Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu amesema Serikali imeamua kuwa mtu yoyote anayefanya biashara ya chuma chakavu atapewa kibali kimoja na sio vitatu tena kama ilivyokuwa hapo awali.
Ummy amesema hayo leo alipokutana na wadau wanaojihusisha na shughuli ya ukusanyaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu.
“Kuanzia sasa tumebadilisha mfumo wa utoaji wa vibali ambapo awali mtu alipaswa kuwa na vibali vitatu ambavyo ni kibali cha ukusanyaji, uhifadhi pamoja na kile cha usafirishaji” amesema Ummy.
Amesema kwa sasa kibali kitakuwa kimoja ila kitakuwa na maelezo yanayomtambulisha muhusika anafanya shughuli ipi ambapo inaweza kuwa moja au zote tatu” amesema Ummy.
Aidha, Ummy amesema kikao hicho kimetoka na maadhimio kadhaa ikiwemo upitiaji wa tozo mbalimbali za biashara hiyo ili kuhakikisha inachangia utunzaji na uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa uchumi wa nchi.