TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imesema dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi (ARVs) zimesaidia kupunguza idadi ya vifo vya watu wanaoishi na ukimwi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids Dk Leonard Maboko alisema hayo jana mjini Morogoro kwenye ufunguzi wa warsha ya watekelezaji wa afua za ukwimu kwa fedha za mzunguko wa kwanza wa mfuko wa ‘Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS’ kwa asasi za kiraia 20 ambazo zitapatiwa jumla ya Sh milioni 543.6.
Tume hiyo kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) imeanzisha mfuko huo muhsusi kwa ajili ya mapambano dhidi ya ukimwi kwa kushirikisha wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali.
Dk Maboko alisema miaka 10 iliyopita zaidi ya watu 85,000 walikuwa wanakufa kutokana na ukimwi, lakini sasa vimepungua hadi 27,400 kutokana na matumizi ya dawa za ARVs na kati ya hao watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni 21,500 na watoto ni 5,900 ambazo ni takwimu za mwaka 2019.
Alisema watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini ni wastani wa milioni 1.7, kati yao watu wazima wenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea ni wastani wa milioni 1.6 na watoto ni wastani wa 90,000 na waliopo kwenye matumizi ya ARVs ni wastani wa watu milioni 1.3.
Kuhusu maambukizo mapya ya virusi vya ukimwi, Dk Maboko alisema kipindi cha miaka 10 iliyopita yalifikia wastani wa watu 130,000, lakini sasa yamepungua.
Alisema utafiti uliofanyika mwaka wa fedha 2016/2017 uliweka makisio ya watu 72,000 wanaambukizwa virusi vya ukimwi kila mwaka nchini.
Hata hivyo, alisema katika makadirio ya mwaka 2019 ilionekana kwa mwaka watu 77,000 walikuwa wanaambukizwa virusi hivyo kila mwaka.
“Kwenye idadi hiyo watu wazima wenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea ni 68,400, wakati watoto chini ya umri wa miaka 15 ni 8,600 amabo wanakuwa wameambukizwa maambukizo mapya kila mwaka na hivyo kupata jumla ya wote 77,000,” alisema.
Dk Maboko alisema mfuko huo awamu ya kwanza utawezesha asasi za kiraia 20 kutoka mikoa 11 ziweze kutekeleza mpango huo ikiwamo huduma na matunzo kwa watu wanaishi na virusi vya ukimwi na huduma za kinga.
Eneo lingine ni utoaji elimu ya masuala ya afya kwa vijana, misaada kwa watoto walio katika mazingira magumu (hatarishi), kupambana na unyanyapaa na ubaguzi, kutoa elimu kwa watoa huduma majumbani na elimu ya matumizi sahihi ya ARVs.