loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Halmashauri tekelezeni ujenzi miundombinu ya shule

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi limetangaza matokeo ya mitihani ya kujipima kwa Darasa la nne, kidato cha pili lakini kubwa zaidi ni matokeo ya kuhitimu elimu ya Sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha nne.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA Dk Charles Msonde , alisema kwa ujumla ufaulu wa mitihani katika matokeo ya mwaka huu umeonyesha kuongezeka kwa wastani wa asilimia 5.19 ya ufaulu ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2019.

Kwa mujibu wa Dk Msonde watahini 340,219 wa Mwaka 2019, walifaulu mtihani huo wakati mwaka 2020 watahiniwa 373,958 sawa na asilimia 85.84 ya watahiniwa 443,654 wamefaulu mtihani huo na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano katika shule mbalimbali.

Aidha inatajwa kuwa miongoni mwa wahitimu hao waliofaulu, wavulana wameongoza kwa asilimia 86.27 na wasichana asilimia 85.44 huku ubora wa ufaulu wa madaraja kuanzia 1 hadi III ukiongezeka kwa asilimia 35.10 ukilinganishwa na Mwaka 2019 uliokuwa asilimia 32.01.

Kimsingi kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi hao kunazidi kuchagiza fursa ya maendeleo ya ukuaji wa elimu hapa nchini ingawaje pia kunazidi kuibua changamoto mashuleni hususani zinazotokana na upungufu wa kiasi fulani cha miundombinu ya ufundishaji.

Ikumbukwe katika kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, Serikali imekuwa ikisisitiza uboreshaji wa miundombinu katika shule zote zikiwemo za msingi na Sekondari kwa lengo maalumu ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Kulingana na maagizo mbalimbali yaliyotolewa kwa nyakati tofauti na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo, halmashauri zote nchini zinapaswa kuhakikisha hadi ifikapo Februari 28 Mwaka huu ziwe tayari zimekamilisha miundombinu hiyo ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo yao.

Lakini wakati hilo la miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza likiendelea kutafutiwa ufumbuzi, tayari matokeo ya kidato cha nne yametoka hali inayozilazimu halmashauri hizo pia kuanza maandalizi mengine kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano.

Kimsingi kila jambo ni hatua na kwenye malengo ya kweli basi mafanikio huonekana, kikubwa wakurugenzi wa halmashauri, maafisa elimu na wote mnaohusika kwa namna moja au nyingine na usimamizi wa elimu ndani ya halmashauri hizo kusimama kidete ili kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wote waliopata nafasi.

GAUDENCIA (31) na Modesta (27) ni ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi