loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi aipongeza JWTZ kuimarisha amani, kulinda mipaka

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kazi wanayofanya ya kuimarisha amani na kulinda mipaka ya nchi.

Aliyasema hayo jana alipokutana na kuzungumza na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo aliyefika Ikulu jijini Zanzibar kumpongeza. Rais Mwinyi alisema JWTZ limeendelea kufanya kazi kubwa ya kulinda amani nchini na kulipongeza pia kwa kuisimamia amani hiyo katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema Watanzania wanajivunia kazi inayofanywa na jeshi lao katika kuhakikisha wanakuwa salama wao pamoja na mali zao wakati wote na kumuhakikishia Jeneral Mabeyo kuwa Zanzibar iko salama.

“Tumeridhika kwa amani na utulivu uliopo na tunatoa shukurani kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania kwa kulinda mipaka yetu na kuendelea kusimamia amani na utulivu hapa nchini,” alisema.

Pia aliitaka JWTZ kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kushirikiana na vikosi vya ulinzi vya Zanzibar ikiwemo Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) katika uzalishaji mali hasa kilimo.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uzalishaji mali katika sekta ya kilimo Zanzibar ikizingatiwa kuwa JKT wana uzoefu mkubwa katika shughuli hizo.

Aidha, Dk Mwinyi alitoa pole kwa jeshi hilo kutokana na kifo cha Brigedia Jeneral mstaafu, Emmanuel Maganga kilichotokea katika Hospitali ya Mirambo Manispaa ya Tabora alipokuwa akipatiwa matibabu.

Brigedia Jenerali Maganga pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma. Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo alimpongeza Rais Mwinyi kwa kushinda nafasi ya urais wa Zanzibar na kueleza imani ya jeshi hilo kutokana na utendaji wake wa kazi.

Alisema ana matumaini makubwa kwa Dk Mwinyi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar, na alimpongeza kwa busara zake katika kuleta maridhiano hali itakayozidisha maelewano sanjari na kudumisha amani na umoja nchini.

Alimhakikishia Rais Mwinyi kwamba JWTZ itaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha amani inadumishwa katika maeneo yote nchini ikizingatiwa kwamba yeye mwenyewe ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama.

Katika hatua nyingine, Dk Mwinyi alikutana na Askofu Michael Henry Hafidh na kumpongeza na waumini wa Kanisa la Anglikana kwa kuendelea kuiombea nchi amani.

Dk Mwinyi pia alipongeza juhudi za uongozi wa kanisa hilo la kutaka kujenga chuo cha amali Kisiwani Pemba na pia azma yao ya kutaka kuwekeza katika eneo la Kiungani Zanzibar.

Askofu Hafidh alimpongeza Rais Mwinyi kwa ushindi alioupata na kueleza matumaini makubwa waliyonayo wananchi wa Zanzibar kutokana na uongozi wake. Pia alimpongeza kwa kuwepo kwa maridhiano na hatimaye kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ameiagiza  Wizara ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi