Baraza la Mitihani nchini (NECTA) limekanusha taarifa za kuwa shule tisa kati ya kumi zilizoburuza mkia katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana zinatoka Mkoa wa Mtwara.
Taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Uhusiano wa baraza hilo, John Nchimbi imebainisha kuwa taarifa hizo zililenga kuuchafua mkoa huo na kuwaomba wananchi kuzipuuzia taarifa hizo.
“Baraza linapenda kuujulisha umma kuwa taarifa hizo ni za uongo na zinalenga kuupotosha umma, kuleta taharuki na kudhalilisha Mkoa wa Mtwara.” Amesema Nchimbi
Nchimbi amefikia kutoa kauli hiyo mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa mapema hii leo kulitaka baraza hilo kutoa ufanuzi juu ya taarifa hiyo.