loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dodoma yaonya ununuzi wa viwanja kupitia madalali

MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amewataka wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali hasa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza kuacha mtindo wa kununua viwanja kwa madalali kuepuka kuuziwa maeneo ya makaburi, barabara na hifadhi ya misitu.

Akizungumza katika mkutano ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge uliolenga kukutanisha taasisi zinazohusika na miundombinu jijini humo, Mafuru alisema jiji hilo lina mpango kamambe wa miaka 20 (2019-2039) ambao wanatakiwa kuutumia kujua maeneo kabla ya kununua.

"Wawekezaji kabla ya kununua kiwanja kwa dalali, wafike ofisi za jiji kuona eneo hilo analotaka kununua limepangiwa matumizi gani," alisema.

Alisema madalali wengi wa jiji hilo  walikuwa wafanyakazi wa iliyokuwa Mamlaka ya  Ustawishaji Makao Mkuu (CDA) hivyo wana uzoefu na wanajua maeneo mengi vizuri, hivyo wawekezaji wasihadaike na kuwaamini bali wafike kwanza ofisi za jiji kujiridhisha kabla ya kununua.

Mafuru alisema, madalali hao wamekuwa wakitumia udanganyifu kwamba viwanja katika jiji hilo vimekwisha jambo ambalo si kweli. Alisema jiji hilo lina viwanja vya kutosha kwa matumizi mbalimbali ya biashara, huduma na makazi.

Akiwasilisha mkakati wa uboreshaji miundombinu wa jiji, Ofisa Mipango Mji  wa jiji la Dodoma, Aisha Masanja alisema kati ya Julai 2017 na Desemba 2020, kuna viwanja 392,837 ambavyo vimeandaliwa katika maeneo mbalimbali katika kata 19 kati ya 41 zilizopo katika jiji hilo, hivyo si kweli kwamba viwanja vimeisha.

Mafuru alisema mkakati wa jiji ni kusambaza miundombinu ya maji, umeme, barabara na huduma nyingine. Katika bajeti ya mwaka 2021/22 jiji linatarajia kutenga fedha kwa ajili ya kusaidiana na Tarura.

Jiji litasaidiana na Tarura katika ujenzi wa madaraja matatu eneo la Mtumba na kufungua barabara katika maeneo mbalimbali na kuimarisha barabara katika mradi mkubwa wa Nala.

Pia katika bajeti ya mwaka 2021/22 litatenga fedha kwa ajili ya kuchangia katika bajeti ya Duwasa na Ruwasa ili kusaidia katika uchimbaji wa visima na miundombinu ya maji katika maeneo yaliyopimwa na yanakua kwa kasi.

Pia Jiji hilo litahakikisha linafikisha miundombinu katika viwanja 69,353 ambavyo vilipimwa na CDA kati ya mwaka 1973 hadi Juni 2017 ambavyo kati yake, viwanja 14,081 vimemilikishwa wananchi katika maeneo mbalimbali havina miundombinu ya barabara, maji na umeme.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof  Sospiter Muhongo ameanzisha ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi