loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wananchi jengeni tabia ya kuandika wosia

MOJA ya migogoro mingi inayojitokeza katika familia nyingi hapa nchini inahusu mirathi na hiyo hutokea pale mmoja wa wanafamilia anapofariki na kusababisha ndugu waliobaki kutofautiana katika mgawanyo wa mali alizoacha.

Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), bado kuna muamko mdogo wa Watanzania kujitokeza katika ofisi hizo na hata sehemu nyingine za kisheria kuandikisha wosia, hali ambayo baadae husababisha mtafaruku mkubwa miongoni mwa wanafamilia hata kupelekea kufikishana mahakamani.

Mathalani, tangu kuanzishwa kwa huduma ya uandikishaji wa wosia katika ofisi za wakala huo, ni watu 780 pekee ndiyo waliofika kwa ajili ya kuandikisha na kuhifadhi wosia ambao wameuandaa ili kuondoa utata pale watakapo patwa na mauti.

Bado haijawekwa wazi nini kinachosababisha wananchi wengi kushindwa kujitokeza na kuweka kumbukumbu hizo muhimu za wosia, ila taarifa zisizo rasmi zinadai kuwa wengi wao wanaona kufanya hivyo ni sawa na ‘kujichulia’ kifo kitu ambacho siyo cha kweli na kinalenga kupotosha umma.

Ikumbukwe kuwa, moja ya matamanio ya kila mtu ni kuona familia yake inakuwa na maisha bora na kuishi kwa usawa wakati wote awapo duniani au hata pale inapotokea Mungu amemchukua; hakuna anayependa kuona familia yake ikija kupagaranyika na kuteseka dunia pindi atakapokuwa ‘ameondoka’ katika dunia hii.

Ipo migogoro mingi, mitafaruku na kesi katika mahakama mbalimbali inayohusu mgawanyo wa mirathi inayojitokeza pale mmoja wa wanafamilia hususani mzazi wa kiume anapokuwa amefariki na kupelekea ndugu kujitokeza na kugombea mali hata kama siyo wahusika wa karibu wa mali hizo.

Katika sula hilo, waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto, ambapo ndugu wa upande wa kiume hujitokeza na kutaka kupewa mali au sehemu ya mali hizo kana kwamba walihusika kwa namna moja au nyingine katika kuzichuma na hivyo kupelekea mke na watoto wa marehemu kubaki bila kitu.

Kwa mujibu wa Rita, zipo faida nyingi za mtu kuandika wosia hivyo kuwataka Watanzania kujitokeza na kujiandikisha kwa lengo la kuepusha migogoro mingi inayojitokeza kipindi mmoja wa wanafamilia hao anapokufa bila kujali kuwa anayeandika wosia huo ni mzazi wa kiume au wa kike.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la Rita wakati wa maonyesho ya wiki ya mahakama inayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Abubakary Kunenge alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kujitokeza na kuandika wosia jambo litakalosaidia kuondoa au kupunguza migogoro mingi inayohusu mirathi katika familia.

Anasema takwimu zinaonyesha bado sehemu kubwa ya wananchi inajificha na kushindwa kujitokeza kuandika wosia huo, jambo linalochangia kuendelea kujitokeza kwa migogoro hiyo ambayo mwisho wake ni chuki katika familia hizo na hata kuvunja undugu.

Alitoa msisitizo kwa wananchi kuunga mkono uamuzi wa taasisi hiyo kulipa kipaumbele suala la wosia kwa kuwa litasaidia kupunguza malalamiko na migogoro mingi katika familia pale kila kitu kitapokuwa kimewekwa wazi na mhusika wa wosia huo inapotokea amefariki.

Naye Mwanasheria wa Rita, Edna Kamara anasema ni vyema wananchi wakajijengea utaratibu wa kuandika wosia kwa kuwa ni njia pekee itakayoziepusha familia kuingia katika migogoro isiyo ya lazima ambayo wakati mwingine husababisha familia kuvunja undugu.

Anasema wao kama Rita wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo huduma ya uandikaji wa wosia ili kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika jamii na kuwataka wananchi wengi kujitokeza katika ofisi za Rita zilizopo mikoani kote kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi