loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TRA Ruvuma wavuka lengo kwa asilimia 109

MAMLAKA ya Mapato (TRA) mkoani Ruvuma, imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 8.442 sawa na asilimia 109 kati ya lengo walilopewa la kukusanya Sh bilioni 7.771 katika kipindi cha miezi sita kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo mkoani humo, Amina Ndumbogani, wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2020/2021 kwa waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea.

Aidha alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021 TRA mkoani Ruvuma ulipewa lengo la kukusanya Sh bilioni 15.639, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi wa mamlaka hiyo hadi kufika Desemba 2020 wamefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya Sh bilioni 8.4 hivyo kuwa na matumaini ya kufika lengo la kukusanya Sh bilioni 15.6.

Alisema mbali na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi pia mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo kutoka kwa wadau wengine wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo Christina Mndeme na wakuu wa wilaya tano za mkoa wa Ruvuma pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ambayo ni sehemu ya mafanikio hayo.

Alisema wanajivunia kuona wadau mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, wakuu wa wilaya za mkoa huo na wafanyabiashara ndiyo waliofanikisha malengo ya Mamlaka hiyo kuvuka malengo katika kipindi cha nusu mwaka kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.

Aidha alisema, kwa mwaka huu wa fedha wameweka malengo mbalimbali kama mkakati wa kukusanya Sh bilioni 15 walizopewa ambayo ni kupanua wigo kwa kuwatambua na kuwasajili wafanya biashara kwa mfumo wa mtandao,kupita mlango kwa mlango ili kuwabaini walipa kodi na wale wanaokwepa kulipa kodi na kuongeza nguvu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine za Efds.

Alisema, mbali na hilo mkakati mwingine ni kuwafuatilia walipa kodi wenye madeni ili kulipa madeni yao kwa wakati kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

“Kazi ya kukusanya kodi ni ngumu sana,lakini kutokana na jitihada kubwa zilizofanyika na wadau wengine kwa kweli ndiyo kwa kiasi kikubwa waliofanikisha malengo hayo,”alisema Amina.

Alisema TRA inaendelea kuwakumbusha wafanyabiashara na wananchi wote kwa jumla kuwa msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni utunzaji sahihi wa kumbukumbu na ni wajibu na kila mwenye sifa kulipa kodi stahiki za serikali.

Alisema mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la kutotumia mashine za Efds adhabu yake ni faini kuanzia milioni tatu na isiyozidi milioni 4.5 au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa kodi ya mwaka 2015.

Pia, aliwataka wanunuzi wote wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanadai risiti pindi wafanyapo manunuzi kwani ni haki ya msingi na kisheria kwa kila mnunuzi, na kutofanya hivyo ni kosa linaloweza kupelekea kupata adhabu kali ikiwemo kutozwa faini kati ya shilingi 30,000 hadi milioni 1.5.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein ...

foto
Mwandishi: Muhidin Amri, Songea

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi