loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EU yaiahidi Tanzania wawekezaji zaidi

UMOJA wa Ulaya (EU) umeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchi wanachama kuwekeza nchini.

Hayo yalisemwa jana jijini Dodoma na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Manfred Fanti, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

“Nimekuwa nikisikia ushuhuda kutoka kwa wawekezaji wengi wanaotoka nchi za Umoja wa Ulaya kuwa wanapata faida katika uwekezaji wao hapa nchini na nikiwa kama mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania ni jukumu langu kuhakikisha kuwa nashirikiana ipasavyo na Serikali ya Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza Tanzania”, alisema Balozi Fanti.

Alisema umoja huo unatambua jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli katika kuboresha mifumo ya kisheria, kisera na ya kitaasisi ili kuweka mazingira rafiki zaidi yatakayovutia wawekezaji na hivyo wako tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali ili kufanikisha lengo hilo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkumbo na Balozi Fanti walijadili pia maeneo bayana ambayo Tanzania na EU wanaweza kukuza ushirikiano wa uwekezaji ikiwemo katika sekta ya uzalishaji nguo, uchimbaji na uchakataji wa madini, uchakataji wa mazao ya mifugo na uvuvi, uzalishaji wa nishati.

Profesa Mkumbo aligusia baadhi ya maeneo ya kimkakati ambayo tayari Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka nguvu kuyatekeleza ikiwemo kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji, utekelezaji wa programu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara pamoja na kuandaa mfumo kamambe wa ukusanyaji takwimu za uwekezaji nchini.

Alimweleza Balozi huyo kuwa hayo ni baadhi ya maeneo ambayo serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya, ili pamoja na mambo mengine, kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili wawekezaji wa kigeni hapa nchini.

Katika hatua nyingine, waziri huyo wa uwekezaji alikutana pia na Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Lianne Houben ambao katika mazungumzo, walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hususani wanaotoka nchi yake.

Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kuwezesha taasisi mbalimbali wezeshi zinazohudumia wawekezaji kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi huku zikizingatia maslahi mapana ya wawekezaji.

Eneo lingine ni suala la uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na fani mbalimbali ambazo wawekezaji wanazihitaji. Uholanzi ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na wawekezaji wengi nchini waliowekeza katika sekta za mbalimbali kama vile kilimo; mfano kampuni za maua zilizowekeza mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Sekta nyingine ni huduma za kifedha mfano Benki ya NMB, viwanda kama ilivyo kwa kampuni Unilever na Heineken; usafirishaji kwa mfano Kampuni ya KLM. Takwimu zinaonesha kuwa takribani miradi 161 ya kutoka Uholanzi imesajiliwa katika za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na mitaji yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani biilioni 1.1 na kutoa ajira 13,995.

SERIKALI imeiruhusu sekta binafsi kuingiza nchini matrekta madogo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi