loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru Pwani yaokoa milioni 58.1/-

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Pwani imefanikiwa kuokoa Sh milioni 58.1 kutokana na malipo mbalimbali yaliyofanywa kinyume cha taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha juzi, Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Pwani, Sadiki Nombo alisema fedha hizo zimeokolewa baada ya kupewa watu wasiostahili au watu kujipatia fedha kinyume cha utaratibu na kutakiwa kurudisha fedha hizo huku hatua zaidi za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi yao.

"Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh milioni mbili ambazo zimefanikiwa kurejeshwa ni za Chama cha Ushirika cha Ichunguro cha wilaya ya Mkuranga ambapo bodi ya chama hicho iliwadhulumu wakulima baada ya kuuza korosho zao zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye ghala la chama hicho," alisema.

Alisema pia walifanikiwa kurejesha Sh milioni 18 ambazo wakulima korosho wa Chama cha Ushirika cha Kimazinchana Kusini walidhulumiwa na bodi ya chama hicho.

"Tulifanikiwa kurejesha Sh milioni moja ambazo ni mali ya wakulima wa Chama cha Ushirika cha Shungubweni ambapo jumla ya kiasi kilichookolewa ni Sh milioni 21.1,” alisema.

Nombo alisema katika wilaya ya Kibiti, Takukuru ilifanikiwa kurejesha zaidi ya Sh milioni 18, ambapo Sh milioni 8.7 ni za mkopo zilizotolewa kwenye vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kutokana na asilimia 10 ya mapato yake ambapo vikundi hivyo vilishindwa kurejesha.

"Katika kipindi hicho tulifanikiwa kurejesha Sh milioni 8.1 baada ya viongozi wa vyama mbalimbali vya ushirika wilaya hiyo kuzirejesha na kugawiwa kwa wakulima waliokuwa wakidai," alisema.

Alisema pia walirejesha Sh milioni moja ambazo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Msafiri alizitumia kinyume cha utaratibu. Alisema fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya madarasa na nyumba ya walimu lakini alizitumia kwa manufaa yake binafsi.

"Fedha nyingine Sh milioni 1.4 ambazo zilifanikiwa kurejeshwa ni za kijiji cha Marui Gwata ambazo zilichangwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji ambapo fedha hizo zilifujwa na mwenyekiti wa kijiji ambaye baada ya kuzikusanya hakuzipeleka sehemu husika," alisema.

“Pia tulifanikiwa kurejesha zaidi ya Sh milioni mbili zikiwa ni malipo ya nauli kwa walimu wa shule za msingi zilizofanyiwa ubadhirifu na watumishi wa idara ya uhasibu Halmashauri ya Kisarawe na Sh 626,000 zilirejeshwa zikiwa ni za ujenzi wa Shule ya Sekondari Kimani ambapo mwalimu mkuu wa shule hiyo alizifanyia ubadhirifu.”

"Tulifanikiwa kurejesha fedha Sh milioni moja ambazo ni ukiukwaji wa taratibu za utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo mkopo ulitolewa kwa kikundi cha Chalinze Jimbo Saccos bila kufuata taratibu na Sh 210,000 ambazo zinatokana na makusanyo ya ushuru wa machimbo ya mawe kata ya Msoga," alisema.

Nombo alisema Takukuru mkoani humo pia imefanikiwa kurudisha Sh milioni 9.5 za manunuzi ya dawa kwenye Kituo cha Afya Mlandizi wilaya ya Kibaha ambazo zilinunuliwa bila ya kufuata taratibu kutoka kwenye kampuni ya Astra Pharma Tz Ltd ambapo mhusika ambaye ni katibu wa kituo hicho alichukuliwa hatua za kinidhamu.

Alisema pia walifanikiwa kuokoa Sh milioni 1.2 za posho zilizolipwa kinyume cha taratibu kwa watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ambapo watumishi hao walitakiwa kuzirejesha fedha hizo ambazo hawakustahili kulipwa.

"Sh milioni 3.9 zilirejeshwa wilaya ya Rufiji ambapo wafanyabiashara wa miti aina ya mikuruti ambao walipigwa faini Sh milioni tatu kutokana na kutofuata taratibu za uvunaji, pia tulifanikiwa kurejesha Sh  600,000 za faini kutoka kwa wafugaji baada ya mifugo yao kuingia kwenye mashamba ya wakulima kijiji cha Muhoro," alisema.

Alisema pia walifanikiwa kurejesha Sh 350,000 kwa mkulima ambaye alidhulumiwa mauzo yake ya korosho na fedha zake kuingizwa kwenye akaunti ya mtu mwingine.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein ...

foto
Mwandishi: John Gagarini, Kibaha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi