Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega amesema Serikali imejipanga kuwekeza kwenye michezo ya vijana ili kuhakikisha sekta ya michezo inasonga mbele kwa kasi.
Ulega amesema hayo akiwa Dar es Salaam alipokuwa anaongea na chombo kimoja cha habari.
“Malengo yetu ni kushirikiana na Wizara zingine kama vile (TAMISEMI) na Wizara ya Elimu kuhakikisha michezo mashuleni kwa maana ya UMISETA na UMITASHUMTA inarejea tena kwa nguvu ya ajabu ili tuweze kupata vipaji huko na kuvilea” amesema Ulega.
Ulega amebainisha kuwa Wizara imepanga kuwa na shule maalum 56 nchini kote ambazo zitakuwa zinaangaliwa kama ‘Center of Excellency’ katika kulea vipaji mbalimbali jambo litakalopelekea kuwa na timu za taifa bora katika michezo mbalimbali.