loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Udanganyifu wa mitihani wapungua

UDANGANYIFU katika mitihani umepungua hatua ambayo Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limeielezea kuwa imechangiwa na wananchi kutoa taarifa juu ya mikakati ya wizi iliyokuwa imepangwa na shule mbalimbali.

Akitangaza matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne, na mitihani ya upimaji ya Kidato cha Pili na Darasa la Nne iliyofanyika mwaka jana kwa nyakati tofauti, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema kwa kuangalia takwimu za waliofutiwa matokeo, udanganyifu umepungua.

Katika taarifa hiyo, pamoja na kubainika kwa dosari za udanganyifu ambazo Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 215, Dk Msonde alisema udanganyifu umepungua kwa kiwango kikubwa na hali hiyo imechangiwa na wananchi kutoka taarifa juu ya mikakati ya wizi iliyokuwa imepangwa na shule mbalimbali.

 

Waliobainika kufanya udanganyifu mwaka huu, 77 ni wa darasa la nne, 63 wa kidato cha pili na 75 ni wa kidato cha nne ambao hawatapata tena nafasi ya kuendelea na masomo kwenye shule za serikali popote nchini.

 

Adhabu hiyo inazingatia Sheria ya Baraza la Mitihani Kifungu cha 5(2) (i) na (j) Sura ya 107 kikisomwa pamojana kifungu cha 30(2) (b) 2016 cha Kanuni za Mitihani.

 

“Ukiangalia takwimu za waliofanya udanganyifu, wamepungua sana na sababu kubwa ni; kuwashukuru wananchi wa Tanzania wamekuwa wema sana. Wametoa taarifa za awali kwetu sisi juu ya mikakati na mipango mbalimbali iliyokuwa imepangwa katika shule mbalimbali,” alisema Dk Msonde.

 

Aliongeza, “Wakati tunatangaza matokeo ya darasa la saba (mwaka jana), tulibainisha shule 71 ambazo wananchi waliziripoti na waliendelea kutaja shule nyingine 26 zilizopanga njama hiyo. Tulizionya shule mapema zisijaribu kufanya hivyo. Na kamati zetu za halmashauri, wilaya na mikoa zilielekezwa. Unachokiona ndiyo udhibiti wenyewe uliotokea.”

 

Akishukuru na kupongeza kamati za mikoa za mitihani kwa usimamizi mzuri, alisema ifike mahala walimu wote wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari waseme sasa ni mwisho kwa vitendo hivyo vya udanganyifu katika mitihani.

 

“Tumeanza vizuri na wanafunzi watambue wazi kuwa kufaulu inawezekana bila kufanya udanganyifu. Madhara makubwa yapo tunapofanya udanganyifu katika taifa letu,” alisema.

 

Katika matokeo ya kidato cha nne na maarifa QT, kidato cha pili  na darasa la nne ya mitihani iliyofanyika mwaka 2019 na kutangazwa mwaka jana, Necta ilifuta matokeo ya watahiniwa 333 waliofanya udanganyifu katika mtihani .

 

Novemba mwaka jana, akitangaza matokeo ya darasa la saba, Dk Msonde alisema watahiniwa 1,059 walifutiwa mitihani kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufanya udanganyifu.

 

Kitendo cha wanafunzi kufutiwa matokeo kimekuwa kikilalamikiwa na wadau mbalimbali kwa kunyooshea vidole shule na uongozi kwa jumla kwa kukatisha ndoto za watoto huku ikielezwa kuwa upo uwezekano wa watoto hao wenye umri wa chini ya miaka 14 kulazimishwa kushiriki udanganyifu. 

 

Baada ya watoto hao zaidi ya 1,000 wa darasa la saba kufutiwa matokeo, baadhi ya wadau wa elimu walinukuliwa na gazeti hili wakiomba Necta iwasamehe kwa kuwapa fursa ya kufanya tena mtihani.

 

Hata hivyo, wadau wa elimu walisisitiza walimu na wote wanaohusika katika udanganyifu kuchukuliwa hatua kubwa ikielezwa kwamba wakiachwa, italeta shida katika jamii kwa kuwa na wasomi wasio na sifa.

 

Hata hivyo, Dk Msonde alisema sheria ni msumeno, hukata kuwili na kusisitiza kuwa wale wote waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani wa darasa la saba na kufutiwa, hawatapata tena nafasi ya kuendelea kusoma kwenye shule zozote za serikali nchini, ila wanaweza kusoma shule binafsi.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof  Sospiter Muhongo ameanzisha ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi