loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kwa mapinduzi haya ya kiuchumi, Zanzibar mpya inakuja

NI miaka 57 sasa tangu Wazanzibari wachache wajitoe muhanga kuongoza Mapinduzi Matukufu yaliolenga kujiondoa katika unyonge, ukandamizaji na madhila ya utegemezi wa utawala wa kisultani visiwani humo.

Hatua hiyo ndiyo inatuwezesha kuwa na Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayoadhimishwa kila mwaka Januari 12.

Mwaka huu katika maadhimisho hayo jana, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyehutubia kwa mara ya kwanza akiwa Rais katika maadhimisho hayo, pamoja na mambo mengine, alieleza maeneo muhimu ya kuifikisha Zanzibar katika mapinduzi makubwa ya kiuchumi hasa yanayobeba maana halisi ya siku hiyo.

Rais huyo wa Awamu ya Nane wa Zanzibar katika hotuba yake alisema, kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wakiongozwa na Shehe Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar huru katika mapinduzi hayo, ni kuwaenzi kwa kuendeleza shabaha yao ya kuondoa unyonge, madhila na kuwarejeshea Wazanzibari utu wao na ari ya kuendeleza nchi yao.

Ili kufikia katika dhamira hiyo ya mapinduzi makubwa ya kiuchumi, Dk Mwinyi alisema hatua ya mwanzo ilikuwa ni kujenga maridhiano na umoja wa kitaifa ikiwa ni takwa la Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo la 2010 linalomtaka Rais kuunda Serikali ya Umoja kwa Kitaifa.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, hatua ya pili baada ya maridhiano ni kuwekeza katika uvuvi ili wavuvi wavue kwa zana za kisasa na Wazanzibari wanufaike kwa rasilimali za bahari kuu.

Nyingine ni kuweka nguvu katika kilimo kwa kuongeza tija ili kuondoa utegemezi wa chakula kutoka nje ya Zanzibar na kuinua zao la karafuu na mwani.

Aidha, Dk Mwinyi alisema Zanzibar inalenga kufanyia maboresho ya sheria mbalimbali na taasisi ili wafanyabishara wafanye shughuli zao bila usumbufu na vikwazo.

Eneo lingine ni katika sekta ya sanaa na michezo ambapo anasema kila Mzanzibari anapaswa kutumia kipaji chake kwa kadri ya uwezo wake kujiendeza kimaisha na kujiongezea kipato.

Mapinduzi makubwa yatafanyika pia katika utumishi wa umma ili kujenga uwajibikaji kuboresha utoaji wa huduma na kujenga maslahi ya watumishi wa umma.

Dk Mwinyi anasema haya yatawezekana kupitia mambo makuu mawili; kwanza kufungua uchumi kwa kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi (kuvutia uwekezaji ndani na nje kuendeleza uchumi) kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha biashara cha Ukanda wa Afrika Mashariki.

Pili, kuongeza makusanyo ya kodi ili kuendelea na kupanua utoaji wa huduma za elimu, afya na nyinginezo.

Mageuzi haya yanapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote ikiwa kweli tunataka maana halisi ya Mapinduzi Matukufu yaliodhimishwa jana ionekane katika maisha ya wananchi.

Kazi ya kufikia mambo haya makubwa yalioelezwa na Dk Mwinyi, si yake wala Serikali peke yake, bali ni ya Wazanzibari wote na Watanzania kwa jumla kwa kuwa Mapinduzi hayo ndio yaliyozaa Zanzibar huru iliyoungana na Tanganyika huru na kupata nchi nzuri ya Tanzania.

Binafsi naamini katika nguvu ya pamoja kuyafanikisha haya kwani siku zote umoja ni nguvu. Wazanzibari msibweteke, kasi hii ya Serikali iungwe mkono kwa maslahi mapana ya wote.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi ...

foto
Mwandishi: Na Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi