loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ubora barabara za kitaifa wafikia 87%

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Leonard Chamuriho amesema ubora wa mtandao wa barabara za kitaifa umeimarika hadi kufikia wastani wa asilimia 87 na za wilaya kufikia asilimia 56.

 

Barabara hizo zimeendelea kuimarika kwa wastani huo katika kipindi cha kati ya mwaka 2015/16 hadi 2019/2020.

 

Akizungumza katika kikao cha pili cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Chamuriho alisema hali hiyo ya kuimarika kwa barabara imetokana na mtiririko mzuri wa fedha kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara (RfB) kwenda kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

 

Aidha, Chamuriho alisema jana jijini Dodoma kuwa wizara hiyo imeendelea kuzisimamia taasisi zake ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kikamilifu kwenye miradi iliyokusudiwa.

 

“Katika mwaka wa fedha 2020/21, wizara hiyo imeidhinisha mpango wa manunuzi wa Tanroads kwa ajili ya miradi 56 ambapo kati ya hiyo miradi 41 ni ya barabara, miradi 11 ya viwanja vya ndege, miradi mitatu ya ujenzi wa madaraja pamoja na mradi mmoja wa ujenzi wa mizani,” alisema.

 

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema hadi Desemba mwaka jana, wakala huo ulipokea Sh milioni 226.6 kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara ambayo ni sawa na asilimia 40 ya bajeti ya mwaka 2020/21.

 

Akifunga kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Anne Kilango Malecela aliitaka wizara hiyo isimamie kwa karibu suala la magari yanayozidisha uzito kwa kuwa yamekuwa yakichangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi.

 

“Hadi sasa eneo la mizani bado halijasimamiwa vizuri na hivyo juhudi ziongezwe ili kuhakikisha magari yanayozidisha uzito, kwani fedha zinazopatikana kutokana na faini ya kuzidisha uzito wa magari barabarani hazitoshi ukilinganisha na uharibifu mkubwa wa barabara unaofanywa na magari hayo,” alisema Malecela.

 

Wizara kupitia taasisi zake iliwasilisha taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa za utendaji kutoka Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).

SERIKALI imeiruhusu sekta binafsi kuingiza nchini matrekta madogo ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi