loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera Iringa muongozo uwekezaji, wengine waige

MKOA wa Iringa umezindua mwongozo wa uwekezaji ambao unabainisha vivutio vilivyoko mkoani humo ikiwamo mazingira mazuri ya biashara, nguvu kazi, amani na utulivu, maliasili na soko la kutosha ili kurahisisha uwekezaji.

Mwongozo huo ulizinduliwa juzi na Waziri Mkuu, Kassim ambaye wakati akizungumza kwenye hafla hiyo alisema serikali itaendelea kudumisha amani na utulivu ambao ni muhimu kwa wawekezaji kutoka nje na wananchi kuwekeza.

Katika kutimiza azma hiyo, Waziri Mkuu amewaagiza watendaji wote wa serikali katika ngazi mbalimbali kushiriki kikamilifu kutangaza fursa za uwekezaji na pia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta wanazozisimamia ili kurahisisha mazingira ya biashara na uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Tukiwa wadau wakubwa wa maendeleo ya nchi yetu, tunaupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kuandaa mwongozo huo wa uwekezaji katika mkoa wao.

Ni dhahiri kuwa, mwongozo huo si tu utavutia uwekezaji mkubwa na mdogo mkoani humo, bali pia utakuwa dira, maono na muelekeo katika kujenga uchumi wa mkoa na utaweka msingi wa kuzalisha ajira za kutosha kwa wananchi hususani vijana.

Ikumbukwe uwekezaji ni tegemeo la taifa lolote lile ulimwenguni katika kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Kutokana na umuhimu huo serikali yetu chini ya Rais John Magufuli imekuwa ikiwekeza nguvu kubwa katika eneo hilo ili Tanzania iweze kunufaika na fursa zote za uwekezaji zilizopo nchini.

Mara kwa Mara Rais Magufuli amekuwa akisema Tanzania si masikini na kuwataka Watanzania kufumbua macho kuziona fursa nyingi za kukuza uchumi tulizo nazo, ili ziweze kutumika kuboresha maisha ya watu na nchi na kuzuia mianya yote ya kuporwa na kwenda kunufaisha wanachi wa mataifa mengine huku Watanzania wakiangalia tu.

Hivyo jitihada zozote za kufikia lengo la serikali la kuinua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zetu tulizonazo kama ilivyofanya mkoa wa Iringa zinapaswa kupongezwa na kuungwa mkono.

Rai yetu kwa mikoa mingine ni kuiga mfano wa mkoa wa Iringa kwa kuainisha miongozo ya uwekezaji ili fursa zote zilizopo katika maeneo hayo ziweze kujulikana vizuri na wawekezaji wa nje na wa ndani.

Nchi yetu imejaaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji zilizotapakaa katika kila kona ya nchi, kinachotakiwa ni utashi wa viongozi wa wadau wote kuzianzisha na kuzitangaza ili ziweze kujulikana na kutumika kwa manufaa ya wananchi na taifa.

Tunawasihi sana wadau wote wa maendeleo hususan viongozi wa serikali na kijamii kuziainisha na kuzitangaza kwa nguvu kubwa fursa zote zilizopo katika maeneo yao ili wawekezaji waweze kuzifahamu kwa kina na kwenda kuwekeza.

Aidha, tuhakikishe vikwazo vyote vya uwekezaji na biashara vilivyopo katika maeneo hayo vinaondolewa ili kutokwaza wawekezaji.

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi