loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

La Majaliwa na binti mwenye ulemavu ni funzo kwa Watanzania

JUZI Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu na Rais John Magufuli walifanya tukio tunaloamini ni funzo kubwa kwa Watanzania kuhusu umuhimu na nafasi ya watu wenye ulemavu nchini.

Katika tukio hilo lililofanyika Mombo wilayani Korogwe katika Mkoa wa Tanga, Waziri Mkuu Majaliwa, alimkabidhi rasmi nyumba ambayo tangu kujengwa kwake hadi kukamilika ikiwa na samani za ndani, imegharimu Sh milioni 47, kwa binti mwenye ulemavu anayeishi na bibi yake, Miriam Msagati, katika Kitongoji cha Fune kilichopo Kata ya Mombo.

Kimsingi, nyumba aliyokabidhiwa Binti Miriam mwenye ulemavu wa mikono na miguu, imejengwa na wadau mbalimbali kutokana na mchango ulioasisiwa na Waziri Mkuu Majaliwa.

Mchango huu ulianza Machi 5, 2020 Majaliwa alipomtembelea Miriam na kumpa wa Sh milioni tano za kuanza ujenzi wa nyumba hiyo na kuomba wadau wengine mkoani humo wasaidie katika jukumu hilo.

Juzi katika hafla ya kukabidhi nyumba hiyo na hati yake, Majaliwa alifanya harambe fupi uliyowagusa Makamu wa Rais, Mama Samia sambamba na Mkuu wa Nchi, Rais John Magufuli ambao hawakuwapo katika tukio hilo mkoani Tanga.

Licha ya kutokuwapo katika tukio hilo, Samia alipiga simu akipongeza kazi hiyo aliyoiasisi Waziri Mkuu na kutangaza kumchangia binti huyo Sh milioni tano ili zimsaidie kuendesha ujasiriamali kwa ajili ya maisha.

Rais Magufuli naye alituma taarifa kuwa naye anamchangia binti huyo Sh milioni kumi ili zimsaidie kwa kazi hiyo kama mtaji wa biashara.

Kimsingi mbali na nyumba hiyo, zilipatikana Sh milioni 18.9 hali inayotufanya kwa pamoja tuseme kuwa, kwa tukio hilo Watanzania tunalo somo la kujifunza kuhusu watu wenye ulemavu. Ikumbukwe Majaliwa alimsaidia binti huyo baada ya kumsikia akimuomba amsaide kupata makazi na bibi yake, kupitia kipindi cha ‘Wape Nafasi’ kinachoongozwa na Tuma Dandi, Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) ambaye pia ana ulemavu wa miguu.

Kwa niaba ya kipindi cha Wape Nafasi, Dandi alichangia Sh 100,000 huku Waziri Mkuu akichangia Sh 500,000 na wadau wengine kuchangia kadiri walivyoweza.

Baada ya kuonana na Miriam mwaka jana, Majaliwa alitoa Sh milioni tano papo hapo na kumkabidhi Mwenyekiti wa Kijiji ili zitumike pamoja na mambo mengine, kutafuta kiwanja kwa ajili ya kumjengea nyumba nzuri itakayokidhi mahitaji yake.

Nyumba hiyo ina vyumba viwili vya kulala, jiko, vyoo vya ndani, maji, umeme, televisheni na fremu ya duka kwa ajili ya biashara/ ujasiriamali katika eneo lake.

Ndiyo maana tunasema, tukio hili ni ishara kuwa yapo mengi ya kujifunza ukiwamo ukweli kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano, ni serikali inayosikiliza sauti za wanyonge na kuzipatia majawabu.

Ndiyo maana tunasema, Watanzania tujifunze kupitia alichoasisi Waziri Mkuu Majaliwa, walichofanya Mama Samia na Rais Magufuli kwa kuonesha upendo na kuwasaidia watu wenye ulamavu.

Ndiyo maana licha ya hali yake, Miriam alimshukuru Rais Magufuli, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, Uongozi wa Mkoa wa Tanga na wote wenye mapanzi mema kwa kujali wanyonge.

Miriamu alinukuliwa akisema: “Siwezi kusahau kitu kama hiki, Mwenyezi Mungu ameniona, Mwenyezi Mungu awabariki watu wote walioshiriki katika kufanikisha jambo hili kwani mmeweka hazina yenu kwa Mungu.”

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi