loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tarura waokoa bil 1.8/- ujenzi wa daraja

WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) umeokoa zaidi ya Sh bilioni 1.8 kati ya Sh bilioni mbili ambazo zingetumika kwa ujenzi ambao tayari umekamilika wa Daraja la Mto Nkonjigwe wilayani Manyoni mkoani hapa.

Kabla ya Tarura kufanya kuamua kutumia mfumo wa ‘force account’ na kuanza kwa ujenzi huo kati ya Juni na Septemba mwaka jana, upembuzi yakinifu wa mradi huo kupitia wazabuni mbalimbali ulikadiriwa kufikia zaidi ya Sh bilioni mbili.

Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kunafungua fursa za uhakika wa upatikanaji wa huduma za afya hususani kwa wajawazito sambamba na kuimarisha wigo wa kibiashara kwa wakazi wa kata tano zinazotumia njia inayounganishwa na daraja hilo yenye urefu wa kilometa 76.2.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wanaozunguka eneo hilo, walisema wamefurahishwa kwa ujenzi wa daraja hilo litakalowasaidia wananchi hususan wajawazito kuvuka na kwenda kujifungulia katika zahanati za Kilimatinde na Chikuyu.

Awali, wanachi kadhaa walikatisha maisha yao kwa kushindwa kuvuka mto huo.

Halima Abdallah mkazi wa Kijiji cha Chikuyu alisema walikuwa wanatoa Sh 2,000 hadi 3,000 kuvushwa kwenye mto huo na watu wenye uzoefu wa kuogelea.

“Jambo hili halikuwa salama kwetu kwani kuna wakati licha ya uzoefu wao, walikuwa wanashindwa kuvuka na kupelekwa na maji pamoja na aliyekuwa anavushwa,” alisema Halima.

"Tulikuwa tukifika hapa tunavua nguo halafu ndipo tunavushwa, tunatoa Sh 2,000 za mtu kuvushwa na Sh 3,000 za nguo. Watu wamekufa wengi sana hapa hasa wanawake wajawazito," alisema Halima.

Thomas Minaloganawenda mkazi wa Kijiji cha Chinyika kilichopo Kata ya Sasajila, alisema moja ya shughuli kubwa ya kiuchumi katika maeneo hayo ni uchimbaji wa chumvi, lakini kuna wakati ilikuwa ikiharibikia kwenye mto kutokana na kukosa daraja.

Alisema amefanya kazi ya kuwavusha watu kwenye mto huo kwa muda mrefu licha ya kujipatia ujira, lakini alikuwa anaumia kuona watu wakipoteza maisha.

Mratibu wa Tarura Mkoa wa Singida, Boniphace William, alisema ujenzi wa daraja hilo umegharimu Sh 122,415,500 hadi kukamilika kwake kwa kutumia mfumo wa 'force account'.

Alisema daraja hilo linatoa fursa ya upatikanaji wa huduma mbalimbali kuzunguka vijiji vya Chikuyu, Chibumagwa, Sasajila, Majiri na Sanza.

Meneja wa Tarura katika Wilaya ya Manyoni, Yose Mushi, alisema daraja hilo lenye urefu wa mita 53 na mita 25 eneo la kupitisha maji, kadhalika lenye tuta mita 28 linatarajia kuchagiza kasi ya ustawi wa uchumi kwa wakazi wanaozunguka maeneo hayo.

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo katika Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Singida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi