loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maofisa ugani watakiwa kuwashauri wanufaika Tasaf

SERIKALI imewataka maofisa ugani nchini kuwatembelea na kuwapa ushauri wa kitaalamu wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ili waweze kutekeleza kwa ufanisi zaidi miradi wanayoanzisha kwa ajili ya kujiingizia kipato na kujikomboa kiuchumi.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi alitoa agizo hilo juzi katika mji mdogo wa Mtinko, Halmashauri ya Wilaya ya Singida wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani hapa kuangalia na kujionea namna mpango huo unavyonufaisha walengwa.

"Lengo kuu la mpango huu ni kumtoa mlengwa kutoka katika umasikini na kumboreshea maisha yake. Kwa mfano, kama alikuwa anaishi kwenye nyumba ya tembe aweze kujenga nyumba ya bati. Katika juhudi zao mbalimbali wengi wao huanzisha miradi lakini kwa vile hawana wataalamu wa kuwaelekeza huwa hawafanikiwi vya kutosha."

“Hilo ni jukumu lenu, hivyo kuanzia sasa hakikisheni mnawatembelea na kuwapa maelekezo ya kitaalamu walengwa wote ili waweze kufanikiwa zaidi kwenye miradi yao mbalimbali wanayoanzisha ili kuondokana na umasikini," alisema.

Ndejembi aliwakumbusha wanufaika wa mpango huo wa Tasaf kuelewa kuwa malengo ya mpango huo si kufanikisha anasa zao bali kuboresha maisha yao huku akiwasihi wasiache kufanya maendeleo kwa kuogopa kuondolewa kwenye mpango huo.

Wakati huo huo, Ndejembi ametoa onyo kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, wakurugenzi wa miji, manispaa na majiji ambao wamekuwa na tabia ya kuwakata  fedha wanufaika wa mpango huo ili kulipia michango mbalimbali katika maeneo yao ikiwamo Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kuacha mara moja.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Theophil Ishengoma alieleza kuwa halmashauri hiyo imepokea Sh bilioni 13.58 kutoka Serikali Kuu kupitia Tasaf, ambapo walengwa 7,407 kutoka vijiji 40 wananufaika na fedha hizo.

foto
Mwandishi: Abby Nkungu, Singida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi