loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mapinduzi ya Zanzibar yalindwe na Watanzania wote

JANA Watanzania waliungana kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Haya ni mapinduzi yaliyouondoa utawala dhalimu wa kisultani Januari 12, 1964 chini ya uongozi wa Shehe Abeid Amani Karume.

Tunawapongeza Wazanzibari wote kupitia awamu zao nane za uongozi kwa kushikamana tangu kipindi hicho hadi sasa kuhakikisha mapinduzi hayo yanadumishwa na Zanzibar inazidi kuimarika.

Aidha, tunawapongeza Wazanzibari na marais wao katika vipindi vyote vinane kwa kuendeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha ya kuwapo changamoto za hapa na pale ambao kwa uungwana na uzalendo wao, hizo hazikupaswa na hazikuwa sababu ya kuchezea Muungano Tanganyika na Zanzibar wala Mapinduzi hayo matukufu.

Kwa kuwa ni maadhimisho yake ya kwanza akiwa Rais wa Zanzibar, tunapowapongeza Wazanzibari wote kwa kulea ‘mayai’ haya mawili ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano ule wa Aprili 26, 1964, kwa namna ya pekee huku tukimpongeza Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kuiongoza Zanzibar huku uongozi wake ukihakikisha unafuata misingi ya katiba hali iliyomfanya aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo sasa inawatumika vyema Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.

Kama kwamba hiyo haitoshi, tunampongeza Rais wa Awamu ya Saba wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kwa kumaliza salama vipindi vyake viwili vya uongozi na kuikabidhi Zanzibar mikononi mwa Dk Mwinyi ikiwa salama.

Kwa hili, tunasema, hongera Wazanzibari kwa kuwa mnaendelea kujua thamani ya Mapinduzi ya Zanzibar na namna ya kuyalea.

Tunawapongeza Wazanzibari wote kwa kuendelea kuwa makini kuifanya Zanzibar na Tanzania kwa jumla, kuendelea na utamaduni wake unaotamaniwa na mataifa mengi ulimwenguni wa kurithishana uongozi kwa njia ya amani na kwa kuzingatia mwongozo wa Katiba.

Ndiyo maana tunasema Mapinduzi ya Zanzibar lazima yalindwe na Watanzania wote kwa manufaa ya Wazanzibari na Watanzania wote.

Hata sasa tunapotoa pongezi hizo, tunapenda kuwakumbusha Wazanzibari kuwa Uhuru ni Kazi hivyo ili kulinda Uhuru wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, hawana budi kutanguliza uzalendo kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuepusha nchi yaani Zanzibar na Tanzania kwa jumla, dhidi ya utegemezi wa misaada toka mataifa mbalimbali maana kupitia misaada hiyo, ukoloni na utumwa uliondolewa Zanzibar kupitia Mapinduzi hayo matukufu, unaweza kurejea maana penye msafara wa mamba, kenge hawakosekani.

Namna nyingine itakayowawezesha Wazanzibari kuendelea kufurahia matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni Wazanzibari wote kushiriki na kuendesha siasa makini zinazochochea maendeleo ya watu na si siasa za ‘majitaka’ zilizo tayari kushuhudia watu wakimwaga damu ili baadhi ya watu waingie madarakani na kukidhi matakwa ya mabeberu wanaowatuma.

Ndiyo maana tunasema mnapowajibika kuyalinda mapinduzi haya ili mzidi kunufaika nayo katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kiulinzi, kisiasa, kitamaduni, kiuchumi na kijamii, endeleeni kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwa kuzingatia kuwa, wapo watu wenye mawazo ya kijamaa katika nchi za kibepari na kadhalika, wapo watu wenye mawazo ya kibepari katika nchi za kijamaa hivyo, wanaotaka kuvuruga amani ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kisingizio cha mgongo wa siasa, katu wasipate nafasi.

Ndiyo maana tunasema Mapinduzi ya Zanzibar yalindwe na Watanzania wote.

 

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi