loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali ilivyorejesha matumaini mapya wanufaika mradi wa maji Matwiga

WAHENGA hawakukosea walivyosema mvumilivu hula mbivu.

Kwa wakazi wa Kata ya Matwiga na maeneo ya jirani wilayani Chunya, mkoani Mbeya, msemo huu umetimia kwao baada ya muda mrefu wa kusubiri kupata maji safi na salama ya bomba.

Ngoja yao imewapa mateso ya muda mrefu ya kutembea umbali mrefu kufuata maji, wakapitia kipindi kirefu cha mkato wa tamaa na sasa kwa waliovumilia wanashuhudia kasi ya Serikali kwenye utekelezaji wa mradi wa maji wa Matwiga.

Mwishoni mwa mwaka jana wakazi hawa wamepelekewa matumaini mapya na kuona sasa Serikali inawajali baada ya kufufuliwa kwa ujenzi wa mradi wa maji wa Matwiga unaotarajiwa kunufaisha vijiji 16. 

Zilisikika nderemo na vifijo baada ya Naibu Waziri wa Maji, Marypriscar Mahundi kuwasili katika kijiji cha Matwiga na kupokelewa na wakazi wa kijiji hicho ziara iliyoashiria mwisho wa mateso yao umekaribia.

Moja ya mambo yaliofanyika ni ujenzi wa tangi kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 500,000, kuchimbwa kwa mtaro kwa ajili ya kutandaza mabomba na kufikishwa kwa vifaa mbalimbali ikiwemo mabomba makubwa na madogo kwa ajili ya kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tangi.

Pia uwepo wa mabomba ya maji kutoka kwenye tangi hadi kwa watumiaji kulionekana kuwapa moyo zaidi wananchi kwamba mradi huo ambao sasa ni miaka nane imepita tangu ulipoanza kutekelezwa, utakamilika.

Naibu Waziri Mahundi alidhihirisha dhamira ya Serikali kuwapatioa maji wananchi hao baada ya kwuahakikishia kuwa ifikapo Machi mwaka huu, vijiji vinane vya awali vitaanza kupata maji safi na salama.

Mahundi aliongeza kuwa tayari Serikali chini ya Rais John Magufuli imetoa fedha kiasi cha Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya kuendeleza mradi huo ili vijiji vya awali vianze kupata maji safi na salama ya bomba.

 

 

 

“Yawezekana walikuwepo walioukwamisha mradi huu kwa miaka ya nyuma wakawafanya muendelee kuteseka kwa kukosa maji. Wengi tunajua watu hao hawapo tena kwenye nafasi zao na sasa tupo watendaji tunaolenga kuwahudumia wananchi kwa kasi,” alisema Mahundi na kusisitiza kuwa fedha za awali zimeshatolewa. 

“Tumelenga kweli kumtua mama ndoo kichwani na itakuwa hivyo hapa Matwiga na vijiji vingine. Machi mwakani mtachota maji bombani tena maji safi na salama katika vijiji nane.

“Tutakwenda kwa awamu mpaka vijiji vyote 16 vilivyolengwa vifikiwe. Juhudi sasa mnaziona zilivyotofauti na huko nyuma. Nawahakikishia tutafanya,” alisisitiza Naibu Waziri Mahundi.

Hata hivyo ili mradi huo uwanufaishe, Mahundi anawataka wananchi wa vijiji hivyo kuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira na miundombinu ya mradi husika ili uwe na manufaa endelevu na kuwataka wawe walinzi wa kwanza.

Anasema Serikali kwa upande wake inatekeleza wajibu wake wa kuhakikisha mradi unakamilika na wananchi kupata maji pasipokutembea umbali mrefu.

“Serikali inatimiza kwa upande wake lakini na ninyi suala la ulinzi na usalama wa miundombinu hii kwenye vikao na mikutano yenu ya vijiji lizungumzwe mara kwa mara.” alisisitiza alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Matwiga yalipohifadhiwa mabomba kwa ajili ya kutandaza mtandao wa maji ya mradi huo.

Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka anatumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo akisema kwa sasa inaonekana kuongezeka zaidi ya miaka ya nyuma hatua ambayo imeongeza ari kwa wakazi wa vijiji vinavyotarajia kunufaika nao.

Kasaka anasema ilifika wakati wananchi walianza kukata tamaa baada ya kuona ahadi za kutekelezwa kwa mradi huo haziendani na kasi ya kiutendaji hatua iliyowafanya wahisi ni sehemu ya viongozi na watendaji kujinufaisha badala ya kujali utatuzi wa changamoto inayowakabili.

 

 

 

“Kwa sasa unaweza kuona hata wananchi wenyewe unapowa ahidi Machi maji yatawafikia, wanakuamini..Hii ni kwa kuwa wanaona kasi ya utekelezaji imeongezeka tofauti na awali. Wanaona kazi zinazofanyika, wanaona vifaa vilivyofikishwa..wanaoona namna Serikali sasa ilivyoguswa na tatizo la maji linalowatesa,” anasema Kasaka.

Clement Kivegalo ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa). Anasema kinachotakiwa hivi sasa katika miradi ya maji ikiwemo uliopo Matwiga ni kuhakikisha wananchi japo katika vijiji vichache wanaanza kunufaika wakati mipango mingine ikiendelea kufanyika badala ya kujiwekea mikakati ya kutimiza malengo kwa miaka mingi huku wananchi wote wakiendelea kuteseka.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, Septemba 2018 aliingia kwenye orodha ya wakuu wa mikoa waliowahi kutembelea mradi huo. Akiwa hapo hakusita kuitupia lawama Wizara ya Maji kwa watendaji wake kuwa na usimamizi mbovu kwenye mradi huo.

Chalamila katika ziara hiyo alitangaza na kuzitanga halmashauri zote za wilaya mkoani humo kuacha kupokea miradi ambayo haijakamilika na ambayo mikataba yake haieleweki ili kuepuka kujiingiza kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima.

Alitoa agizo hilo baada ya kukagua bwawa lililokuwa limejengwa kwa ajili ya mradi wa maji wa Matwiga mradi ambao ulitarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 50,252 sawa na kaya 8,827 zilizo katika vijiji 16 vya kata sita lakini ulishindikana kukamilika tangu mwaka 2004 ulipoanza kutekelezwa.

Katika ziara hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja alisema wananchi wamechoka kusubiri maji kutokana na kuwa na shida ya maji ya muda mrefu na kwamba mradi huo unasimamiwa na Wizara ya Maji moja kwa moja hivyo ni muda muafaka kwa waziri mwenye dhamana kupewa taarifa ili achukue hatua.

Mtunguja alisema katika mwaka huo wa fedha Wizara ilikuwa imetenga Sh milioni 500 kwa ajili ya kusambaza maji kutoka katika bwawa hilo kwa vijiji vitatu ambapo alishauri Waziri kutuma watalaamu kuja kuangalia namna ya kufanikisha zoezi hilo ili lisije likakwama kama ilivyokuwa mpaka siku hiyo.

 

 

 

Kufuatia maelezo hayo, Chalamila alimwagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Chunya kufika ofisini kwake ili kutengeneza taarifa ambayo itapelekwa wizarani kwa ajili ya kuleta wataalamu wa wizara kusimamia na kukamilisha mradi ndipo upokelewe.

Chalamila pia alifuatilia mradi huo Oktoba 2018 alipofika eneo hilo na kushangaa hakukua na hatua zozote zilizochukuliwa na Wizara ya Maji huku akisema kuwa miradi hiyo yenye dosari yote imefanywa na kampuni za jijini Dar es salaam jambo linaloonesha kuwepo kwa ushirikiano kati yao na baadhi ya maofisa wa wizara na huenda ndiyo sababu wanaogopa kuwachukulia hatua.

Kauli hizo za Chalamila zinatajwa huenda zilichochea mradi huo na mingine mkoani humo kuangaliwa upya kwani Machi mwaka juzi 2019 aliyekuwa Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa alimwagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Chunya, Samwel Hechei kujiridhisha haraka juu ya mkandarasi anayetaka kumpa zabuni ya Usanifu wa mradi wa kusambaza mtandao wa maji kutoka bwawa la Matwiga haraka ili wakazi wa kata hiyo wilayani Chunya waanze kunufaika. Waziri huyo alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua Bwawa hilo.

Wakati huo Mahundi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya na alimwambia waziri huyo kuwa wananchi wamechoshwa na ujio wa viongozi kila siku kutembelea bwawa hilo na kutoa ahadi zisizotekelezwa na akamuomba Mbarawa kuwatendea haki wakazi wa kata hizo wanaoendele kupata shida.

"Tuna imani kwa ujio wako huu wa leo wananchi hawa watapata majibu kwa  uhakika tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Wanachotaka wananchi hawa ni maji na si maneno yetu sisi viongozi. Viongozi wengi wamekuja hapa lakini matunda ya ujio wao hayakuonekana hapa,"alisema Mahundi akiwa Mkuu wa Wilaya hiyo.

Sasa kasi ya Serikali kupitia Mahundia anyeujua vizuri mradi huo, inarejesha matumaini kwa wakazi wa wilaya hiyo hasa wanufaika wa vijiji hivyo 16 kuwa watapata maji safi na salama muda si mrefu.

GAUDENCIA (31) na Modesta (27) ni ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi