loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mikakati yawekwa nchi kujitosheleza mafuta

SERIKALI imeeleza mipango na hatua inazochukua kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa mafuta nchini yanayotosheleza mahitaji hatua itakayosaidia kushuka kwa bei yake.

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliliambia gazeti hili kwamba serikali imependekeza kuwekeza katika zao la alizeti ili kuzalisha mafuta ya kutosha.

Hatua ilizoanza kuchukua ni kuzalisha mbegu bora za alizeti ambazo zitawawezesha wakulima kupata mazao mengi ikizingatiwa kwamba, wakulima wengi hutumia mbegu wanazozalisha shambani bila kuangalia ubora.

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe, mahitaji ya mafuta nchini ni metriki tani 570,000 kwa mwaka. Kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000 huku asilimia 60 ikiingizwa kutoka nje ya nchi.

Bashe alisema Tanzania inahitaji tani 5,000 ya mbegu bora za alizeti. Alisema kwa sasa serikali pamoja na taasisi binafsi zinazalisha tani 1,200 za mbegu bora za alizeti.

Ili kuwawezesha wakulima kuzalisha alizeti ya kutosha, alisema Wizara ya Kilimo imeamua kuweka nguvu katika uzalishaji wa mbegu bora za OPV na Hybrid .

“Sisi kama Wizara tumewapa jukumu Wakala wa Kuzalisha Mbegu pamoja na TARI ndani ya mwaka mmoja kufanya kila wawezalo kuhakikisha tunafikia lengo la uzalishaji wa mbegu tani 5,000,” alisema Bashe.

Hatua nyingine inayofanywa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo ni kugawa mbegu na miche ya michikichi bure katika mikoa mbalimbali ili kuimarisha uzalishaji wa michikichi ya kutosha kwa lengo la kupata mafuta mengi ya mawese.

“Mikoa iliyolengwa ni pamoja na Kigoma, Tabora na Rukwa ambako tumegawa miche milioni 1.5 na mpaka sasa kuna miche mingine milioni moja ambayo iko mashambani chini ya taasisi yetu ya TARI ambazo tutazigawa kwa wakulima na lengo ni kila mwaka tuzalishe miche milioni moja ya michikichi,” aliongeza Bashe.

Bashe alisema hatua ya tatu ni uanzishwaji wa mashamba makubwa yenye ukubwa wa hekta kuanzia 2,000 hadi 5,000 kisha kuwagawia wakulima kuanzia ekari tano hadi 10 kila mmoja watakaokuwa wakilima alizeti hususani katika mikoa ya Simiyu, Singida, Shinyanga na Tabora.

Alisema Wizara itawasaidia wakulima hao kupata wataalamu, kuwapatia mbegu bora pamoja na kuwasaidia katika mahitaji ya vifaa ikiwa ni miongoni mwa hatua ambazo serikali imeanza kuchukua ili kukabiliana changamoto ya mafuta ya kupikia nchini.

Hivi karibuni Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema ili kuhakikisha mafuta ya kupikia yanapatikana kwa kiasi kinachotakiwa, serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Alisema serikali itahakikisha kuwa inaondoa vikwazo mbalimbali vinavyowakwamisha wawekezaji katika sekta ya mafuta pamoja na kuwapa nafasi wakulima wadogo waweze kuzalisha mazao ya kutosha.

Profesa Mkenda alisema serikali imeshaanza kupitia kanuni upya kubaini mahali panaposababisha mkwamo wa uzalishaji wa mafuta nchini. Kupitia kanuni na sheria hizo, serikali inalenga kukuza uzalishaji wa ndani zaidi.

Wakati huo huo Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amewahakikishia wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa mafuta ya kupikia katika sehemu mbalimbali nchini itatengamaa katika kipindi kifupi kijacho kutokana na hatua za kukabiliana na hali hiyo zilizokwisha chukuliwa.

Waziri Mwambe aliliambia gazeti hili kuwa uhakika huo unatokana na kuanza upakuaji wa mafuta ya kupikia yaliyoingizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es salaam.

Alisema meli mbili ya UACC SHMIYA imepakua mafuta ya kupikia yenye ujazo wa metriki tani 21,800 na nyingine, MELATI SATU ilikamilisha kupakua mafuta metriki tani 26,450 Januari 22, mwaka huu na yako mbioni kuingia sokoni.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, waziri Mwambe alisema serikali imezipatia leseni kampuni mbili za uagizaji wa mafuta hayo ambazo ni East Coast Oil and Fats Ltd pamoja na Murzah Wilmar East Africa Ltd.

Kampuni hizo zimekuwa zikiingiza mafuta ya kupikia nchini kukidhi upungufu wa metriki tani 365,000 kwa mwaka ya mahitaji halisi ambayo ni metriki tani 570,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Kilimo, Bashe, kupanda kwa bei ya mafuta ya kula kumetokana na kushuka uzalishaji wa mafuta hususani mafuta ya mawese duniani ambayo ndio yanayotumika.

Hali hiyo imesababisha bei ya mafuta duniani kupanda kutoka Dola za Marekani 600 kwa metriki tani moja Oktoba mwaka jana hadi kufikia Dola za Marekani takribani 1,000 kwa metriki tani moja mwezi huu.

“Ukiangalia takwimu hizo kuna ongezeko la bei karibia asilimia 60 duniani, kwa hiyo tatizo hili si la Tanzania peke yake bali ni la dunia nzima,” alisema Naibu Waziri Bashe.

Alisema sababu kubwa ya bei ya mafuta hayo kupanda duniani ni kuwa uzalishaji wa michikichi duniani umepungua kutokana na madhara yaliyosababishwa na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi Corona (Covid 19).

Nchi nyingi zinazozalisha michikichi ni pamoja na Malaysia ambazo kutokana na kufungiwa ndani kujikinga na corona, uzalishaji wa mashambani ulipungua kwa kiasi kikubwa.

SERIKALI imeiruhusu sekta binafsi kuingiza nchini matrekta madogo ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi