KOCHA Msaidizi wa Simba Selemani Matola amesema wanahitaji kufanya maandalizi ya mapema kujiandaa na hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya timu kupangwa kwenye makundi zinarudi Februari kucheza hatua hiyo kutafuta nafasi ya kuingia robo fainali katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Akizungumza Dar es Salaam Matola alisema anatambua ugumu wa michuano ile ila hana wasiwasi kwasababu wachezaji alionao wengi ni wazoefu na waliwahi kucheza msimu wa mwaka juzi.
“Kundi letu ni gumu sio rahisi kwasababu kule huendi kukutana na mtu mdhaifu, ni timu zilizojiandaa ndio maana tunahitaji kuandaa timu mapema kwa ajili ya mashindano hayo,”alisema.
Simba baada ya kuingia hatua ya makundi Kocha wake Mkuu Sven Vanderbroeck aliachana na timu hiyo baada ya kupata dili la kuifundisha klabu ya AS FAR ya Morocco, kikosi kikiwa chini ya Matola kwa sasa.
Matola alisema katika kuelekea huko wachezaji pia, wanatakiwa wajitambue na kujipanga kwenda kupambana ili kukabiliana na yeyote kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.
Simba inatarajiwa kufungua dimba dhidi ya AS Vita katika mchezo wa kwanza utakaochezwa Februari 12, mwaka huu nchini DR Congo.
Baadaye watacheza nyumbani dhidi ya Al Ahly Februari 23, mwaka huu kisha Machi kucheza na Al-Merrikh ugenini na kumaliza mzungumko wa kwanza kabla ya baadaye kurudiana wa pili.
Mbali na Simba, timu nyingine inayowakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ni Namungo inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.