Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amewataka wafugaji na wakazi wanaozunguka hifadhi za taifa zilizopo wilayani Chato mkoani Geita kuacha mara moja kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi hizo kwa lengo la kutunza mazingira.
Dk Ndumbaro amebainisha hayo alipofanya ukaguzi wa shamba la miti la Biharamulo lililopo wilayani humo na kusema kuwa mtu yoyote atakayeingiza mifugo yake katika hifadhi hizo mifugo yake itataifishwa.
“Naitangaza Wilaya ya Chato kuwa kitovu cha uhifadhi na utalii kwa Kanda ya Ziwa, kutokana na Wilaya hii kuwa na vivutio vingi vya kitaali hivyo asitokee mtu akaingiza mifugo yake ndani ya hifadhi kwakuwa mifugo uharibu mazingira ya hifadhi” amesema Ndumbaro.