loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakulima miradi ERPP sasa kazi kwenu

LEO katika gazeti hili tumeandika taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, kwamba wizara hiyo kupitia mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga (ERPP) imefanikiwa kukamilisha miradi kumi na moja iliyopo mkoani Morogoro.

Aidha katika taarifa hiyo katibu mkuu huyo alisema kwamba miradi hiyo itakabidhiwa kwa wakulima mwisho wa mwezi huu.

Kauli aliyoitoa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya inaleta matumaini makubwa kwa wakulima wa mpunga ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakihangaika kuongeza tija katika kilimo chao na kushindwa. Kwa kuleta taarifa hiyo inadhihirisha ni kwa jinsi gani serikali inatilia maanani maendeleo ya kilimo nchini ambacho ndio ajira kubwa kwa wananchi.

Mradi huo ambao ulijumuisha ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na skimu ya umwagiliaji ni sehemu muhimu ya juhudi za serikali za kubadili kilimo kuwa kilimo biashara ambapo wananchi wanakuwa na chakula cha kutosha na kingine kuuza kwa ajili ya kukuza kipato cha kaya.

Wakati tunaipongeza serikali kwa kufanya nafasi yake tunapenda kuwahimiza wakulima waliokuwa katika miradi hiyo kuwa makini nayo ili iwe endelevu.

Kazi iliyofanyika katika wilaya za Mvomero, Kilombero na Kilosa mkoani Morogoro kwa fedha nyingi za umma inafaa kuendelezwa ili kuwa na faida ya fedha hizo.

Kwa kuwa Mradi wa ERPP ulilenga kujenga maghala matano, skimu za umwagiliaji tano na maabara moja ya kilimo kwenye wilaya hizo ni matarajio yetu kuwa kutakuwa na matokeo chanya na kuleta msukumo mpya katika kilimo cha mpunga.

Kama alivyofarijika Katibu Mkuu Kusaya kuona miradi yote ipo tayari kukabidhiwa kwa wakulima nasi pia huku tukihimiza serikali pia kuendelea kupeleka watumishi wake katika miradi hiyo ili isizimike kama ilivyozimika miradi mingine ya kilimo nchini.

Tunasisitiza kama alivyosema Kusaya wakulima mkoa wa Morogoro ambao mradi wa ERPP umetekelezwa kuitunza miradi hiyo iliyogharimu fedha nyingi za serikali ili idumu na kunufaisha vizazi vijavyo.

Heshima kubwa ambayo wakulima wanaweza kuipatia serikali ni kuitunza miradi hiyo ili waongeze uhakika wa upatikanaji chakula na kipato cha kaya na kuchangia kukuza uchumi wa wakulima wa zao la mpunga.

Kwa kuwa katika kipindi cha miaka minne, mradi huu unaonesha kwamba umefanikiwa katika malengo yake ya kupeleka mbegu bora, kuboresha skimu za umwagiliaji na kujenga maghala matano ya kuhifadhia nafaka, kazi iliyobaki ni kuhakikisha kwamba mradi unakuwa endelevu.

Haitakuwa na maana kwa wakulima kuzembea katika kutunza miradi na malengo yake na hivyo kurudisha mafanikio ya kuwa na uzalishaji wa tani tano kwa hekta kutoka tani mbili za mwaka 2016.

Kwa kuwa Mradi umefanikiwa kufanya wakulima wa Morogoro kuwa na uhakika wa chakula kwa familia na sasa ziada inatumika kuuza kwenye masoko na kuwapatia kipacho cha uhakika, wadau wa kilimo na maofisa wa serikali kutoka wizara ya kilimo wanatakiwa kutupia macho miradi hii hata kama imekabidhiwa kwa wakulima ili maana ya uwapo wake ionekane wazi.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi