loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DC Butiama ataka ushirikiano kuongeza ufaulu wa wanafunzi

WENYEVITI wa vijiji na vitongoji pamoja na watendaji wa mitaa na kata kwa kushirikiana na wazazi na walezi wilayani Butiama katika Mkoa wa Mara, wametakiwa kusimamia na kufuatilia mienendo ya watoto shuleni ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubhi, alitoa mwito huo katika Kongamano la Elimu wilayani hapa na kusisitiza kuwa, wazazi ama walezi na viongozi wapo karibu na wanafunzi, hivyo wanayo nafasi kubwa kuwafanya watoto wafanye vizuri katika masomo yao.

Alitaka kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu ili kukuza maendeleo ya elimu wilayani Butiama sambamba na kufuatilia mienendo ya watoto kitaaluma na kitabia ili kuchagiza mafanikio ya watoto kielimu.

Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) kutoka Mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju, aliyekuwa mgeni mwalikwa alisema Simiyu wanafanya vizuri katika elimu kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wazazi, walimu, serikali na wanafunzi sambamba na kila mmoja kufanya kazi kwa bidii.

Alisema ubunifu katika utendaji na ushirikiano ni miongoni mwa mambo yanayosababisha Mkoa wa Simiyu kufanya vizuri katika taaluma na hata kuingia katika nafasi kumi bora kitaifa.

“Tulianzisha kambi za kitaaluma na vikao na wadau wa elimu pamoja na wazazi; tuna desturi ya kuwasomea taarifa za elimu ikiwemo utoaji wa motisha na zawadi kwa waliochangia elimu au kwa wanafunzi na walimu waliofanya vizuri ili kuwa karibu nao katika ukuaji elimu,” alisema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Deus Wambura, alisema ili ufaulu uongezeke wilayani Butiama, lazima walimu wapunguze adhabu kali kwa wanafunzi hasa katika madarasa ya mitihani akitolea mfano shule zilizopo Ukanda wa Kata ya Buswahili ambapo wanafunzi wengi wameacha shule kutokana na kukwepa adhabu za viboko.

Mbunge wa Jimbo la Butiama aliyekuwa Mwenyekiti wa kongamano hilo, Jumanne Sagini, aliwapongeza madiwani kwa juhudi zao kuhakikisha wanatilia mkazo elimu ikiwemo kuchangia vifaa vya ujenzi wa shule katika vijiji ili kuwapunguzia mwendo wanafunzi kufuata elimu katani.

Aliunga mkono mwitikio wa wadau wengi wa elimu waliotaka utumike mfumo wa mkakati sera wa kuinua ufaulu unaotumiwa na Mkoa wa Simiyu ambapo yeye pia alikuwa ni mmoja kati ya waandaji wa mfumo huo alipokuwa katibu tawala mkoani hapo.

PAPA Francis ameanza ziara yake ya ...

foto
Mwandishi: Yohana Shida, Butiama

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi