loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi apania biashara EAC

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema mapinduzi ya kiuchumi ni njia muhimu ya kujibu changamoto za sasa na za vizazi vijavyo, hivyo anataka kurudisha hadhi ya visiwa hivyo katika biashara Afrika Mashariki.

Dk Mwinyi alisema mjini Unguja jana kuwa, mapinduzi hayo yanawezekana kwa kutekeleza mambo mawili ikiwamo kuufungua uchumi kwa kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi.

Alisema hayo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja wakati akihutubia taifa katika kilele cha sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia mwaka 1965 hadi 1969 zilikuwa zikifanyika katika viwanja vya Mnazi Moja hadi ulipokamilika uwanja wa michezo wa Amaan ambao ulifunguliwa Januari 12, 1970 na Rais wa Tanzania, Julius Nyerere na kuanzia hapo zikiwa zinafanyika uwanjani hapo.

Wazanzibari Januari 12, 1964 walifanya Mapinduzi yaliyoongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kumuangusha mtawala wa mwisho Jemshid bin Abdallah Al-Said aliyetawala kuanzia Julai Mosi, 1963 mpaka alipopinduliwa Januari 12, 1964.

“Ni azma ya serikali yangu kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ili kuendeleza uchumi wetu, lengo ni kuifungamanisha sekta ya uvuvi na utalii kwa kupanua shughuli za utalii ukiwamo uwekezaji wa utalii kisiwani Pemba.

” “Tunataka kurudisha hadhi ya Zanzibar kama kituo cha biashara cha ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Dk Mwinyi na kuitaja njia ya pili ya kuwezesha mapinduzi ya kiuchumi ni kuongeza makusanyo ya kodi. Alisema Zanzibar inahitaji kuongeza ukusanyaji kodi ili iendelee na iongeze utoaji wa huduma za elimu, afya na nyinginezo.

“Tunapaswa kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi ili wavuvi wetu wavue kwa zana za kisasa na tuweze kufaidika na rasilimali za bahari kuu.

Tunapaswa kuleta mapinduzi katika kilimo ili wakulima wetu waongeze tija na kutuondoleza utegemezi wa chakuka kutoka nje ya Zanzibar pamoja na kuinua zao la karafuu na mwani,” alisema.

Katika sherehe hizo ambazo ni za kwanza kwa Dk Mwinyi tangu achaguliwe kuwa Rais wa Zanzibar, visiwa hivyo pia vinahitaji mapinduzi katika sheria ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao bila usumbufu au vikwazo.

“Tunahitaji mapinduzi katika sanaa na michezo ili kila Mzanzibari aweze kutumia kwa kadri ya uwezo wake kipaji chake kujiendeleza kimaisha na kuongeza kipato,” alisema.

Dk Mwinyi alisema Zanzibar inahitaji mapinduzi katika utumishi wa umma, kujenga uwajibikaji, kuboresha utoaji huduma, na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.

Kupunguzwa shamra shamra

Alisema sherehe za Mapinduzi mwaka huu zimefanywa kwa namna tofauti na ilivyozoeleka kutokana na hali ya uchumi.

“Kama mnavyofahamu hali ya uchumi wa dunia imeyumba sana kutokana na madhara ya ugonjwa wa covid- 19 hivyo basi tumelazimika kupunguza baadhi ya shamrashamra ili fedha tutakazookoa tuzielekeze kufidia mapengo ya wajibu wa serikali kwa wananchi ikiwamo huduma za elimu, afya na nyinginezo,” alisema.

Alisema hali hiyo ni ya mpito na siku zijazo hali ikiwa ya kawaida sherehe hizo zitaadhimishwa kama ilivyo kawaida.

“Naamini mtatuelewa na kutuunga mkono katika nia na dhamira yetu hii njema,” alisema na kubainisha kuwa shabaha ya mapinduzi ni kustawisha maisha ya Wazanzibari.

Maridhiano

Dk Mwinyi alisema umoja wa kitaifa ni nguzo muhimu katika kuijenga Zanzibar mpya, hivyo miongoni mwa hatua za mwanzo alizochukua ni kujenga maridhiano na umoja wa kitaifa.

“Kwetu sisi viongozi kazi iliyo mbele yetu ni kuyatafsiri maridhiano haya katika kuwaletea neema Wazanzibari,” alisema.

Mapinduzi kulindwa

Alisema Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yataendelea kulindwa na kuenziwa kwa kuwa ni kielelezo cha Wazanzibari kujikomboa na kuwa huru.

Alisema mafanikio makubwa yamepatikana ikiwamo sekta ya elimu ambapo kasi ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari inaendelea Unguja na Pemba zikiwamo shule za ghorofa ili kuweza kuchukuwa idadi kubwa ya wanafunzi.

Aidha alisema kasi ya ujenzi wa vyuo vya amali inaendelea ambao lengo lake kubwa ni kutoa mafunzo ya kazi za amali kwa wananchi ili waweze kujiajiri wenyewe.

Aliwapongeza wazazi kwa kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wao kuanza shule za maandalizi na msingi ambayo sasa imefanywa kuwa ya lazima.

Katika sekta ya afya, Dk Mwinyi alisema anakusudia kuimarisha huduma hizo kuwa bora na kwamba kwa sasa serikali ipo katika mchakato wa ujenzi wa hospitali kubwa ya rufaa huko Binguni wilaya ya Kati Unguja ambayo itazalisha wataalamu bingwa pamoja na vifaa na miundombinu.

‘’Napenda kuwajulisha wananchi wa Zanzibar kwamba Serikali yenu itaendelea kutoa huduma zote muhimu za kijamii na maendeleo ikiwAmo sekta ya afya na elimu bure kwani hayo ndiyo matunda ya Mapinduzi ambayo ni urithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu’’alisema.

Alizitaja sekta nyingine ambazo zitaendelea kuimarishwa ni usambazaji wa nishati ya umeme hadi vijijini kwa ajili ya kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo.

‘’Tutaendelea kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii ikiwAmo maji safi na salama pamoja na usambazaji wa nishati ya umeme hadi vijijini kwa lengo la kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi,’’alisema Dk Mwinyi.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kubadilika na kuongeza ufanisi wa kazi unaotokana na uwajibikaji ili kuleta ufanisi.

Alisema katika eneo hilo amejikita zaidi kupambana na rushwa na kuipa uwezo Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) kuongeza kasi ya kushughulikia masuala ya rushwa kwa watumishi wa umma wanaokwepa uwajibikaji.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi