loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwanaidi Bilali: Albino anayeamini ulemavu si mwisho wa safari

Mwanaidi Bilali, mkazi wa kijiji cha Matandu, wilayani Kilwa ni kati ya watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi Albino. Pamoja na ulemavu alionao amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za walemavu wenzake pamoja na jamii kwa ujumla na mshiriki hodari wa shughuli za maendeleo kwa wilaya hiyo, Beda Msimbe anasimulia zaidi.

ULEMAVU si mwisho wa safari, ulemavu ni changamoto ambayo inakabiliwa vilivyo na mlemavu mwenyewe na katika hili jamii ikimsaidia ataibuka mshindi na kusonga mbele katika hali ya kawaida ya mwanadamu yoyote yule.

Kauli hiyo imetolewa na Mwanaidi Bilali mmoja wa wanaharakati mlemavu ambaye amekuwa akiwaongoza walemavu wengine na hata wasiokuwa walemavu katika safari ya kujikomboa kijamii, kiuchumi, kupinga ukatili na kuwa mwalimu bora kwa waliokata tamaa.

Katika mahojiano Mwanaidi anasema kwamba ujasiri mkubwa ameupata baada ya kupata mafunzo mara kadhaa na taasisi ya TCRS Kilwa ambao walikuwa wakijishughulisha na mafunzo ya kuwakomboa walemavu na wanawake na wanajamii wengine kutoka katika lindi la ukatili na pia kuwapa mwanzo mzuri wa kuonesha uwezo wao.

"Kuwa mlemavu hakumaanishi kwamba wewe ndio umefika ukomo. La hasha, walemavu wote katika nafasi yao wana fursa za kujifanyia shughuli za kiuchumi na wakafanikiwa na si lazima awe amesoma na kuajiriwa," anasema Mwanaidi ambaye anaongoza kikundi cha walemavu.

 

Kwake yeye kuwa mlemavu hakumaanishi kuishi kimaskini, anachopaswa kuzingatia aliye mlemavu anasema ni kujitambua na kuthubutu kutumia fursa zilizopo kujipatia kipato na kusonga mbele. 

Anasema pamoja na yeye kuwa mlemavu wa ngozi, lakini anafanyakazi za shamba, akiwa na eka tano za shamba la mpunga na amekuwa akiwaambia walemavu wenzake kwamba inawezekana kubadili maisha kwa kujitambua na kujithamini.

"Huwa naenda shamba asubuhi nikitoka huko najifanyika kazi zangu nyingine ikiwa pamoja na kwenda kwenye vikundi" anasema akimaanisha kwamba pamoja na kuwa na ulemavu wa ngozi, muda wa asubuhi anaweza kuutumia kufanya shughuli za shamba na amekuwa na mafanikio makubwa katika hilo.

Lazima niwashukuru TCRS wamekuwa msaada mkubwa kwetu walemavu hapa Kilwa kutokana na mafunzo mbalimbali wanayofanya na kisha kutupatia nyenzo ya kujisogeza.

Mwanaidi anasema kwa sasa yeye na wenzake wamefanya andiko la kupatiwa mashine ndogo lakini ya kisasa ya kubangua korosho baada ya kuona kwamba shughuli hiyo inalipa kwani itamfanya kila mlemavu kushiriki.

Anasema wameanza mbali katika kundi analoliongoza kwamba walianza na usukaji wa mikoba na kuuza baada ya kupatiwa mtaji na TCRS lakini biashara hiyo ilikuwa ngumu na baadaye walitumia fedha walizopata kununua mashine ya Sido ya kubangua korosho na sasa wanataka mashine ya kisasa ya kutumia umeme ili waweze kujisughulisha na kubangua korosho.

"biashara ya mikoba kwetu ilikuwa ngumu sana. Watu wa hapa hawajui maana ya kuwa na mikoba. Lakini tulihangaika na tukapata shilingi laki mbili ziziotufanya tuwe na uwezo wa kununua mashine Sido ya mkono ya kubangua korosho," anaeleza Mwanaidi ambaye alishawahi kugombea udiwani wa viti maalumu uchaguzi uliopita lakini kura hazikutosha.

Pamoja na safari kuwa ngumu na ndefu kikundi anachooongoza Mwanaidi kwa sasa kinajishughulisha na ujenzi wa ofisi na kwamba kwa kutumia nguvu zao na msaada kutoka TCRS Kilwa wamepanga kuwa na ofisi ambako watakuwa wanafanya shughuli zao kwa tija zaidi.

"TCRS wametupatia bati na saruji sisi tumetumia nguvu zetu, tunaamini tukiwa na ofisi tutakuwa na eneo litakalokuwa linatuipa m,heshima na uwezo wa kufanya mambo mengi," anasema Mwanaidi.

Anasema jamii inayojali watu wake huwezesha kuishi kwa furaha na kwamba TCRS wamekuwa mstari wa mbele kusaidia kuondoa unyanyapaa na kutojiamini, hali ambayo inakuwa na maana zaidi hasa walemavu wanapojitambua na kujithamini kama moja ya watu katika jamii wenye maana kubwa.

Mwanaidi anasema angefurahi kama serikali nayo ingepanua zaidi wigo wa kukopesha mitaji walemavu kwa maana kwamba si lazima wawe katika vikundi wale wanaojitambua wanaweza wakakopa wao wenyewe na kuendelea na safari ya haba na haba hadi kibaba kijae.

"Serikali imeweka vyema utaratibu katika halmashauri kwa kikundi kwa zile asilimia mbili za mapato ya ndani, lakini naona hii pekee haitoshi imwezesha mlemavu mmoja mmoja mwenye mawazo ya kusonga mbele  bila kuwa katika kikundi," anashauri Mwanaidi anayeamini wapo walemavu wangependa kujiendesha wenyewe.

Utaratibu wa asilimia mbili ya halmashauri unamtaka mwombaji awe katika kikundi.

Mmoja wa wakazi wa Matandu, Salama Kilambo anasema Mwanaidi pamoja na kuwa mlemavu amekuwa ngome kubwa kwa wanaopenda maendeleo kutokana na yeye kuwa chemchem ya matumaini kila watu wanapokata tamaa katika kikundi.

Anasema hajawahi kuona mwanamke mchakarikaji kama Mwanaidi ambaye anasema alifaa hata kuwa diwani wao kutokana na jinsi anavyowashirikisha wananchi katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

"Kwa jinsi alivyo chachu sijaelewa kwanini hakuteuliwa hata kwa udiwani viti maalumu, tunahitaji viongozi wa aina hii ambao wanatekeleza wanachoamini na kuwasaidia wenzao vivyo hivyo," anasema Salama.

Naye Saidi Malenga, Mwenyekiti wa Kijiji cha Matandu, anasema Mwanaidi ni mfano wa kuigwa na balozi mzuri hata katika mambo ambayo yanahusu usawa wa kijinsia na kupinga ukatili. 

"Mwanaidi yuko vizuri sana katika kuhimiza walemavu wenzake na watu wa kawaida kuondokana na unyanyapaa. Huyu ni mfanyakazi mzuri katika jamii anaibeba," anasema Malenga na kuongeza kuwa Mwanaidi alishafikisha kwake taarifa tatu za ukatili wa kijinsia na zilifanyiwa kazi.

Nao Rosemary Matikisasu, Mkoyola Mkoyola na Sada Hassan wote wakazi wa Matandu, wanasema kwa nyakati tofauti kwamba harakati za Mwanaidi, ni harakati za kuokoa kizai cha sasa kukiaminisha uwezo wao na kukifanya kutumia fursa zilizopo kusonga mbele kimaendeleo.

Wanasema kama si Mwanaidi, walemavu wengi eneo hilo wangekuwa bado wanafanya shughuli za ombaomba. Yeye amesaidia kuamsha morali ya kujitegemea kwa kazi na hivyo wanapambana na hali zao na hawajishughuli na kuombaomba.

 

Waliungana na Mwanaidi kutaka serikali iangalie uwezekano wa kumpatia mtaji mlemavu mmoja moja badala ya kikundi.

Alipoulizwa akikutana na Rais John magufuli atamwambia nini? Mwanaidi alisema pamoja na kumshukuru atamwambia walemavu wapewe nafasi ya kuongoza kutoka ngazi za chini kwani kuongoza kwa ngazi za chini si lazima kuwa na elimu kubwa bali uwezo wa mtu kubadili maisha ya wale wanaomzunguka.

Anataka kuona kiongozi anawashirikisha watu wake katika maamuzi na kwa kushirikisha watu wake atajua shida ya kweli inayogusa kundi hilo na hivyo kutengeneza mikakati ya kusaidia.

GAUDENCIA (31) na Modesta (27) ni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi