loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shamba la miti TFS Biharamulo kichocheo cha utalii Kanda ya Ziwa

SHAMBA la miti Biharamulo ni miongoni mwa mashamba ya Serikali yaliyoanzishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika mwaka wa fedha 2017/18.

Ukubwa wa shamba hilo ambalo limeanzishwa kwenye eneo lililokuwa msitu wa hifadhi Biharamulo-Kahama, ni hekta 69,756. Hifadhi yenyewe ya Biharamulo-Kahama ina ukubwa wa hekta 134,680 na urefu wa mpaka wa kilometa 254.

Hivi karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alitangaza Chato kuwa Kitovu cha uhifadhi na utalii katika Kanda ya Ziwa hivyo amemwelekeza Kamishna wa Uhifadhi TFS Profesa Dos Santos Silayo kufikiria kujenga hoteli nzuri na kutenga eneo la camping ili kuinua utalii eneo hilo.

Akitoa maelekezo hayo, Waziri Ndumbaro anasema kazi ya wizara hiyo ni kufufua utalii kwa mujibu wa ilani ya CCM kama Watanzania walivyowatuma.

“Tunakuza utalii kona zote za Tanzania kuanzia Kanda ya Kaskazini, Kusini, Magharibi na Mashariki tunataka baada ya miaka mitano tuwaambie Watanzania tuliahidi hivi na tumetekeleza hivi.

“Kila maeneo ya nchi yatakuwa na maeneo yake yakukuza utalii wa nje na wa ndani,” anasema na kuongeza kuwa hivi sasa wanakwenda kwenye maeneo ambayo hayafanyi vizuri ili waweze kuyainua.

Dk Ndumbaro anasema eneo la Chato kuna utalii wa maji, fukwe na wa nchi kavu lengo lao ni sekta hiyo iweze kuchangia uchumi wa nchi zaidi ya ilivyo sasa. 

Kwa sasa utalii huchangia asilimia 17.5 katika Pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni. Watalii wanaofika nchini kwa takwimu za mwaka 2019 kabla ya janga la Covid-19 walikuwa zaidi ya milioni 1.5 lakini lengo ni kufikia watalii zaidi ya 5,000,000 ifikapo 2025.

Anashauri katika kufanikisha jambo hilo, TFS iweze kuwashirikisha wanawake, wazee pamoja na vijana katika nyanja tofauti tofauti ili kutoa ushirikiano unaohitajika ikiwa ni pamoja na kuulinda msitu huo.

Ili kufanikisha hayo anawataka wafanyakazi kuacha uzembe kwani hatomvumilia ambaye atazembea ikiwa ni pamoja na kuendekeza vitendo vya rushwa. Pia aliwataka wananchi kutovamia maeneo ya hifadhi kwani kwa kufanya hivyo watalia na hakuna wa kuwabembeleza.

“Hatufanyi hivyo kwa kuonea, ila maeneo ya uhifadhi na utalii, kiuchumi ni eneo muhimu sana, hatuwezi kukubali livamiwe na watu wachache, ilani imetutaka tufike dola bilioni sita hatuwezi kufika huko kama watu wanaharibu mazingira,” anasema.

“Tunataka kukuza utalii, tunajua Kanda ya Kaskazini imeshakuwa kimataifa ukiongelea Serengeti, Ngorongoro, Tarangire na Manyara watu wanazijua.

“Tunataka maeneo mengine ya utalii ya Kanda ya Ziwa, Magharibi, Kusini nazo tuzitangaze na katika kila kanda tutatafuta wapi kitovu,” anasema.

Waziri huyo anasema kama wizara wanataka kuleta muunganiko wa utalii kutoka Serengeti mpaka Chato kwa kuisaidia Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kupeleka watalii katika uwanja wa Chato.

Anawataka Watanzania wanaotaka kuwekeza utalii wa maji wajitokeze kwa kuwa ni fursa katika eneo hilo hivi sasa. “Wawekezaji kwenye sekta ya utalii waje kuwasiliana na wizara wa ajili ya kuwekeza,” anasema.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo la Biharamulo, Thadeus Shirima, anasema mwaka 2017, Menejimenti ya TFS Kanda ya Ziwa ilipendekeza kwa Mtendaji Mkuu juu ya uanzishwaji wa Shamba la miti katika Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama kwa upande wa Wilaya ya Chato, mkoani Geita.

Shirima anasema uanzishwaji wa shamba hilo ulilenga maeneo yaliyoharibiwa na yaliyokuwa yamevamiwa kwa kuanzishwa shughuli mbalimbali za kibinadamu hivyo ili kunusuru hilo serikali ikapanga kupanda miti ya biashara pamoja na kuimarisha usimamizi wa maeneo yote ambayo ni lindi maji (Cathments) yaliyopo ndani na nje ya maeneo ya hifadhi hiyo.

“Hii ilikuwa moja ya mikakati ya kuendeleza na kuanzisha mashamba ya miti ili kuongeza mapato ya Serikali na kutoa ajira na kuongeza mapato kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hii.

“Pia kutoa elimu kwa jamii zinazozunguka msitu huu juu ya uhifadhi na kutoa hamasa juu ya kilimo bora cha miti kwa kuzingatia matumizi ya mbegu bora,” anasema.

 

 

 

Anasema mashamba ya miti ni miongoni mwa misitu ya hifadhi za Serikali Kuu zinazosimamiwa na TFS ambayo yapo 23 nchini lengo la uanzishwaji wake ni kukidhi mahitaji ya mazao ya misitu.

“TFS ina jukumu la kuendelea kuongeza mashamba mengine kwa ajili ya kuzalisha mazao mengi ya misitu. Katika mwaka 2017/2018 Wakala uliongeza mashamba mapya manne ambayo ni Biharamulo (Chato, Geita), Iyondo Mswima (Ileje, Songwe), Buhigwe (Kigoma) na Mpepo (Mbinga, Ruvuma),” anasema.

Kwa maelezo ya Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo Shirima, lengo la uanzishwaji wake ni kuotesha na kukuza miti ya mbao laini na ngumu kwa ajili ya kutoa malighafi kwa viwanda vya misitu katika hali endelevu.

Pia kuhifadhi mazingira vyanzo vya maji, udongo na bioanuai zilizopotea, kulipatia taifa mapato kutokana na mauzo ya mazao ya misitu na huduma mbalimbali pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.

Kwa kipindi cha miaka minne kutoka mwaka 2017/18 hadi 2020/21 jumla ya miche 7,449,255 imepandwa kwenye hekta 2,682 sawa na eka 6,705.                    

“Uanzishwaji na uendelezaji wa shamba hili unaenda sambamba na malengo ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani malighafi itakayopatikana katika shamba hili baada ya miti kufikia umri wa kuvunwa itatumika katika viwanda vya kuzalisha karatasi, viwanda vya kuzalisha nguzo za umeme na vinginevyo.

“Hii ni katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 46 (a) katika kulipatia ufumbuzi tatizo la ajira nchini ambapo kipaumbele chake ni kukuza na kuanzisha viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa vyenye uwezo wa kuajiri watu wengi na uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazotumiwa ndani ya nchi na ziada kuuzwa nchi za nje,” anasema.

Kwa upande wake Kamishna Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo anasema shamba hilo la miti Biharamulo linategemea kuwa la pili kwa ukubwa likizalisha miti kwa ajili ya biashara mbalimbali na uhifadhi.

Anasema maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Ndumbaro ikiwamo ujenzi wa hoteli katika shamba hilo ili kuvutia watalii zaidi, wanayapokea na kuyafanyia kazi kwani wanataka waende na kasi kubwa.

 

“Tutaongeza kasi katika uhifadhi mfano eneo la ufugaji nyuki tutaanza utekelezaji huo ikiwa ni pamoja na kushirikisha wananchi katika kupambana na matukio ya moto na kuwashirikisha katika upandaji ili kuhakikisha malighafi yanakuwepo,” anasema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Aloyce Nzuki anasema shamba hilo la Biharamulo litakuwa na mchanganyiko wa msitu wa asili na eneo jipya lililotangazwa mwaka 2010 la upandaji miti. Faida yake katika shamba hilo ni kufanya shughuli za utalii na ufugaji nyuki.

I NAELEZWA kwamba matumizi ya dawa za kulevya ni moja ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi