kali kwa wazazi wote ambao wataonekana kukwamisha watoto wao kupata elimu kwa sababu ambazo wameshazitolea ufafanuzi wanazishugulikia.