loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wadau wachambua siri ufaulu kupaa

WADAU wa elimu wameendelea kuweka bayana mambo yanayochangia ufaulu wa wanafunzi katika mitihani, wakisema siri kubwa ni mazingira bora ya kusoma ikiwamo walimu wazuri, ushirikiano wa wazazi na wanafunzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wamiliki wa shule, wanafunzi, wazazi na mamlaka za usimamizi zilizofanya vizuri katika matokeo ya mwaka huu, wamekiri kuwa mambo hayo ni chachu kwa shule na wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma.

Mshikamano waipaisha Ilala

 

Akizungumzia Halmashauri ya Ilala, jijini Dar es Salaam ambayo imekuwa miongoni mwa halmashauri 10 bora kwenye matokeo ya darasa la nne mwaka 2020, Mkurugenzi wake, Jumanne Shauri alisema wamejizatiti katika mshikamano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.

Alisema wanajiandaa kuwapongeza walimu kwa kuwatambua na kuwapa vyeti vya motisha.

Alisema Manispaa ya Ilala imeandaa utaratibu wa kuwatambua walimu ambao masomo yao yamepata ufaulu mzuri kwa kuwapa vyeti. Watafanya hivyo pia kwa walimu wote walioongeza juhudi za ufaulu kwenye masomo husika na wale walioendelea kushikilia ufaulu huo nzuri.

“Pia tunaangalia jinsi ya kuwapa pia vyeti ya kuwatamba wanafunzi waliofanya vizuri ili iwe motisha kwa wengine, shule zilizofanya vizuri nazo tutaangalia kwa baadaye utaratibu labda wa kuwapa fedha kidogo kama motisha kwa maana tuna shule nyingi hivyo hatuwezi kuwapa walimu wote fedha…,” alisema.

Lindi ilivyohudumia walimu

Ofisa Elimu wa Sekondari, mkoa wa Lindi, Omary Maje alisema utoaji wa mitihani ya mara kwa mara kwa wanafunzi, kujua na kutatua changamoto za walimu ni miongoni mwa mambo ambayo wanaamini yamewezesha kufanya vizuri kwenye ufaulu  katika kidato cha nne kwa asilimia 94.3 kwa mwaka 2020/2021.

 

Kulingana na matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili na cha nne yaliyotangazwa juzi na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde,  mkoa wa Lindi umeshika nafasi ya pili kwa mikoa mitatu iliyofanya vizuri zaidi katika matokeo ya darasa la nne.

Pia inashika nafasi ya kwanza kwa mikoa mitatu iliyoongeza ufaulu mfululizo katika matokeo hayo ya darasa la nne kwa kupanda wastani wa asilimia 3.

 

Ofisa elimu huyo wa mkoa alisema mara nyingi fedha zinapoingizwa kutoka serikali kuu au kwa wadau, suala la kwanza ambalo wamekuwa wakifanyia kazi ni kushughulikia walimu kuhakikisha madai yao yanapunguzwa au kumalizwa.  

 

Alisema pia wamekuwa wakifuatilia upandaji wa madaraja ya walimu wakitambua kuwa ni miongoni mwa mambo yanayoleta ari ya kazi kwa walimu.

 

Akizungumzia upungufu walimu wa masomo ya sayansi, alisema  kila idara ya elimu iliweka kambi kusimamia mada ngumu ikiwa ni pamoja na walimu kutoka kituo kimoja kwenda kingine kuwezesha wanafunzi kufundishwa.

 

Kwa mujibu wa ofisa elimu, ufaulu katika Manispaa ya Lindi mwaka 2018 ni asilimia 82, mwaka 2019 ni 91.7 na ufaulu 2020 ni 94.4.

 

 

Arusha yashukuru wazazi, walimu

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, maofisa elimu sekondari na Msingi jijini Arusha, wameshukuru ushirikiano uliopo baina ya wazazi ,walezi ,kamati za shule pamoja na walimu na kuwezesha mkoa kushika nafasi ya tatu kitaifa matokeo ya darasa la nne na kidato cha pili kufaulisha kwa asilimia 98.

 

Ofisa Elimu Sekondari,Valentine Makuka alisema mafanikio hayo yametokana na mikakati waliyojiwekea kwa kushirikiana na walimu,wazazi pamoja na kamati za shule.

 

Ofisa Elimu Msingi Jiji la Arusha,Omar  Kwesiga alisema miongoni mwa mikakati waliyojiwekea ni kuhakikisha wanafunzi wa darasa la awali ,la kwanza ,pili na la tatu wanajua kusoma,kuandika na kuhesabu (KKK).

 

Pia ufuatiliaji wa mara kwa mara wa masomo na ufundishwaji wa walimu kwa kufuata mitaala, kamati za shule ikiwemo mitihani ya mara kwa mara.

 

Walipe walimu vizuri

 

Mmiliki wa Shule ya Msingi Hannah Bennie (HBS)  iliyoongoza kwa ushindi wa matokeo ya darasa la nne katika Halmashauri ya Kigamboni, Dar es Salaam, Massu Nghwani alisema mazingira mazuri ya kusomea ikiwamo malipo mazuri kwa walimu ni chachu ya ufaulu kwa wanafunzi katika shule mbalimbali. "Walipe vizuri, wape nyumba ya kuishi kwa utulivu, watafanya kazi kwa moyo."

 

Msichana 10 bora azungumza

 

Mmoja wa wasichana bora katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2020, Rose Peter Kaale (15) kutoka Shule ya Sekondari Precious Blood ya Arusha, ameeleza siri ya mafanikio hayo kuwa yamewezeshwa kwa kiwango kikubwa na ushirikiano wa wazazi,walimu na yeye binafsi.

“Shuleni kulikuwa na ushindani, kila mwanafunzi anasoma kwa bidii na kila mmoja alikuwa anataka afaulu sasa hiyo pekee inakufanya nawe usome,lakini pia mazingira ya kujifunzia shuleni ni mazuri na walimu walitutia moyo na kutufundisha kwa juhudi,”alisema Rose.

 

Viongozi washauriwa

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema kauli mbaya za viongozi kwenye mikoa na halmashauri mbalimbali nchini dhidi ya walimu zina uhusiano mkubwa na matokeo.

Akizungumza na gazeti hili, Mtaka alishauri viongozi kujizuia kutoa lugha zinazokwamisha utendaji kazi wa walimu. Alisema siri kubwa ya mafanikio kielimu mkoani kwake ni ushirikiano baina ya viongozi,walimu,wazazi na wanafunzi uliojengwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi kijiji.

Katika taarifa ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Msonde, Halmashauri ya Meatu katika mkoa wa Simiyu, imeongeza ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo.

 “Meatu mwaka 2015/16 ilikuwa Halmashauri inayoongoza nchini kwa kufeli kielimu, ilikuwa ina shule zinazoshika mkia kitaifa, lakini tukakaa na walimu, wazazi na wanafunzi, tukagundua Meatu ni eneo la wafugaji, hivyo shule siyo kipaumbele kwao, tukawaelimisha wazazi, tunarudi kwa walimu na wanafunzi, leo Meatu inaongoza kwa kuongeza ufaulu darasa la nne’’,alisema Mtaka.

Alisisitiza kuwa siri kubwa ya kufanya vizuri ukaribu wa wazazi,walimu huku akisisitiza kuwa changamoto zote za elimu zenye uwezo wa kushughulikiwa ndani ya mkoa, zishughulikiwe ikiwemo viongozi kuwa na kauli nzuri kwa walimu.

Habari hii imeandikwa na Ikunda Erick, Dar, Veronica Mheta, Arusha na Kennedy Kisula, Lindi

 

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof  Sospiter Muhongo ameanzisha ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi